Aliyebeba kibuyu tukio la Muungano azikwa, Shoo ataka umakini kwenye elimu

Hai. Wakati Sifael Shuma (92)aliyekuwa mmoja wa vijana wanne walioshiriki tukio la kuchanganya udongo, Aprili 26,1965,akizikwa nyumbani kwake Machame, Wilaya ya Hai, Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo ameiomba Serikali kuwekeza katika sekta ya elimu na kuhakikisha wanazalishwa vijana wenye elimu bora. 

Dk Shoo amesema katika kuyakumbuka maisha ya Sifael,  tunapaswa kujiuliza kuhusu aina na  ubora wa elimu inayotolewa kwa vijana wa Tanzania.

Askofu Fredrick  Shoo akiuombea mwili wa Sifael Shuma kabla ya kupelekwa makaburini.

Sifael alifariki dunia Februari 20,2025, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu, amezikwa leo Februari 26, nyumbani kwake, Machame, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Katika ibada hiyo ya mazishi iliyofanyika Usharika wa Nkwarungo, Dayosisi ya KKKT, imehudhuriwa na mamia ya waombolezaji na viongozi wa Serikali wakiongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza.

Wazee wa kanisa la  Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Nkwarungo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wakiupeleka mwili makaburini.

Kifo cha Sifael, kimefunga ukurasa wa vijana wanne, wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Tanganyika, walioshiriki tukio la kuchanganya udongo, ikiwa ni ishara ya muungano wa nchi hizo mbili na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vijana wengine walioshiriki tukio hilo ambao walishafariki ni Hassan Omar Mzee (aliyefariki dunia Agosti 28, 2024 akiwa na umri wa miaka 76) na Khadija Abbas Rashid (aliyefariki dunia Agosti 22, 2023 akiwa na umri wa miaka 74) wote kutoka Zanzibar na Hassaniel Mrema (aliyefariki dunia Mei 4, 2024 akiwa na umri wa miaka 80) na Sifael waliotoka Tanganyika.

Kwa mujibu wa historia Hassaniel Mrema na Hassan Omar Mzee ndio walioshiriki kushika chungu kilichowekwa udongo wa nchi hizo mbili, huku Khadija na Sifael wakibeba vibuyu vilivyokuwa na udongo wa nchi hizo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza, akiweka shada la maua kwenye kaburi la Sifael Shuma.

Akizungumza katika ibada hiyo Askofu Shoo amesema katika kuenzi maisha ya Sifael, Serikali inapaswa kuwekeza katika elimu na kuhakikisha inawathamini na kuwajali walimu.

“Huyu mama alitambua kwa kipawa na nafasi aliyompa Mungu ya ualimu, akatumika vyema kuwajengea uwezo wasichana wa nchi hii na vijana wengine. Alipambana kwa nafasi yake ya kuwa mwalimu, alijitoa na akaitumia nafasi yake vizuri” amesena Dk Shoo na kuongeza:

“Sisi wa sasa tuna wiwa kujiuliza sana kuhusu aina ya elimu na ubora wa elimu tunayotoa kwa vijana wetu wa Tanzania leo hii, tunapaswa kujiuliza tunaweka kipaumbele gani katika kuhakikisha vijana wetu wanapata elimu iliyo bora.”

Amesema pamoja na jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya shule na madarasa hata sasa anafikiri walimu wanastahili kuangaliwa zaidi kwa kuwa wajibu wao ni mkubwa katika kuzalisha vijana wenye elimu bora.

“Kweli shule zimejengwa nyingi, madarasa yamejengwa mengi na kwa hili tunaipongeza Serikali kwa jitihada zinazofanyika, lakini ukiangalia hakuna walimu wa kutosha, kutoka kijiji changu tu hapo ng’ambo shule nzima ya msingi ina walimu wanne, niambie hao walimu watajizungushaje kwenye hayo madarasa yote,” amesema.

Jeneza lenye mwili wa Sifael Shuma likishushwa kaburini.

Akihubiri katika ibada hiyo, mkuu wa pili wa jimbo la Hai la KKKT, Mchungaji Dominick Mushi amesema matendo mema  ni akiba na ushuhuda unaoishi na kutoa wito kwa Watanzania kutumikia vyema na kuepuka vitendo vya ubinafsi na kujilimbikizia mali.

Amesema baada ya mama Sifael kufariki, anakumbukwa kwa matendo yake mema katika jamii na Taifa, hivyo ni wakati wa kila mmoja kutafakari wakati akiondoka duniani ataacha alama gani na atakumbukwa kwa lipi.

Ametoa wito kwa Watanzania kusimama vyema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, na kuhakikisha wanapatikana viongozi ambao watalipenda na kulibeba Taifa la Tanzania.

“Mama huyu alisimama kwa uadilifu katika nafasi aliyokuwepo, nawe umepewa nafasi ya kutumika kama mkuu wa mkoa, waziri au nafasi nyingine katika jamii,  unatumikaje kwa ajili ya watu wengine.

“Na kwa wakati huu tunapenda watu ambao wanalipenda Taifa letu, huyu mama aliipenda Tanzania, alilipenda Taifa, alikuwa mzalendo kwa Taifa lake. Leo tunashuhudia roho ya ubinafsi, roho ya kujilimbikizia, roho isiyoangalia miaka mitano Watanzania watakuwa wapi miaka 20 ijayo Taifa letu litakuwa wapi,” amesema Mchungaji Mushi.

Akitoa salamu za Serikali, Khamis Hamza amesema mama Sifael alikuwa kielelezo kwa Taifa, jasiri na wakati wote alisimama kuulinda na kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar lilifanyika Aprili 26,1965 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Muungano ambapo wakati huo mama Sifael alikuwa na umri wa miaka 32.

“Tumeondokewa na mzalendo, kwani kukubali kushiriki kwenye kuunganisha nchi hizi ni kitendo kimoja cha uzalendo sana. Lakini alikuwa jasiri na tayari kueleza ukweli na uhalisia wa Taifa hili tulipo, tunakotoka na tunakoendelea na alikuwa mjenga historia,”amesema.

Related Posts