Aliyemuuza Mayele, amng’oa Mzize | Mwanaspoti

PALE Yanga kuna mastaa kibao wanaowaka kwa sasa wakipambana kulisaka taji la nne mfululizo la Ligi Kuu Bara msimu huu, huku wakiweka majina yao katika mizani ya kusakwa na timu za nje ya nchi kwa mkwanja wa maana.

Lakini, wakati unasoma hapa, nyota wa kikosi hicho aliyepandishwa kutoka timu ya vijana wakati wa kocha Nasrredine Nabi, Clement Mzize mambo yake ni bambam zaidi akitupia apendavyo nyavuni na kwa usomapo habari hii anaongoza msimamo wa wafunga Bara akiwa na mabao 10 sambamba na nyota mwenzake wa Yanga, Prince Dube pamoja na kiungo wa Simba, Jean Ahoua.

Katika anga za kimataifa, wakala aliyesimamia dili la kuuzwa kwa nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele kwenda Pyramids ya Misri amemchomoa Mzize kwa kutoa kauli ambayo itawapa presha mashabiki wa klabu hiyo, huku akimtaja Kibu Denis wa Simba.

Aliyeyasema hayo ni meneja wa Aziz KI, Pacome Zouzoua, Jean Charles Ahoua na wengine, Zambro Traore akikiri yeye ni shabiki mkubwa wa Mzize na kwamba kwa ofa alizonazo mshambuliaji huyo haoni kama atasalia Yanga msimu ujao.

Zambro alisema Mzize ana ofa nyingi za klabu za Kaskazini mwa Afrika na haoni kama klabu yake itaziacha kwa kumbakisha mwisho wa msimu.

Meneja huyo ameongeza kwamba klabu hizo zinafuatilia ubora wa mshambuliaji huyo kila akiwa uwanjani kuitumikia timu yake ambapo Yanga hata hivyo itavuna fedha nyingi kutokana na umri na ubora wa kinda huyo.

“Hapa Tanzania mchezaji wa kwanza wa Kitanzania ninayempenda ni Mzize (Clement) ni kijana mdogo lakini ana kipaji kikubwa sana, kiukweli sioni kama atabaki Yanga kwa msimu ujao,” amesema Zambro.

“Mimi ndiye nilisimamia dili la Mayele kwenda Pyramids nazijua klabu za Afrika Kaskazini hawatamuacha Mzize abaki Yanga. Kwanza ofa hizi ni kubwa sana na zinaweza kuongezeka kidogo sidhani kama klabu yake itaacha kumuuza.

“Unajua umri wa mchezaji na hata kiwango chake kwa wakati husika ndio vitu ambavyo vinazivutia klabu nyingi na wataendelea sana jambo zuri ni kwamba mchezaji bado yuko kwenye mkataba mzuri na klabu yake kwahiyo ni wazi Yanga itapata fedha nyingi.

Hadi sasa Mzize ameifungia Yanga mabao 10 katika Ligi Kuu Bara na asisti tatu, akichuana na nyota wengine wawili wa kideni akiwamo mshambuliaji mwenzie wa Yanga, Prince Dube na Ahoua wa Simba.

Kwa michuano ya kimataifa, Mzize ameifungia Yanga mabao matano kuanzia hatua ya awali hadi makundi ambapo timu hiyo iliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu uliiopita ndiye aliyekuwa Mfungaji Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) akifunga mabao matano.

Aidha Zambro alisema nje ya Mzize, nyota mwingine anayemkubali ni Kibu wa Simba akisema kiungo huyo mshambuliaji ni mchezaji mzuri mwenye nishati kubwa uwanjani.

Zambro amesema nishati ambayo Kibu anaitoa uwanjani sio kitu rahisi kocha yeyote kumuacha nje ambapo ana vitu ambavyo vitaisumbua timu pinzani.

Kibu alisajiliwa na Simba msimu wa 2021-2022 akitokea Mbeya City na misimu mitatu iliyopita ameifungia mabao 11 yakiwamo nane na msimu wa kwanza, mawili ya msimu wa pili na moja la msimu uliopita na hadi sasa hajaifugia bao katika ligi licha ya kutupia matatu katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Related Posts