Shahidi aieleza mahakama mtuhumiwa alivyokiri kumuua mpenzi wake

Moshi. Shahidi wa 11 katika kesi ya mauaji ya Josephine Mngara (30), aliyeuawa kwa kuteketezwa kwa moto, E7657 D/SGT Hassan ameieleza mahakama namna mshtakiwa Erasto Mollel alivyokiri kuhusika na mauaji ya mpenzi wake.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Februari 24, 2025 mbele ya Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi huku upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Kambarage Samson, Frank Ong’eng’a na Grace Kabu.

Mbali na mawakili hao, utetezi katika kesi ya mauaji namba 3382/2024, inayowakabili washtakiwa wawili, Erasto Mollel na Samwel Mchaki, unawakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Alfredy Sindato Silayo na Lilian Mushi.

Washtakiwa hao kwa pamoja, wanashtakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi, mwanamke huyo eneo la Mtemboni, Mji Mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Februari 19, 2023 kwa kumteketeza kwa moto.

Kwa mujibu wa upande wa mashitaka marehemu alikuwa akiishi na Mollel ambaye alikuwa ni mpenzi wake na aliuawa kikatili usiku wa kuamkia Februari 19, 2023 na mwili wake kuteketezwa kwa moto kwenye pagale kwa kile kilichodaiwa na Polisi kuwa ni wivu wa mapenzi.

Shahidi huyo ambaye ni Ofisa wa Polisi kitengo cha upelelezi, Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Moshi, ameieleza Mahakama hiyo kuwa, Mei 16, 2023 wakati akimuhoji mtuhumiwa alikiri na kueleza namna alivyoshiriki mauaji ya mwanamke huyo kwa kushirikiana na rafiki yake, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.

“Mei 16, asubuhi nikiwa kazini, niliitwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya, ASP Levina na kunipa jalada la kesi ya mauaji Him/IR/544/2023 na kwamba kuna mtuhumiwa mahabusu natakiwa nikamuhoji,”  ameeleza shahidi huyo.

“Nilimuita mtuhumiwa kwa majina yake, akaitika, baada ya kujiridhisha yupo, nikamjulisha msimamizi wa kituo kwamba kuna mtuhumiwa nataka kumtoa naenda naye kwenye mahojiano,” ameeleza mahakamani hiyo.

Amedai kuwa, baada ya kumtoa mahabusu alikwenda naye chumba maalumu cha mahojiano ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya.

“Nilimuuliza majina yake akaniambia anaitwa Erasto Gabriel Mollel, baada ya hapo nilimfahamisha kosa lake na halazimishwi  kutoa maelezo na maelezo yake atayaandika na yatatumika mahakamani kama ushahidi dhidi yake. Pia nilimueleza ana haki ya kumuita wakili na ndugu zake wawepo wakati wa kuandika maelezo yake,  lakini aliridhia kutoa maelezo yeye pekee na alisaini na kuweka alama ya dole gumba na mimi nikasaini”, amesema shahidi huyo.

Pia, ameieleza Mahakama hiyo kuwa, wakati anamuhoji mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo na akaridhia maelekezo yake yatumike kama ushahidi mahakamani.

Ameeleza kuwa,  katika mahojiano hayo alimweleza kosa analotuhumiwa nalo la kumuua mtu aliyekuwa akiishi naye kitongoji cha Mtemboni kama mume na mke aitwaye Josephine Dismas.

“Alikubali na akasema ni kweli alimpiga na kumuua na baadaye alimtafuta rafiki yake aitwaye Samweli (mshtakiwa wa pili) na kumpa taarifa hizo”, amesema na kuongeza:

“Baada ya kumwambia ameua walitoka wote pamoja mpaka eneo ambalo alifanyia mauaji nyumbani kwa Erasto walichukua mwili wakaweka kwenye godoro na nguo za marehemu wakapeleka nyumba ya jirani.”

Aliendelea kueleza kuwa, baada ya kufikisha kwenye hiyo nyumba ya jirani ambayo haiishi mtu walivunja kufuli la chumba kimoja ambacho kilikuwa na mbao na kuuweka ule mwili ukiwa umezungushiwa kwenye godoro ambapo walimwaga mafuta ya taa.

“Baada ya kumwagia mafuta ya taa kwenye ule mwili na zile nguo walifunga mlango na kufunga dirisha wakatoka pale ndani, wakazunguka nje dirishani Samweli aliwasha kiberiti na kutupia kwenye ule mwili,”ameeleza shahidi huyo.

Amedai kuwa, baada ya kutekeleza tukio hilo mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, alimtaka mshtakiwa wa kwanza aondoke kwenye hilo eneo na asionekane kabisa.

Hata hivyo, baada ya ushahidi wake, shahidi huyo aliomba Mahakama hiyo ipokee ushahidi wake  kama kielelezo katika kesi hiyo.

Hivyo, Jaji Kilimi alipokea kielelezo hicho kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo.

Maelezo ya shahidi wa 8, 9 na 10

Aidha, Shahidi wa nane E6548 D/SGT Rick ameieleza Mahakama hiyo kuwa Februari 21, 2023 jioni akiwa kwenye kituo chake cha kazi Himo, alipokea vielelezo kutoka kwa askari E 4525 D/SGT Ziadi vikiwa kwenye bahasha ndogo nne za kaki.

Shahidi huyo, ambaye ni mtunza vielelezo alidai vielelezo hivyo vilikuwa ni mfupa wa mkono wa kushoto wa binadamu, mfupa wa nyonga, jino la gego la binadamu, sampuli ya DNA, damu kavu iliyokuwa imechukuliwa ukutani na sakafuni, magome ya miti yaliyokuwa na damu iliyoganda, vyote alivikabidhi kwa askari E 4525 D/SGT Ziadi vikiwa vimefungwa kwenye bahasha.

Naye Shahidi wa tisa, kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai J3632 PC John alieleza Mahakama hiyo kuwa, mnamo Machi 14, 2023 akiwa ofisini Moshi, alifika Koplo Ziadi akiwa na vielelezo vya kesi ya mauaji Him/IR/5442/2023 na kumkabidhi ili vipelekwe ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA).

“Bosi wangu ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kilimanjaro, aliniambia nikague vizuri vielelezo hivyo na baada ya kuvikagua nilipata kibali cha safari kuelekea Dar es salaam, ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali,”

Shahidi wa 10, katika kesi hiyo, 4525 D/SGT Ziadi, kutoka kitengo cha upelelezi kituo cha Polisi Himo, alieleza mahakama hiyo namna alivyokusanya mabaki ya mifupa kwenye eneo la tukio na kuyaweka kwenye mfuko maalumu na kisha kupoleka hospitali ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu (postmortem).

Related Posts