Rais Mwinyi: Uwekezaji umechochea sekta ya utalii

Unguja. Licha ya kuwapo madai kuwa hakuna faida zinazopatikana katika uwekezaji Zanzibar, Serikali imesema faida zipo na ndio sababu ya kuendelea kutoa kipaumbele cha miradi ya uwekezaji visiwani humo.

Hayo ameyasema Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo Jumatano, Februari 26, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa Hoteli ya Sandies Nungwi Beach, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk Mwinyi amesema miongoni mwa faida inayopatikana katika uwekezaji ni ongezeko la idadi ya watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani wanaofika kutembelea visiwa hivyo.

“Kwa hivyo, sisi hatuna budi kuendelea kusisitiza uwekezaji katika utalii ili nchi iweze kupata mafanikio kiuchumi,” amesema Dk Mwinyi

Amesema uwekezaji ndio chachu ya kuleta ajira kwa vijana ikiwemo wakati wa ujenzi wa miradi ya uwekezaji huo na baada ya kukamilika (vijana wataajiriwa kwenye uendeshaji).

Pia, amesema kupitia miradi hiyo Serikali inaendelea kupata kodi kutoka wawekezaji na wageni wanaofika visiwani humo kutalii ambapo watalipa kodi itakayotumika kujenga miundombinu ya nchi ikiwemo ya  afya, barabara, elimu, maji na umeme.

Amesema, hoteli hizo zinazojengwa Zanzibar zitawasaidia wajasiriamali wadogowadogo wanaotengeneza bidhaa kupata soko la bidhaa zao.

“Kila wawekezaji wanapokuja kuwekeza hapa nawasisitiza kuangalia changamoto ya wananchi katika maeneo yao uwekezaji na kuzitafutia ufumbuzi, lazima watoe huduma kwa wananchi,” amesema Dk Mwinyi.

Dk Mwinyi amesema, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa asilimia saba, na unaongozwa na sekta ya utalii ikifuatiwa na ya ujenzi.

Mbali na hayo, Dk Mwinyi ametoa shukurani kwa wawekezaji hao kuendelea kuichagua Zanzibar kwani ushindani ni mkubwa wa uwekezaji duniani.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohammed amesema jumla ya miradi 268 imesajiliwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, yenye thamani ya Sh3.75 bilioni, kati ya hiyo 106 imesajiliwa katika kipindi cha miaka mitano.

Mkurugenzi huyo, amesema mradi huo wa Sandies Nungwi Beach umewekezwa kwa dola za Marekani milioni 17, sawa Sh44 milioni.

Amesema, mradi huo unatarajiwa kutoa ajira 200 za moja kwa moja kwa wananchi wa kisiwa hicho hususan  wakazi wa eneo hilo ili kunufaika na miradi inayotekelezwa katika mkoa huo.

Related Posts