Dar es Salaam. Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeita wawekezaji wa Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuwekeza kwenye hatifungani za miaka 20 huku ikiahidi riba ya asilimia 15.25 kila mwaka.
Taarifa iliyotolewa na BoT Februari 13, 2025 katika tovuti yake inaonyesha kuwa, Serikali inahitaji kukusanya Sh224.88 bilioni kwenye mnada wa ushindani utakaofanyika Februari 19, 2025.
“Mnada huo utakaofanywa kupitia Benki Kuu ya Tanzania unatarajia kukusanya Sh224.88 bilioni kwa ajili ya zabuni shindani na ziada ya Sh11.84 bilioni itatengwa kwa wazabuni wasio na ushindani,” inaeleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo inaeleza kuwa hatifungani hizo za miaka 20 zinatarajiwa kuiva Februari 20, 2045.
“Wawekezaji wanatakiwa kuwasilisha zabuni mtandaoni kupitia taasisi washiriki (CDPs) kabla ya saa 5:00 asubuhi katika tarehe ya mnada,” inaeleza taarifa hiyo.
BoT inaeleza kuwa, kiwango cha chini cha uwekezaji katika hatifungani hizo ni Sh1 milioni.
Pia, mnada huo utasajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) sambamba na ule wa pili utakaoanza Februari 21, 2025.
BoT imetangaza kuwa hatifungani hizo zinaweza kushindaniwa na mtu yeyote ambaye ni mkazi wa nchi Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Mchumi, Rosemary Malalo amesema hatifungani hizo za muda mrefu zinaweza kuwa mkakati wa kuongeza uwekezaji wa ndani na kudhibiti athari za mfumuko wa bei kwa wawekezaji wa muda mrefu.
“Riba ya asilimia 15.25 kwa hatifungani ya miaka 20 ni nzuri ukilinganisha na viwango vya mfumuko wa bei vya sasa. Hii inawapa wawekezaji fursa ya kupata faida bila kuhofia kuyumba kwa thamani ya pesa yao katika kipindi kirefu,” amesema Rosemary.
Kwa upande wake, Mack Patrick ambaye ni mtafiti wa masuala ya uchumi, amesema ujumuishaji wa wawekezaji kutoka EAC na SADC unaweza kusaidia kuongeza mtaji wa kigeni nchini.
“Hatua ya kuruhusu wawekezaji wa EAC na SADC ni ya kimkakati kwa sababu itasaidia kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa nje, ambao wanaweza kuleta mtaji wa kigeni na kusaidia uthabiti wa soko la fedha la Tanzania,” amesema Patrick.