Dar es Salaam. Ilianza kama ndoto za kufikirika, ahadi, mipango na sasa imetimia. Ingawa bado inaenda ‘mdogomdogo’, lakini kipenga kimeshapulizwa kuruhusu biashara kufanyika kwa saa 24 katika eneo la Kariakaoo jijini Dar es Salaam.
Kariakaoo iliyokuwa ya biashara mchana usiku viunga vya malazi ya wasio na makazi maalumu, kwa sasa inaanza kubadilika kuwa eneo la mauzo na manunuzi ya bidhaa kutwa na kucha bila kusimama.
Ingawa hatua hiyo inakabiliwa na maswali kadhaa hasa kuhusu ulinzi na usalama na uzoefu wa wafanyabiashara wenyewe, lolote linaloshuhudiwa kwa hatua za awali, linasawiri msemo wa ‘mwanzo mgumu.’
Hata hivyo, wafanyabiashara wamepokea hatua hiyo kwa mtazamo chanya, huku wakipendekeza soko lililojengwa upya lifunguliwe ili kuchochea pilikapilika saa hizo 24.
Hatua hiyo ni mkakati wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyetangaza mpango wa shughuli za biashara kwa saa 24, akiamini zitakuza uchumi na kurahisisha huduma za upatikanaji bidhaa.

Chalamila alifanya uzinduzi huo Jumatatu, Februari 24, 2025 akisema mpango hyuo unakwenda sambamba na utendaji wa maeneo mengine ya kibiashara, ambayo yamekuwa yakifanya kazi muda wote kama — Bandari, Uwanja wa Ndege, Stendi ya Magufuli na treni ya kisasa ya SGR.
Mwananchi limeweka kambi katika eneo hilo usiku wa kuamkia leo, Jumatano Februari 26, 2025 kushuhudia mwanzo wa utekelezaji wa mpango huo.

Kilichoonekana dhahiri si maduka yote yaliyokuwa wazi katika soko hilo, mengi yalifungwa jioni kwa maana ya kuendelea kwa utaratibu wa siku zote.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara ambao, Mwananchi imezungumza nao, wamesema hawakuzoea kufanya biashara saa 24 katika soko hilo.
Mitaa mingi iliyozoeleka kuwa na hekaheka za watu majira ya mchana kama Msimbazi na Congo na mingine jirani ilionekana imepoa na hakukuwa na kinachoendelea.
Maduka mengi yalifungwa kati ya saa 4 na tano usiku na kwa wachuuzi wanaouza bidhaa za kumwaga chini, shughuli zao zilikoma saa sita usiku.
Hali ilikuwa tofauti katika mtaa wa Sikukuu ambako muda wote watu walipita huku na kule na biashara kadhaa, hasa za kubadilisha fedha, ziliendelea usiku wote. Maeneo ya mvinyo na kumbi za starehe, mambo yaliendelea kama kawaida.
Ingawa hawakuonekana askari waliovalia sare kwenye maeneo hayo, hali ya usalama ilikuwa shwari, watu walitembea mitaani bila shida.

Ingawa awali baadhi ya wafanyabiashara walionesha wasiwasi kuhusu hali ya usalama, Chalamila aliwaondoa wasiwasi kwa kutoa kauli ya kuwaonya vibaka kutothubutu kuifanya sehemu ya majaribio yao.
Akieleza sababu ya kutaka Kariakoo kufanya kazi saa 24 juzi, Chalamila alisema mbali ya kuongeza mapato na ajira, pia ni kwenda sambamba na maeneo mengine ya kibiashara, ambayo yamekuwa yakifanya kazi saa hizo.
Vyombo vya usafiri wa umma, vilionekana kwa uchache, hasa pikipiki na bajaji za kwenda maeneo kama Mbezi, Kimara, Tegeta na Mwenge, ingawa si kwa idadi kama inavyokuwa mchana.

Si magari ya mwendokasi wala daladala yaliyoonekana kufanya shughuli zake muda wote na maeneo mengi yalionekana vizuri kutokana na uangavu uliotokana na taa zilizofungwa eneo hilo.
Baadhi ya wafanyabiashara na wateja waliozungumza na Mwananchi wameeleza maoni na kile walichokishuhudia huku wakitaka subira ili kufikiwa malengo.
Mjasiriamali wa vifaa vya kielektroniki anayefanya shughuli zake mkabala na Soko Kuu la Kariakoo, Mrisho Maeda amesema kufanya shughuli hizo usiku kucha bado ni changamoto.
“Soko hili likifunguliwa linaweza kutupatia matumaini ya kuwa na mzunguko wa watu wengi wanaoingia sokoni kununua bidhaa na kutoka, inaweza kutushawishi kuendelea kufanya kazi muda wote lakini kama hawatafungua itakuwa shida,” amesema.
Maeda ambaye anasema shughuli zake huwa anafungua kuanzia jioni kila siku na kufunga saa 4 usiku, amesema ni kama Serikali haijajipanga.
Kwa upande wa mjasiriamali anayeuza vyombo Mtaa wa Sikukuu, amesema hadi anakutana na mwandishi wa Mwananchi saa 5 usiku, hakuwa ameona wateja, hivyo ameamua kufunga shughuli zake.

“Nimeamua kufunga muda huu kwa sababu sijaona wateja, nafikiri watu wengi hawajafikishiwa taarifa au hawajazoea utamaduni huu mpya ila natumaini kadiri siku zinavyokwenda wataanza kuzoea,” amesema.
Amesema Watanzania waliowengi hawana utamaduni wa kufanya biashara usiku kwa kuwa unakuja utaratibu mwingine, itachukua muda kuwa hali ya kawaida.
Omary Kiuta amesema pamoja na kwamba utaratibu huo ni mzuri, itachukua muda na viongozi lazima wakubali kutumia muda mwingi kuwaelewesha.
“Watu wakielewa itakuwa fursa kwa wafanyabishara kwenye kupandisha mauzo ya siku, lakini hata wateja wanaotoka nje ya nchi watakuwa wanachukua bidhaa na kuondoka usiku kwa usiku,” amesema.

Gilibert Renard, amesema shughuli hizo zikifanyika saa 24 hata ajira zitaongezeka kwani kuna baadhi ya wafanyabishara watalazimika kuajiri vijana wanaoingia mchana na wengine usiku.
Mamalishe katika soko hilo, Jasmine Abdallah amesema yeye ni desturi yake kuuza chakula hadi saa sita usiku wa kila siku.
Amesema kufanya kazi kwa saa 24 Kariakoo ni suala la muda hadi pale watu watakapozoea.
“Kwa leo wateja wangu ni walewale wa kila siku, sijaona mtu mpya, ninachoamini watu bado hawajazoea na wakizoea nitakuwa napika hadi asubuhi,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi amesema ni mwanzo mgumu lakini ni imani yake watafika kulingana na azma ya Serikali.
“Tunachohitaji ni mazingira rafiki, taa ziongezwe ndiyo maana unaona baadhi ya maeneo mwanga si wa kuridhisha, lakini tunahitaji njia ziwe wazi ukiangalia watu wamepanga mizigo barabarani ni lazima ziwe wazi ili watu wawe huru,” amesema.
Katika maelezo yake, amependekeza kwa kuiomba Serikali kuharakisha mahitaji muhimu kama ufungaji wa kamera na taa ili kuende sambamba na ufanywaji wa shughuli saa 24.

“Jamii yenye inahitaji kuendelea kuhamashishwa na kupewa elimu ni imani yangu huu ni mwanzo na ni utamaduni mpya itachukua muda kuzoea lakini tutafika,” amesema.
Tatizo la kufurika kwa chemba eneo la Kariakoo bado linaonekana mfupa mgumu licha ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) kueleza mikakati yake katika kutatua tatizo kuanza kwa Kariakoo ya saa 24.
Hii ni baada ya Mwananchi leo Jumatano Februari 26, 2025 kushuhudia chemba ikiwa imefurika maji mtaa wa Mkunguni eneo ambalo shughuli za uzinduzi wa Kariakoo ya saa 24 zikiwa zinaendelea.
Leo ikiwa ni siku ya pili ya uzinduzi huo ambapo kutakuwa na utoaji elimu kuhusu maboresho hayo ya ufanyaji biashara na semina mbalimbali kuhusu ulipaji kodi, ukataji bima za majengo, uanzishaji jina la kampuni na biashara na fursa za kuweza kufikia mikopo, shughuli ambazo zinafanyika Mtaa wa Mkunguni.
Pamoja na shughuli hiyo kuwekwa hapo, kumeonekana chemba inayotiririsha maji eneo ambalo kumefungwa jukwaa maalumu kwa ajili ya shughuli za utoaji burudani.
Baadhi ya wafanyabiashara akiwemo Hassan Nkya, amesema hali hiyo kwa Kariakoo ni jambo la kawaida na hawajui litaisha lini.
Nkya amesema anachokiona ni mifumo ya upokeaji maji taka imezidiwa, kwa kuwa Kariakoo ya miaka 60 iliyopita.

Naye Mwajuma Heri, amesema hali huwa mbaya zaidi kipindi cha mvua na ameomba mamlaka zinazohusika kushughulikia kwa haraka tatizo hilo kabla mvua hazijaanza kunyesha.
“Mchana maji unayaona unayaruka, sasa Karikaoo inaenda kuwa ya saa 24, si tutakuwa tukikanyaga vinyesi huku na ukizingatia na mvua ndio hizo zinakuja, mamlaka zitimize majukumu yake na wasisubiri hadi mlipuko wa magonhwa utokee,” amesema Mwajuma.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuwa wamejipanga kulishughulikia ikiwemo kuongeza mashine za kuzibulia.
Ukiacha kuongeza mashine, Everlasting amesema wameamua kufungua mabwawa yao ya kumwagia maji machafu ya Vingunguting na Buguruni saa 24 kutoka saa 16 walizokuwa wanafanya kazi awali.
“Vilevile kituo chetu cha huduma kwa wateja kilichopo Upanga kitakuwa wazi saa 24 na tuna magari sita ambayo muda wowote yatapatikana maeneo hayo, endapo kutatokea tatizo iwe rahisi kufika,” amesema.
Kuhusu chemba kuzidiwa nguvu kutokana na kuongezeka kwa majengo na watu, msemaji huyo amesema sio kweli kwani kwa namna zilivyotengenezwa bado zina uwezo mkubwa wa kupokea uchafu na kuwa tatizo wanaliona kwa wamiliki wa majengo ambao wakiboresha nyumba zao wanaacha mfumo uleule wa maji taka.
“Tunaomba wenye nyumba wanapomoa hasa kuzibadili nyumba za familia kuwa za biashara, waje tuwape ushauri namna ya kufunga mifumo yao ya maji safi na maji taka ili kwa pamoja tuweze kupunguza tatizo hili la kufurika kwa chemba Kariakoo,” amesema Evalasting.
Kwa mujibu wa msemaji huyo mpaka sasa Dawasa ina zaidi ya chemba 5,000 katika maeneo hayo ya Kariakoo.
Imeandikwa na Tuzo Mapunda, Sute Kamwelwe na Nasra Abdallah