Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kuvunja mkataba na mwekezaji anayeendesha Bandari ya Malindi na kurudisha shughuli za uendeshaji wa bandari kwa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC).
Chama hicho kimedai mwekezaji huyo aliyekuwepo imeshindwa kuweka ufanisi wa bandari hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji, imezorotesha biashara na kuongeza gharama za maisha kwa wananchi wa Zanzibar inayotokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Ismail Jussa leo Alhamisi Februari 27, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya makao makuu ya chama hicho, Vuga.
Hata hivyo, Mwananchi alipomtafuta Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Mohammed kuhusu hoja za chama hicho, amesema hayupo katika nafasi nzuri kuyazungumzia hayo.
“Sipo katika position nzuri kwa sasa kuyazungumzia hayo,” amesema Waziri Khalid.
Jussa amesema wakati zikifanyika juhudi mpya za wazi na zinazofuata sheria kwa ajili ya kupata mwekezaji mpya atakayeendesha bandari ya Malindi na kufanya uwekezaji katika bandari hiyo na huduma zinazoambatana nazo, isimamiwe na ZPC.
Pia, amesema Serikali ichukue hatua za dharura na za haraka za kuhakikisha meli zote zilizopo bandarini zinapata nafasi ya kupakua mizigo na wafanyabiashara kupata mizigo yao.
“Mizigo hiyo ipatikane kwa wakati na kwa gharama nafuu ili kuwarahisishia wananchi wa Zanzibar upatikanaji wa mahitaji yao yote muhimu katika kipindi cha Mwezi wa Ramadhani,” amesema Jussa.
Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani unatarajiwa kuanza kati ya Machi Mosi au mbili.
Makamu huyo ametumia nafasi hiyo kuwapa pole wananchi kisiwani humo kwa kile alichodai kupitia matatizo na hali ngumu ya maisha yanayosababishwa na uamuzi mbaya unaotendeka.
Pia, Jussa amedai watu waache kutumia ofisi za umma kujinufaisha kwani mamlaka hizo ndio zenye jukumu la kulinda masilahi ya Taifa, kupambana na ufisadi sio kuwanyanyasa watumishi wa Serikali.
Amedai zaidi ya meli 16 zipo katika bandari ya Malindi zinasubiri kupakuliwa kwa zaidi ya wiki mbili.
Ameendelea kudai kuwa, malalamiko makubwa ya wafanyabiashara katika bandari hiyo ni ucheleweshwaji wa kutolewa makontena bandarini hapo hasa kipindi hiki cha kuelekea Mwezi wa Ramadhani na kusababisha hasara kwao.
Amedai kuwa huduma za ushushaji wa makontena hayo zimezidi kuzorota kwani kabla ya mwekezaji huyo kukabidhiwa mtu aliweza kutoa kati ya makontena 10 hadi 15 kwa siku, ila sasa kwa siku anatoa kontena moja.
Amesema, athari ya mwekezaji huyo inaonekana kwa wananchi kwani imevuruga hali zao kwa sababu wananchi wengi kisiwani humo wafanyabiashara na mzunguko wa fedha zao unategemea bidhaa hizo.
Amedai, gharama za kutoa mizigo bandarini (port charges) ambazo ziliahidiwa zitapungua zimeongezeka kutoka Sh450,000 hadi kufikia Sh870,000 kwa kontena moja.