Zanzibar, Februari, 2025 – Airtel Afrika imeingia kwenye ushirikiano na wadau wa muziki kukuza vipaji vya muziki Afrika kupitia teknolojia ya mawasiliano ya intaneti ya kasi ili kuhakikisha wasanii wanafikia ndoto zao.
Kampuni hiyo ilidhihirisha dhamira hiyo kwa kushirikiana na jukwaa la Trace Awards and Summit 2025 iliyofanyika The Mora visiwani Zanzibar kuanzia Februari 24 hadi 26.
Jukwaa la Trace Awards2025 lilizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ambae aliahidi kuwa serikali iko tayari kutoa mchango kwa sekta ya muziki kwa kuwaunga mkono wasanii na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya ukuaji wa sekta hiyo.
“Tunaamini katika nguvu ya sekta ya burudani katika kuchochea mabadiliko. Muziki ni nyenzo muhimu katika uwezeshaji, kukuza utalii, kuleta maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii. Pia nachukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wadau wote waliofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tukio hili linafanyika kwa mafanikio,” alisema Mwinyi.
Akizungumza kuhusu ushiriki wa Airtel Africa kwenye tuzo hizo, Mkurugenzi wa Masoko wa Airtel Tanzania, Timea Chogo alibainisha kuwa hatua hiyo inatokana na dhamira ya Airtel kuhakikisha inatoa fursa kwa kila mtu kuweza kufikia ndoto zake.
“Kufanyika kwa tamasha pamoja na utoaji tuzo za TraceAward2025 visiwani Zanzibar kunatengeneza fursa za kiuchumi na kuendelea kuwafungulia dirisha wasanii wetu kimataifa. Ni jambo lakufursahisha mwaka huu tunafanya tamasha Tanzania tukiwa na wasanii tisa wanaowania tuzo hizi. Hii ni sababu tosha kwa Airtel kuweza kushiriki kuungana na wasanii hao kupitia muunganiko wa kibunifu na mtandao ili waweze kuusambaza muziki wao ndani na nje ya Tanzania,” alisema Chogo.
Kwa upande wake, Balozi wa Airtel Tanzania, Diamond Platnumz alisema; Trace awards inajumuisha watu wote kutoka Afrika na nje ya Afrika wanakuja hapa.
“Trace awards imeleta watu wote kutoka Afrika na nje ya Afrika kukutana hapa. Uwepo wa Airtel unasaidia watu waliokuja kwenye tuzo hizi waweze kuunganishwa na data na kupata huduma zingine zitakazowasaidia kuwasiliana na ndugu na jamaa na kuwawezesha kufanya biashara na hali kadhalika kushare maudhui yao na wasanii wengine.”,” alisema Diamond Platnumz.