Kilimo cha kutegemea mvua chaathiri umwagiliaji

Unguja. Serikali imekiri mpaka sasa wanatumia kilimo cha kutegemea mvua za msimu na kuathiri uzalishaji wa kilimo.

Hata hivyo, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo inaendelea na jitihada za kuongeza ukubwa wa maeneo ya kilimo cha umwagiliaji.

Hayo yamesemwa na waziri wa wizara hiyo, Shamata Shaame Khamis leo Jumatano Februari 26,205 katika mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Amesema kuongeza ukubwa wa maeneo na mifumo ya kilimo cha umwagiliaji maji itawasaidia wakulima kupunguza utegemezi wa kilimo cha kutegemea mvua. 

Waziri Shamata amesema Serikali imeongeza ukubwa wa eneo la umwagiliaji kutoka ekari 2,187.5 mwaka 2019 ekari 5,750  mwaka huu. 

“Hili ni ongezeko la eneo la ukubwa wa ekari 1,425 kwa kilimo cha umwagiliaji maji ambacho kinamwezesha mkulima kulima mara mbili kwa mwaka,” amesema Shamata.

Amesema, uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka tani 1.5 kwa heka kwa mwaka kwa kilimo cha kutegemea mvua hadi wastani wa tani 11 kwa heka kwa mwaka kwa kilimo cha umwagiliaji.

“Nikubaliane na mjumbe kwamba asilimia kubwa ya kilimo chetu bado ni cha kutegemea mvua za msimu, hivyo kuathiri uzalishaji wetu, hata hivyo wizara inaendelea na jitihada za kutekeleza maagizo ya Serikali ya kuongeza ukubwa wa maeneo na mifumo ya kilimo cha umwagiliaji,” amesema Shamata. 

Amesema kilimo cha umwagiliaji kinasaidia kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji.

Katika matarajio ya kuendeleza kilimo hicho na kutokana na umuhimu wake wizara inaendelea na jitihada za kuyaendeleza maeneo ya umwagiliaji maji hasa kukarabati na kujenga miundombinu mipya.

Awali, Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir alihoji ni lini Serikali itaondokana na kilimo kutegemea mvua huku akitaka kujua tathmini ya kilimo hicho cha mvua za msimu.

Related Posts