Kibaha. Serikali imekuja na mpango maalumu wa kuwanoa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, lengo wawe na ujuzi utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa mfumo mmoja tofauti na ilivyo sasa.
Wahudumu wa afya ya jamii wamekuwa wakipatikana kwa kupewa mafunzo na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na wengine na halmashauri kulingana na mahitaji yaliyopo kwa wakati huo, jambo ambalo limekuwa likisababisha wengi wao kukosa baadhi ya stadi za kazi.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Juni 10,2024 na Mratibu wa mpango wa Taifa wa huduma za afya ngazi ya jamii kutoka Wizara ya afya, Dk. Meshack Chinyuli wakati wa kikao kazi cha wataalamu wa afya kilichofanyika Kibaha Mkoa wa Pwani.
“Kutakuwa na hatua mbalimbali za namna ya kuwapata wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwanza yatatolewa matangazo ili waombaji wajitokeze kulingana na vigezo ambavyo watajadiliwa na maeneo wanakotoka, kisha majina yao kufahamika Tamisemi,” amesema.
Amesema baada ya hatua hiyo, wahudumu hao watapelekwa vyuo mbalimbali ambako watasoma kwa miezi sita wakipata ujuzi ndipo watakapoanza kutekeleza majukumu yao kwa jamii.
Amesema hali hiyo itaboresha utendaji kazi kwa wahudumu hao, kwani wote watakuwa na uelewa mmoja nchi nzima kwa kuwa Serikali imeshaandaa masomo watakayosoma na kuhakikisha wanafikia kiwango stahiki.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Tamisemi, Zainabu Kitembe amesema kupatikana kwa wahudumu hao hakuondoi nafasi za wale waliokuwepo ambao hawakupitia mpango huo na badala yake wataendelea kutoa huduma hadi miaka mitano ijayo.
“Kuna wahudumu wa afya ambao wapo na hawakupatikana kupitia utaratibu huu mpya na baadhi yao wapo ambao vigezo vinawashinda, ili kwenda kusoma miezi sita hao wataendelea kuhudumu hadi miaka mitano ijayo,” amesema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk Benedict Ngaiza amesema wameopokea mpango huo na kwamba watahakikisha taratibu zote zinafuatwa katika utekelezaji wake.
“Kwa Mkoa wa Pwani tuna jumla ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii 123 ambao miongoni mwao wapo wanaojihusisha na masuala ya wagonjwa wa kifua kikuu, Ukimwi na wengine wanahudumia watu wenye magonjwa yasiyopewa kipaumbele, lakini sasa utaratibu huu mpya utawaweka wote kwa pamoja, kwani watapata mafunzo ya aina moja na kuwa na ujuzi wa kufanya kazi zote,” amesema.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Dk Kandi John amesema mpango huo utaongeza ari ya kutoa huduma za afya kwa kundi hilo kwa kuwa watakuwa rasmi tofauti na ilivyo sasa, ingawa wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kwa jamii.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge akifungua kikao hicho amewataka watendaji ndani ya mkoa huo kuhakikisha watafuata taratibu zilizowekwa, ili kufanikisha mpango huo.