Sh1.4 bilioni kukwamua soko lililokwama kwa miaka 10 Mara

Tarime. Serikali imetoa zaidi ya Sh1.4 bilioni kukamilisha mradi wa ujenzi wa soko la kimkakati la kimataifa la mazao ya kilimo katika eneo la Sirari mkoani Mara, ambapo ujenzi wake ulikwama kwa takriban miaka 10.

Soko hilo linalotarajiwa kunufaisha wafanyabiashara wa mazao ya kilimo zaidi ya 300 linatajwa kuwa mwarobaini wa changamoto zinazowakumba wafanyabiashara hao.

Hii inatokana na kutakuwepo kwa soko la aina hiyo licha ya kuwa mpakani mwa Tanzania na Kenya hivyo kuwepo kwa fursa nyingi za biashara ya mazao.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa soko hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi aliyefanya ziara kukagua maendeleo ya mradi huo leo Jumatano Februari 26, 2025, Mhandisi kutoka kampuni ya Nice construction wanaotekeleza mradi huo, Samuel Lutaja amesema umefikia asilimia 69 unatarajiwa kukamilika Mei 2025.

Kuhusu malipo amesema tayari wamepokea zaidi ya Sh750 milioni kwa ajili ya utekelezaji na hadi sasa hakuna changamoto kubwa inayoweza kukwamisha mradi huo kukamilika kwa wakati.

“Tumeanza utekelezaji wa mradi Novemba mwaka jana na tunatarajia ifikapo mwishoni mwa Mei mwaka huu utakuwa umekamilika,”amesema Lutaja

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mtambi ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuanza mara moja mchakato wa kuwapata wafanyabiashara watakaofanya shughuli zao katika soko hilo.

“Mchakato uanze mara moja na kusiwepo upendeleo wa aina yoyote kwani miradi kama hii inatekelezwa na Serikali ili kuwanufaisha wananchi bila ubaguzi wowote, mradi huu unalenga kuwakomboa wananchi na sio kuwa mateso kwa wananchi,” amesema.

Amesema awali mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2013 na ilipofika mwaka 2014 utekelezaji wake ulisimama kutokana na kukosekana kwa fedha.

Amesema kutokana na umuhimu wa soko hilo kwa Mkoa wa Mara, Serikali mkoani humo ilianza mchakato wa kuomba tena fedha kutoka Serikali kuu ambapo mwaka jana Novemba Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

Mtambi ameziagiza mamlaka husika pia kuanza mchakato wa kufikisha huduma muhimu katika eneo hilo ikiwamo maji na umeme,  ili mradi utakapokamilika uanze kutumika mara moja bila kuwepo kwa kikwazo.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao katika mji wa Sirari wamesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira bora na salama.

Mataro Nyablangeti amesema kutokana na kutokuwepo kwa eneo maalumu kwa ajili ya biashara ya mazao ya kilimo wafanyabiashara hao mara kadhaa wamekuwa wakijikuta wakiingia katika migogoro na mamlaka za Serikali, kutokana na wengi wao kufanya biashara kwa njia zisizo rasmi.

“Kuna muda tunakamatwa kuwa tunatorosha mazao na nafaka lakini ukweli ni kuwa wengi wanafanya hivyo kwa sababu hakuna soko rasmi kwa ajili ya biashara hii, sasa soko likikamilika hii misuguano baina yetu na Serikali itamalizika rasmi,”amesema.

Anna Maira amesema soko hilo litasaidia kuongeza thamani ya biashara kwani   hawatalazimika tena kupeleka mazao na nafaka nchini Kenya, badala yake watakuwa na sehemu rasmi ya kuuzia.

Related Posts