Baada ya kucheza mechi nane mfululizo za Ligi Kuu bila kupata ushindi, Fountain Gate leo Februari 26, 2025 imeuona mwezi baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati.
Bao pekee la ushindi la Fountain Gate limefungwa na Amos Charles kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 27.
Penalti hiyo imepatikana baada ya beki Michael Ismail kumfanyia faulo Salum Kihimbwa ndani ya eneo la hatari la Tanzania Prisons.
Matokeo hayo yameifanya Fountain Gate kufikisha pointi 25 ambazo zimeitoa katika nafasi ya 13 iliyokuwepo kabla na kuisogeza hadi nafasi ya nane.
Kwa Tanzania Prisons, matokeo hayo yameifanya ibakie katika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi zake 18 ilizokusanya katika mechi 21.
Kabla ya kupata ushindi leo, Fountain Gate mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa ni Desemba 13, 2014 ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union.
Baada ya hapo ilipoteza mechi sita na kutoka sare mbili.
Nuksi ya Fountain Gate ambayo leo imehitimishwa ilianzia kwa kichapo cha mabao 2-0 mbele ya Azam FC, ikafungwa mabao 2-1 na Namungo na kisha ikachapwa mabao 5-0 na Yanga.
Baada ya hapo ikatoka sare ya bao 1-1 na Simba, ikafungwa mabao 2-0 na KenGold, ikachapwa mabao 3-0 na Kagera Sugar, ikalazimishwa sare tasa na Tabora United na ikafungwa bao 1-0 na Dodoma Jiji.
Kichapo cha leo mbele ya Fountain Gate kimeifanya Tanzania Prisons ikose ushindi katika mechi tano mfululizo za Ligi Kuu.
Timu hiyo tangu ilipopata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa, Februari 6, 2025, imepoteza mechi nne kati ya tano na imepata sare moja.