Abiria afa safarini kwenye ndege, wana ndoa wasimulia magumu ya kusafiri na maiti

Doha. Safari ya ndege kwa wanandoa wawili Mitchell Ring na Jennifer Colin, waliokuwa wakitokea Australia kwenda Venice, Italia imegeuka ya huzuni baada ya abiria mmoja wa kike (jina halijaanikwa) kufariki dunia wakati ndege hiyo ikiwa angani.

Ring na Colin, waliokuwa wakisafiri katika ndege ya Shirika la Qatar Airways kwenda Venice kwa ajili ya mapumziko, waliiambia Televisheni ya Channel 9 ya Australia kwamba mwanamke huyo alifariki dunia karibu nao wakati wa safari kutoka Melbourne hadi Doha, wiki hii.

Wanandoa wawili, Mitchell Ring na Jennifer Colin, waliokuwa kwenye safari yao ya mapumziko, lakini safari hiyo iligeuka kuwa ya masikitiko baada ya abiria mmoja kufariki dunia angani.

Tukio hilo lilitokea wakati wa safari ya ndege ya Shirika la Qatar Airways kutoka Australia kwenda Venice, Italia.

Abiria huyo alikufa karibu na wanandoa hao, na mwili wake ulifunikwa na blanketi na kuwekwa kwenye kiti kilichokuwa kando ya Ring kwa saa nne za mwisho za safari hiyo, bila ya kuhamishiwa kwenye kiti kingine licha ya kuwapo kwa viti vilivyokuwa wazi.

Wanandoa hao walisema hawakupewa msaada wowote kutoka kwa Qatar Airways wala Qantas, ingawa walikuwa na wasiwasi na hali ya abiria aliyeaga dunia.

Ingawa mkewe, Colin alihamia kiti kingine cha jirani kilichokuwa wazi, Ring alisema hakupata nafasi ya kuulizwa ama kupewa chaguo la kuhamia kiti kingine licha ya viti vya wazi kuwapo.

Rubani wa zamani wa ndege za Shirika la Virgin Atlantic, Barry Eustance, alisema vifo angani hutokea mara nyingi zaidi kuliko watu wanavyofikiria lakini, kadri anavyojua hakuna taratibu maalumu zilizoainishwa kwa matukio kama hayo.

“Katika safari ndefu, inategemea zaidi ni lini na wapi tukio linatokea, na wahudumu wana vifaa gani vya kuweka mwili mahali salama kwa sababu ndani ya ndege hakuna njia ya kufikia sehemu ya mizigo.

 “Kuna eneo la mapumziko ya wahudumu, lakini hilo ni kwa ajili ya wafanyakazi kwa hiyo inaweza kuwa changamoto kuuweka mwili pale,” alisema.

Alisema eneo la choo ama sehemu ya maandalizi ya chakula linaweza kuzuiwa kwa muda, lakini wahudumu wana wajibu wa kuhakikisha kuna vyoo vya kutosha kwa abiria.

Hata hivyo, Eustance alisema, ingawa hakutaka kuhukumu kwa sababu hakuwa na taarifa kamili za tukio hilo, alishangazwa na hatua ya wahudumu kutomhamisha Ring ikiwa kulikuwa na viti wazi.

“Ningetarajia wahudumu kufanya kila wawezalo kuepuka hilo. Unaweza kuanzisha matatizo ya kisheria ya baadaye kutokana na mshtuko wa kihisia kwa watu walioketi karibu na mwili huo.

“Kulingana na uzoefu wangu, wahudumu kawaida hujaribu kutenga mwili ili kuhakikisha hakuna abiria anayekutana moja kwa moja na mwili huo kwa heshima, faragha, na sababu za kiafya. Mwili wa mtu aliyefariki dunia unapaswa kushughulikiwa kwa uangalifu kwa sababu kuna changamoto za kiafya pia.” alisema.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts