Ajali ndege ya kijeshi yaua maofisa wa jeshi, raia 46 Sudan, mapigano yashika kasi

Khartoum. Watu 46 wamefariki dunia katika ajali ya ndege ya kijeshi ya Sudan iliyotokea katika eneo la Omdurman, Makao Makuu ya nchi hiyo, Khartoum.

Al Jazeera, imeripoti ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana Jumatano Februari 26,2025 ikihusisha ndege ya kijeshi aina ya Antonov, wakati wa kuruka kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Wadi Seidna uliopo Kaskazini mwa Omdurman jijini Khartoum.

Kwa mujibu wa Wizara ya Habari ya Sudan miongoni mwa waliofariki dunia katika ajali hiyo ni wanajeshi 17, wakiwemo maofisa wa ngazi za juu na raia 29.

Ofisi ya Habari ya Khartoum ilisema ajali hiyo pia imejeruhi watu wengine 10.

Meja Jenerali, Bahr Ahmed ambaye ni Kamanda Mwandamizi ndani ya Jeshi la nchi hiyo ni miongoni mwa waliofariki dunia katika ajali hiyo.

Jeshi la Sudan, ambalo limekuwa kwenye vita na Rapid Support Forces (RSF) tangu Aprili, 2023, lilitoa taarifa kuthibitisha wanajeshi na raia waliuawa katika ajali hiyo huku likieleza vikosi vya zimamoto vilifanikiwa kudhibiti moto eneo la ajali.

Taarifa hiyo haikutoa maelezo kuhusu chanzo cha ajali japo vyanzo vya kijeshi vililiambia shirika la habari la Reuters huenda ilisababishwa na matatizo ya kiufundi.

Wakazi wa kaskazini mwa Omdurman waliripoti mlipuko mkubwa uliotokana na ajali hiyo, ambayo iliharibu nyumba kadhaa na kusababisha kukatika kwa umeme katika vitongoji vya jirani.

“Hali ya ndege kuanguka muda mfupi baada ya kupaa inaonyesha kuwa RSF siyo waliohusika na shambulio hilo kwa sababu RSF hawapo katika eneo ambapo ndege hiyo ilianguka,” alisema Hiba Morgan wa Al Jazeera, akiripoti kutoka Khartoum.

Mapigano yanayoendelea nchini Sudan yamesababisha vifo vya maelfu ya watu huku chanzo chake kikitajwa kuanzia kwenye mvutano kati ya Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan na Kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Daglo kuhusu muundo wa Serikali ya baadaye ya taifa hilo.

Hivi sasa, jeshi linaendelea kupata mafanikio makubwa katikati mwa Sudan na Khartoum katika mashambulizi yake yanayofanyika maeneo mengi ya nchi hiyo  dhidi ya RSF.

Ajali ya ndege hiyo imetokea siku moja baada ya RSF kudai kuidungua ndege ya Russia aina ya Ilyushin huko Nyala, kwenye mji Mkuu wa Darfur uliopo Kusini mwa nchi hiyo.

Shirika la Chakula Duniani (WFP), ambalo ndilo mtoaji mkubwa wa misaada ya chakula nchini Sudan, mapema wiki hii lilisema kuwa limesimamisha ugawaji wa chakula katika kambi ya Zamzam, Kaskazini mwa Darfur huku raia wakikabiliwa na njaa kali.

Kambi hiyo imekuwa ikilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya RSF.

“Bila msaada wa haraka, maelfu ya familia zinazohitaji msaada Zamzam zinaweza kukumbwa na njaa katika wiki zijazo,” amesema Laurent Bukera ambaye ni Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa WFP na Mkurugenzi wa muda wa Shirika hilo nchini Sudan.

“Tunapaswa kuanza tena kusambaza msaada wa kuokoa maisha ndani na nje ya Zamzam kwa usalama, haraka, na kwa kiwango kikubwa. Ili hilo lifanikiwe mapigano lazima yakome na mashirika ya kibinadamu yapatiwe dhamana ya usalama,” Bukera alisema.

Jumatatu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionya kuhusu “kuongezeka kwa mzozo” baada ya RSF na washirika wake kutangaza kuwa wataunda serikali katika maeneo wanayodhibiti.

UN inasema kuwa mzozo huo umesababisha zaidi ya watu milioni 12 kuyakimbia makazi yao huku ukiacha mgogoro mkubwa zaidi, njaa na wakimbizi duniani.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts