Moshi/Dar. Nini hasa kimewasukuma Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, wasaidizi wake wizarani na vigogo wa Jeshi Polisi kukaa kitimoto kipindi hiki?
Hili ndio swali linaloibua mjadala nchini licha ya nia ya kikao hicho kuelezwa bayana, na mambo sita yametajwa kuwa huenda yamewasukuma kukaa na kukuna vichwa kuhusu mambo yanavyokwenda huku vidole vikinyooshwa upande wao.
Kikao cha vigogo hao kimeketi wakati yakiwepo madai ya kuongezeka kwa matukio ya utekaji, mauaji na watu kupotea, sakata la wananchi wa Ngorongoro, matukio ya ubakaji na ulawiti na ukiukaji wa haki za binadamu na za wanasiasa.
Mbali na hayo, huenda suala la maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 nalo likawekewa mikakati ya namna ya kuimarisha ulinzi na usalama.
Miongonui mwa vigogo waliokaa na Masauni jijini Dodoma Agosti 27 ni Naibu wake, Daniel Sillo na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillus Wambura.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, kikao hicho kimehusu mambo yanayohusu usalama na amani ya nchi ikiwemo kujadili matukio ya kiuhalifu yanayotokea sehemu mbalimbali nchini na hatua zinazochukuliwa kuendelea kudhibiti matukio hayo.
Wengine walioshiki kikao hicho ni Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Maduhu Kazi na makamishna wa polisi, Suzan Kaganda (Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu), Liberatus Sabas wa Fedha na Lojistiki, Awadhi Juma Haji (Operesheni na Mafunzo), Shabani Hiki (Sayansi ya Uchunguzi wa Jinai), Ramadhani Kingai, Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai (DCI) na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.
Wakati Masauni na vigogo wa polisi wanakutana kujadili hilo, suala la utekaji na kupotea kwa watu jana liliiibuka bungeni baada ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenan kuomba mwongozo wa Spika ili Bunge lilijadili na kutoa maelekezo kwa Serikali ili haki ya kuishi iendelee kupatikana.
Ingawa haikuwekwa bayana kama utekaji na kupotea kwa watu ni miongoni mwa agenda, lakini wachambuzi wa haki za binadamu na wanaharakati wanaona hilo ni moja ya mambo yanayosababisha hali iwe tete.
Wakati vigogo wenye jukumu la kulinga usalama wa raia na mali zao wanakaa kitimoto, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga Agosti 28, 2024 kutoa uamuzi kuhusu maombi ya dhamana au kufikishwa mahakamani vijana watatu wakiwemo viongozi wawili wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema – Bavicha) – Deusdedith Soka, Jacob Mlay na Frank wanaodaiwa kushikiliwa kizuizini kwa siku 10 mpaka leo na polisi wanaoshtakiwa hawajasema kama wanawashikilia.
Katika mazingira hayo, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kijamii na kisiasa wametamani jeshi hilo litumie kikao hicho kujitathmini, kufanyia kazi malalamiko yaliyo ili kurejesha imani ya wananchi.
Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, amesema kupitia kikao angependa kuona Jeshi la Polisi likirudisha imani kwa jamii ambayo kwa sasa amedai imeshuka.
“Watanzania wana hamu ya kutaka kuliamini Jeshi la Polisi, ningetamani kikao hicho kirejeshe imani, ningetamani wakimaliza basi imani ya wananchi ambayo ipo chini irejee upya,” amesema Dk Bagonza.
Amesema mtu anayehamia au anayekwenda mtaa fulani afahamike kwenye ofisi ya kijiji akisema kwa sasa watu wanaingia na kutoka kwenye mitaa bila viongozi wa mitaa/mabalozi kujua.
Watanzania wasikie matokeo
Akizungumzia kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga amesema baada ya kikao hicho, Watanzania wangependa kusikia au kuona Jeshi la Polisi likija na mkakati utakaowezesha kupatikana suluhisho la vitendo vya utekaji, watu kupotea, kubakwa au kukatwa mapanga.
“Tunahitaji kusikia suluhu ya majanga yanayotukumba, ikiwemo mtu anapotea siku 29, siku ya 30 polisi wanasema walikuwa naye, tunataka kujua kwa nini yanatokea hivi, watu wanachinjwa ovyo au kutekwa.
“Waje na suluhu wanakuja na mkakati gani, kuna wakati walinihoji nikawaambia tuje na mkakati wa dharura na wa muda mrefu, ili kukomesha haya mambo yanayozidi kutokea kwa siku za hivi karibuni. Polisi ije na mipango inayotekelezeka, sidhani kama wanashindwa kwa sababu wana ujuzi na kila kitu,” amesema Henga
Umuhimu wa jeshi la polisi kuja na mkakati unatokana na ukweli kwamba kwa muda sasa, halijatoa kauli yenye mashiko kuhusu matukio mbalimbali ya hivi karibuni.
Mathalan, Agosti 9, 2024, Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) lilitoa tamko likilalamikia ongezeko na vitendo vya utekaji na kupotea kwa watu.
Takatika taarifa yake chama hicho mbali na kuambatanisha orodha ya watu 83 kilichodai walitekwa, kuteswa au kupotea kati ya mwaka 2017 hadi sasa, kilieleza kusikitishwa na matukio hayo na kikayalaani vikali.
Chama hicho kilisema mara kwa mara Jeshi la Polisi limekuwa likikanusha kutokea kwa matukio hayo lakini baadaye inakuja kubainika kwamba matukio hayo ni ya kweli, hivyo kililitaka jeshi hilo kutimiza wajibu wake wa kulinda raia na mali zao.
Vilevile, TLS ilimshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume Maalumu ya kuchunguza matukio yote ya kupotea kwa kutekwa, kutekwa na kuteswa na pia kuunda Tume ya kuchunguza ushiriki wa Jeshi Polisi katika masuala ya utekaji.
Pamoja na hayo, TLS ilipendekeza kuundwa kwa chombo maalumu (oversight body) cha kudumu cha kuangalia utendaji wa vyombo vya dola ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa kuzingatia Katiba na Sheria za Nchi na kwa kufuata maadili.
Kabla ya vumbi la TLS halijatua, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe Agosti 22, 2024 alizungumza na wanahabari akawataja baadhi ya maofisa wa polisi kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam akidai wanahusika na kikosi cha utekaji.
Katika maelezo yake ambayo pia hajajajibiwa, Mbowe aliungana na TLS kumtaka Rais Samia aunde Tume ya majaji kuchunguza watu kutekwa, kuteswa na kupotea kwa watu.
Aliyasema hayo akiwa ameambatana na familia za watu ambao wanadai ndugu zao walitekwa au kupotea.
Tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (TBUB) inayoongozwa na Jaji Mathew Mwaimu, nayo imeingia mzigoni kufuatilia kilio cha utekaji na watu kupotea nchini na imetangaza kuzunguka mikoa 15 ya Tanzania Bara yalikotajwa matukio yapatayo 80 ili kutafuta ukweli.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mwaimu aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma Agosti 22, 2024, tume hiyo inafanya uchunguzi katika mikoa ya Dar es Salaam, Singida, Mara, Shinyanga, Mwanza, Kagera, Geita, Kugoma, Tanga, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Arusha, Ruvuma na Rukwa.
Mapema leo Agosti 27, 2024 mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Mbunge Khenan ameomba mwongozo wa Spika ili chombo hicho kijadili masuala hayo na kutoa maelekezo kwa Serikali ili haki ya kuishi iendelee kupatikana.
Mbunge huyo amesema kumekuwa na matukio ya utekaji, upoteaji na mauaji kwa watoto, wanaharakati, wanasiasa na makundi mengine.
“Kwa kuwa jambo hili limeshazungumza na taasisi mbalimbali ambazo wameshafanya tathmini, Tume ya Haki za Binadamu, TLS pamoja na vyama vya siasa ikiwemo Chadema, jambo hilo lina masilahi na linaumiza Watanzania na Bunge liko kwa ajili ya Watanzania, hivyo limuunge mkono.
Akijibu mwongozo huo, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema mambo aliyozungumza mbunge huyo ya kuuawa, kupotea na kutekwa kwa watu ni mazito na kuwa taasisi alizozitaja, yeye (Spika) hajazisikia wala kupitia taarifa zao.
Hivyo, Spika alisema kwa jambo hilo, kama uchunguzi umefanyika au unapaswa kufanywa, basi si mtu kama yeye kusimama na kusema kuna mtu sijamuona ama akasema mtu huyo ameuawa.
Dk Tulia amesema pamoja na uzito wa mambo hayo, Serikali ichukue hatua zile inazochukua na kama zile za kawaida zinashindikana basi iongeze nguvu kwenye kuhakikisha raia wanakuwa salama.
Uchaguzi, Ngorongoro, Simiyu
Mbali na matukio hayo ya utekaji na kupotea kwa watu, baadhi ya wachambuzi wanaona suala la uchaguzi mkuu wa serikali za mita, hali inayoendelea Ngorongoro na katika mikoa mbalimbali kama Simiyu ambako wananchi waliandamana kutokanana kutorishwa na utendaji wa polisi, huenda ikawa moja ya agenda za kikao hicho.