WAFANYABIASHARA zaidi ya 50 wanadai kutishiwa kuondolewa kwenye majengo ya wakfu wanayofanyia biashara kutokana na deni la kodi ya pango, ambayo wamesema walilipa kwa kamati ya mpito ya Msikiti wa Ijumaa Jijini Mwanza.
Wakizungumza na waandishi wa habari, leo wafanyabiashara hao wamesema wanakabiliwa na changamoto ya kufukuzwa kutokana na kudaiwa kodi ya pango,tayari baadhi wamepewa ilani (notice) ya kuondoka na wameiomba serikali iwasaidie wasiondolewe katika nyumba za wakfu wanazofanyia biashara.
Wafanyabiashara hao wamedai kwamba walilazimika kulipa kodi ya pango mikononi kwa viongozi wa kamati ya mpito ya msikiti, badala ya kulipa kupitia mifumo rasmi ya benki na kisha kuwasilisha pay inslip wapewe stakabadhi.
“Viongozi wa Kamati ya Mpito walitutaka kulipa fedha za kodi mkononi wakidai akaunti za msikiti zimefungwa, wana shida ya kulipa mishahara na huduma zingine.Awamu ya pili walikuja na hoja hiyo hiyo wakiongozana na madalali,wakatishia atakayekaidi kulipa watamwondoa,”amesema Abass Omary
Ali Mukoko amesema ni mhanga mkubwa,baada ya kulipa benki sh.milioni 10 za kodi ya miaka miwili (2024 na 2025), alifungiwa biashara kwa miezi sita ikiwemo kufunguliwa kesi mahakamani,na hakupewa stakabadhi wala mkataba wa upangaji, anadaiwa kodi ya miaka miwili ya nyuma iliyolipwa kamati ya mpito kwa fedha mkononi.
“Wapo wapangaji wanadaiwa hadi milioni 42.Bodi mpya haitambui malipo yaliyofanywa mkononi na fedha haikuingizwa benki,hivyo tunaiomba serikali itusaidie maana tuliowalipa fedha hizo wapo na wanafahamika kwa majina,”amesema.
Aidha,Wilfred Were,amesema wafanyabishara hawana ugomvi,kwa sababu fedha za pango wanazodaiwa waliilipa kamati ya mpito na kupea stakabadhi, hivyo wanaomba warudishwe waendelee kufanya biashara ili kulinda mitaji yao,kwani baadhi wamekopa benki.
“Kamati ya mpito ya Msikiti wa Ijumaa inatajwa kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za Msikiti wa Ijumaa,wafanyabiashara tulilipa fedha mikononi badala ya kupitia mifumo benki,bodi haitambui madeni tuliyolipa mkononi na kamati ya mpito haionekani,tunashindwa tuwapate wapi.Kwa vile suala hili liko TAKUKURU watusaidie ili tujue hatima yetu,”amesema Mandela Andrew.
Naye Shujaa Abdallah, amesema kamati ya mpito ilikuja na utaratibu wake na hawakuwa na uwezo wa kupinga na ndiyo sababu walilazimika kulipa fedha mkononi badala ya benki na kuiomba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, iwasaidie wapate haki yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Adhamini wa Msikiti wa Ijumaa, Abdallah Amin Abdallah ,akizungumzia kadhia hiyo amesema baada ya bodi yao kuvunjwa mwaka 2019, ikaundwa kamati ya mpito na kutambulishwa kwa wapangaji wakaelekezwa wasilipe fedha mkononi.
Amesema kuwa waliwashauri wapangaji hao wawatafute waliowapa fedha mkononi ama wazipeleke wenyewe (kamati ya mpito) benki, watuletee slip tuwape stakabadhi waendelee kufanya biashara.
“Sisi hatuna ugomvi nao tunasimamia maagizo ya serikali.Kabidhi Wasii Mkuu,aliagiza wakalipe kielektroniki.Wakachukue hatua ya kuwatafuta na kuwafungulia mashitaka waliowakabidhi fedha.Kama sikosei suala hili liko TAKUKURU,tutawaondoa na huo ndio msimamowa bodi,”amesema Abdallah.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi, amekiri kwa simu kuwa kamati aliyoiunda ilibaini ubadhirifu wa fedha za Msikiti wa Ijumaa jijini Mwanza na kupeleka suala hilo kwa mamlaka za uchunguzi.