Arusha. Madhara ya kuchukua Sheria mkononi. Ndicho kilichomkuta mkazi wa Mara, Rhobi Chacha, ambaye amekwaa kisiki Mahakama ya Rufani iliyobariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kuwauwa watu wawili waliotuhumiwa kwa wizi.
Tukio hilo lilitokea Aprili 28,2018 katika Kijiji cha Nyarwana wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, kundi la watu karibu 50 akiwemo Chacha wakiwa na panga, pinde, mishale na mikuki waliwakamata watu hao na kuwashambulia hadi kufariki dunia.
Licha ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Makende ambaye alikuwa shahidi wa tatu katika kesi ya msingi, Joseph Ryoba kujaribu kuwaokoa wananchi hao walimzidi nguvu.
Rhobi alishtakiwa kwa kosa la mauaji ya watu wawili ambao ni Marwa Ryoba na Otaigo Kinyang’ore.
Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walioketi Musoma, ambao ni pamoja na Barke Sehel, Lucia Kairo na Amour Khamis, wametoa hukumu hiyo Jumanne Februari 25, 2025 katika rufaa hiyo ya jinai namba 362 ya mwaka 2021.
Jopo la majaji hao baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, walieleza kuwa baada ya kuchunguza kumbukumbu za rufaa,wamebaini kwamba Otaigo na Marwa walikufa kifo kisicho cha kawaida na maswali yaliyopo ni iwapo mrufani alisababisha vifo hivyo.
Jaji Sehel amesema hiyo ni rufaa ya kwanza, hivyo wana haki kwa mujibu wa kanuni ya 36(1)(a) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania, kutathmini upya ushahidi huo upya na kufikia uamuzi wao.
Amesema kutokana na jumla ya ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu, wamejiridhisha kuwa mahakama ya awali ilikuwa na uhalali wa kutoamini utetezi kinzani wa mrufani.
Jaji Sehel amesema kesi ya upande wa mashtaka ambayo iliegemea zaidi ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa tatu na vielelezo vitatu vilivyowasilishwa ili kuthibitisha kosa la mauaji.
Amesema shahidi wa tatu alidai alipofika eneo la tukio, aliona kundi la watu wenye hasira kali akiwamo mrufani aliyekuwa ameshika panga.
Amesema wakati kundi hilo la watu wakiwavamia Otaigo na Marwa, alimuona mrufani akiwakata kwa panga mmoja baada ya mwingine.
Jaji Sehel amesema kuhusu hoja ya mrufani kutambuliwa eneo la tukio, wameridhika na kukubaliana na uammuzi wa Mahakama ya wali kwamba mrufani alitambuliwa na shahidi wa tatu katika eneo la tukio.
Hivyo, akasema wanatupilia mbali rufaa hiyo kwa sababu haina mashiko na hukumu iliyotolewa ni sahihi kwa vile ushahidi wa mashtaka umethibitisha makosa hayo bila kuacha shaka.
Rufaa hiyo inatokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma Juni 2, 2021 baada ya Hakimu kuongezewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Ilidaiwa siku ya tukio Ryoba, alipokea simu kutoka kwa mwenyektii wa Kijiji cha Nyarwana, John William, akimjulisha kuhusu tukio hilo.
Alimweleza kuna kundi la watu walikuwa wamezunguka nyumba ya mrufani ambayo ilikuwa haijakamilika, wakiwa na silaha hizo za jadi.
Shahidi wa tatu alidaiwa kujaribu kuwasihi wananchi wamsubiri Mwenyekiti wa Kijiji chao afike na alifika dakika 15 baadaye na Joseph na John walivunja mlango na kuwakamata watuhumiwa hao.
Wakiwa njiani kuelekea ofisi ya kijiji, mrufani alikatiza huku akisema anataka watuhumiwa hao wauawe kwa sababu ni wezi hivyo kifo ni stahili yao.
“Ndipo umati uliokuwa na hasira uliunga mkono msimamo wa mrufani wakaanza kuwarushia mawe na eenyeviti hao walikimbia na kuwaacha watuhumiwa wa wizi,” amesema shahidi huyo.
Shahidi wa tatu alidai kusimama umbali wa mita 20 na kushuhudia umati wa watu wenye hasira kali wakiwavamia watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi kwa kutumia mawe, mikuki na mapanga na washukiwa hao walijaribu kutoroka bila mafanikio.
Ilidaiwa Marwa alikimbilia nyumbani kwa Nossy lakini umati wa watu wenye hasira walimfuata na kumuua hapo hapo, kisha wakamfuata Otaigo ambaye alikuwa amejificha kwenye nyumba moja kuukuu, wakamtoa nje na kumuua karibu na nyumba hiyo.
Shahidi huyo wa tatu alidai kumwona mrufani akiwakata kwa panga lake watuhumiwa na kumsikia akisema wezi hao walimuibia, itabidi awaue na baada ya kuwaua, umati ule kila mmoja alikimbia.
Shahidi wa pili ambaye ni Ofisa Tabibu Msaidizi, Devotha Katunzi, alidai Aprili 29, 2018, aliufanyia uchunguzi mwili wa Marwa kichwani alikuwa na majeraha mengi sambamba na shingoni alikuwa na jeraha lililosababisha kuvunjika kwa mfupa wa shingo na ndiyo sababu iliyosababisha kifo chake kwa kuwa alivuja damu nyingi.
Tabibu huyo amedai Mei 2, 2018 aliufanyia uchunguzi mwili wa Otaigo na alibaini ana majeraha mengi kichwani na sehemu kubwa ya kidevu na chanzo cha kifo chake ni kupoteza damu na mshtuko wa moyo.
Mrufani huyo alikamatwa Aprili 28, 2018 na kupelekwa katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji kisha Kituo cha Polisi Tarime.
Katika utetezi wake, Rhobi alikiri kukamatwa na na kukana kutenda makosa hayo huku akidai siku ya tukio, saa 12 alfajiri alienda Kijiji cha Nyarwana na wakati wa tukio, alikuwa nyumbani kijiji kingine cha Weigita.
Aidha, mahakama hiyo ilikataa utetezi huo ikisema mrufani alishindwa kuwasilisha ushahidi wowote wa kuunga mkono hoja yake na iligundua kuwa mrufani alitambuliwa vyema na shahidi wa tatu katika eneo la uhalifu, hivyo imemtia hatiani na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.
Katika rufaa hiyo Rhobi aliwakilishwa na Wakili David Mahemba huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Charles Kagirwa na Janeth Kisibo.
Mrufani huyo alikuwa na sababu nne za rufaa ikiwemo upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kesi kwa kiwango kinachohitajika cha uthibitisho bila shaka yoyote.