AKILI ZA KIJIWENI: Prisons, Kagera zinahitaji maombi

TUWAWEKE kwenye maombi jamaa zetu wa Kagera Sugar na Tanzania Prisons maana kama bundi wa kushuka daraja anawanyemelea  kwa nguvu msimu huu.

Timu mbili ambazo ziliwahi kusumbua katika soka la Tanzania na kufanya timu vigogo ziugue pindi zinapokaribia kucheza nazo, leo zipo katika nafasi za hatari kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Ni tofauti ya pointi mbili tu ambayo imezitofautisha timu hizo ambapo Prisons ipo katika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi ikiwa imekusanya pointi 18 na tayari imeshacheza mechi 22.

Kagera wao wapo katika nafasi ya 15 na pointi zao 16 ambazo nao wamezivuna katika mechi 22 za ligi na hivyo wamebakisha mechi nane za kujitetea kwa kila timu.

Baada ya kufanya tathmini ya kisoka hapa kijiweni tumegundua kwamba timu hizo mbili zinaangushwa na usajili ambao zimeufanya msimu huu ambao ni wachezaji wengi wenye daraja na uwezo wa kawaida na sio wa juu wa kuzipa muendelezo wa kufanya vizuri timu hizo.

Tukategemea katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari timu hizo zingemwaga fedha kusajili wachezaji wazuri wa kuzitoa mahali zilipo na kuzisogeza juu lakini imekuwa tofauti na wengi mchango wao unaonekana kuwa mdogo.

Katika nyakati kama hizi tulitegemea kuona uongozi wa timu hizo ukitenga bonasi nono za fedha kwa wachezaji wao na mabenchi yao ya ufundi ili kuwaongezea zaidi hamasa ya kupambania nembo za klabu hizo.

Hata hivyo, hakuna kitu kama hicho na zinaonekana kama zimeshakata tamaa na ligi zinasubiria msimu uishe zikajichezee zao Ligi ya Championship baada ya kushuka daraja kujaribu kama zinaweza kurudi tena.

Inasikitisha kuona Kagera na Prisons zipo hapo zilipo kwenye msimamo wa ligi lakini kama zenyewe hazioni uchungu tuziache tu.

Related Posts