Dk Biteko awataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi kutatua kero za walimu

Geita. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk  Doto Biteko amewaagiza wakurugenzi na wakuu wa wilaya nchini,  kuanzisha utaratibu wa kukutana na walimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili,  badala ya kusubiri malalamiko hayo kufika ngazi za juu kwa utatuzi.

Uamuzi wa Naibu Waziri Mkuu,  umetokana na taarifa ya timu ya Kliniki ya Samia ya kusikiliza na  kutatua kero za walimu,  kubaini matatizo mengi yanayowakabili walimu,  yangeweza kutatuliwa kwenye halmashauri lakini hayafanyiwi kazi.

Amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto za walimu kwakuwa nchi zote duniani zilizofanikiwa,  ziliwekeza kwenye elimu,  na ili liwe na Taifa lenye maendeleo lazima wawepo walimu bora.

“Taifa linalopiga hatua kwenye maendeleo lisiache kuwekeza kwenye elimu na hasa  utatu wake  kwa maana ya mitaala, utahini na udhibiti ubora. Kwenye mnyororo wote huo,  huwezi kufanikisha elimu kama huna mwalimu bora aliyemotishwa na anayependa kazi yake,”amesema.

Amesema kliniki hiyo inawakumbusha walimu kuwa wao ni nguzo muhimu ya Taifa na kuwataka walimu kutoa shida zao kwa haki na uwazi,  kwakuwa Serikali ndio yenye dhamana ya kusimamia maslahi ya wengi.

Akizungumzia changamoto za walimu zilizotatuliwa mkoani Geita, Dk Biteko  amesema kwa kipindi cha miaka minne ya awamu ya sita,  walimu 5,061 wamelipwa madai yao yenye thamani ya Sh4.6 bilioni yakiwemo malimbikizo ya mshahara.

Aidha Sh2.2 bilioni zimelipwa kwa ajili ya uhamisho kwa walimu 1028 ,walimu 1839 wamepandishwa madaraja walimu 876 wamebadilishiwa muundo wa utumishi .

Kwa kipindi cha miaka minne Sh4.2 bilioni zimelipwa kama malipo ya likizo,   huku Sh25 milioni  zikilipwa kama malipo ya matibabu pale ambapo bima haikufanya kazi.

Awali Katibu Mkuu wa Chama cha walimu Tanzania (CWT) Joseph Misalaba amesema kliniki hiyo imeanzishwa ili kusikiliza na kutatua changamoto za walimu, na  imetokana na ziara ya kwanza ya Oktoba 2024 jijini mwanza ikihusisha maofisa utumishi kutoka ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma,  kubaini changamoto nyingi za kiutumishi kwa walimu.

Amesema katika ziara hizo walibaini walimu nchini wana changamoto nyingi za kiutumishi zinazomhitaji mwajiri mkuu,  hivyo walimu kulazimika kusafiri hadi Dodoma ambapo ni gharama na matokeo yake wengi hubaki na changamoto zao bila kuzipatia ufumbuzi

Mkuu wa Mkoa wa Geita,  Martine Shigella akizungumza kwenye kliniki hiyo amesema mbali na changamoto za kiutumishi kwa walimu,  pia zipo za kimfumo ambazo zimewafanya walimu kuingia kwenye matatizo hasa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Mfumo wetu wa Nest una masharti magumu walimu wamesomea ualimu sio uhasibu,  wanahitaji kujengewa uwezo  maana wanapokosea kwenye mfumo wa ununuzi,  wanajikuta kwenye mikono ya Takukuru, ”amesema Shigella.

Related Posts