Wasira: Tuchague watu wanaokubalika, wasiwe wapenda rushwa

Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewatahadharisha wanachama wa chama hicho kuchagua watu wanaokubalika lakini wasiwe wapenda rushwa.

Wasira ametoa tahadhari hiyo jijini Dodoma leo Jumanne, Februari 4, 2025 alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kongamano la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) ambalo linakwenda sambamba na maandalizi ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Kongamano hilo, lililohudhuriwa na wanawake kutoka sehemu mbalimbali za nchi, lilijikita kujadili changamoto na fursa zinazohusiana na usawa wa kijinsia na jinsi wanavyoweza kushiriki zaidi katika uongozi na maendeleo ya Taifa.

Wasira ametoa wito kwa wanawake kuendelea kujitokeza kwa wingi katika nafasi za uongozi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wakuu wa CCM kutoa kauli hiyo, mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi katika nyakati tofauti wamekemea mambo ya rushwa.

Hata hivyo, Wasira amesema mikusanyiko na mikutano inayoendelea ya chama hicho, siyo kuanza kwa kampeni bali wanafanya alichokiita ku-test mitambo.

Amesema yeye (Wasira) ni mwenyekiti wa kamati ndogo ya maadili kwa muundo wa Katiba ya CCM, hivyo watu wanaokiuka maadili watakutana naye.

“Tunataka watu wachaguliwe ambao wanakubalika, na ninyi mkaangalie hilo siyo kuchagua watu wanaodhani uongozi ni kununua, tambueni siyo kila kitu kinanunuliwa, hata mapenzi hayanunuliwi ndiyo maana dereva wa bodaboda anaweza kumnyang’anya tajiri mke,” amesema.

Makamu mwenyekiti huyo, amesema uchaguzi wa mwaka huu kwenye kura za maoni ni kuwachuja wagombea na kubaki watatu ambao watakwenda kushindanishwa.

Pia, amesisitiza viongozi kushuka ngazi ya chini kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kama wanavyofanya viongozi wa juu kwa ngazi ya Taifa.

Akizungumzia kauli hiyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Wakili Fredrick Kalonga amesema ni haki kuzungumza kwa sababu CCM ililalamikiwa kwa rushwa kwenye chaguzi za ndani.

Kalonga amesema chama hicho huenda kimesoma alama za nyakati kwamba walikuwa wakibeba viongozi walionunua madaraka.

“Wakitoa fedha na kushinda chaguzi za ndani, huko nje wanakutana na ugumu kwani wanakuwa na bidhaa isiyonunulika kwa watu, kwa mtindo huu wanaweza kupata watu ambao itakuwa rahisi kuwanadi,” amesema Kalonga.

Kwa upande wake, Dk Nchimbi amewataka wanaCCM kutokuwadharau wagombea wa vyama vingine kwa udogo wao hata kama watafanana na sisimizi.

Dk Nchimbi ambaye Mkutano Mkuu wa CCM wa Januari 19, 2025 ulimpitisha kuwa mgombea mwenza wa kiti cha urais, amesema wakati wote katika chaguzi ambazo amekuwa akishinda hupata nguvu kubwa kutoka kwa wanawake kwa kuwa, wakiamua huwa hawarudi nyuma.

“Kushinda tutashinda, lakini lazima tushirikiane na tusidharau mgombea yeyote kama ni sisimizi lazima tujipange ili tushinde kwa kishindo,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema kwa upande wake ni mtetezi na mpenda haki za wanawake na ndiyo maana akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alianzisha dawati la jinsia kwa vituo vya polisi, hivyo hatawatupa.

Related Posts