Shangazi mbaroni akituhumiwa kumuua mtoto wa kaka yake

Njombe. Watu wawili Furahini Kipela (50) na Josephat Kiduligo (48), wanaoishi Mtaa wa Mapinduzi, Kata ya Lyamkena, Halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi  kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mtoto Wilson Kipela (5).

Mtoto huyo ni wa kaka yake Furahini Kipela.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 27, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Banga amedai kuwa watuhumiwa hao wawili walishirikiana kutekeleza mauaji hayo kwa kumpiga mtoto huyo baada ya kutoka kunywa pombe usiku wa kuamkia Agosti 26, 2024, wakiwa nyumbani kwao.

Kamanda Banga amedai licha ya wote wawili kutajwa kuhusika na tukio hilo, mtu wa mwisho aliyekutwa akitekeleza mauaji hayo ni Furahini Kipela, ambaye ni shangazi wa marehemu. “Mtoto huyu aliyekuwa mgonjwa, alishambuliwa na shangazi yake, Furahini Kipela, akiwa na mshirika wake, Josephat Kiduligo,” amedai kamanda huyo.

Amedai kitendo kilichofanywa na watuhumiwa hao hakiwezi kuelezwa tu kwa sababu ya ulevi, bali kuna uwezekano wa imani za kishirikina kuhusika.

“Haiwezekani watu wakamuua tu mtoto ambaye hajawakosea jambo lolote, kuna kitu cha ziada, tunawashikilia na tunaendelea kuwahoji kabla hatujawafikisha mahakamani,” amesema Kamanda Banga.

Akizungumzia mauaji hayo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mapinduzi, John Mligo amesema alipofika nyumbani kwa watuhumiwa alizikuta chupa mbili za bia.

“Pale nilichobaini ni ulevi, maana nilipofika nilikuta chupa mbili za bia na watu wenyewe wamelewa. Marehemu alikuwa akiishi Igwachanya na mama yake na alipokuja hapa alikuwa kwa upande wa baba yake,” amesema Mligo.

Amesema kwa kuzingatia busara alizonazo Furahini, ni vigumu kuamini kuwa angeweza kufanya kitendo cha namna hiyo.

“Hakuna anayeamini kama ametekeleza hili na mauaji haya yameleta taharuki mtaani hapa,” amesema Mligo.

Amesema mtaa huo uliweka sheria kuwa wanawake hawapaswi kukaa kwenye vilabu vya pombe baada ya saa 12 jioni, licha ya kwamba vilabu hivyo vinafungwa saa nne usiku. Kutokana na tukio hili, amepanga kuzungumza na vyombo vya usalama ili kuhakikisha sheria hiyo inafuatwa kwa nguvu zaidi.

Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mapinduzi, akiwemo Joyce Mdugo, amesema, “ukatili kama huu unatuumiza sana, hasa sisi akina mama. Ulevi mpaka kusababisha kifo ni jambo la kusikitisha sana na tunataka sheria ifuate mkondo wake.”

Mtoto wa mtuhumiwa Furahini, Suzana Malekela ameiomba Serikali kumsamehe mama yake akisema kuwa tukio hilo lilitokea bila kukusudia.

“Tunaomba jamii itusaidie, mama hakukusudia kufanya tukio hili. Hata sisi katulea hivihivi akiwa anakunywa pombe,” amesema Malekela.

Related Posts