Barua yawa gumzo Mchome, Chadema wavutana

Dar es Salaam. Kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lembrus Mchome ameendelea kuikalia kooni ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kile anachodai kushindwa kumpatia majibu ya barua yake, huku akisema amejipa saa 48 za kutafakari na kuja na hutua nyingine.

Barua hiyo aliyoiandika kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema na nakala kuituma Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa akipinga uteuzi wa viongozi wa juu na wajumbe wa kamati kuu ulioufanywa na Tundu Lissu Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.

Mchome, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, katika barua hiyo amesema uteuzi wa vigogo hao uliidhinishwa bila akidi ya kikao cha baraza kuu kutimia.

Kwa mujibu wa Mchome, viongozi waliopatikana katika utaratibu huo ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).

Katika barua hiyo, Mchome amesema wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala, akidai uteuzi wao ni batili.

Wakati Mchome akieleza hayo leo Alhamisi, Februari 27, 2025 alipozungumza na Mwananchi kuwa anatafakari cha kufanya baada ya muda alioutoa wa saa 48 kupita, Naibu Katibu Mkuu (Chadema) Bara, Amani Golugwa amemjibu akimtaka kutii alichoambiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na kuacha kujibishana na mtendaji kwenye vyombo vya habari kwani kwa kufanya hivyo ataonekana kama ana nia ovu.

“Aje achukue majibu kwani chama kina kazi kubwa za kufanya ikiwemo hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi na Watanzania wana hamu ya kuona mabadiliko, ilikuwa rahisi kama alivyoleta barua yeye hapa kwa nia njema tu basi aje achukue,” amesema.

Wakati pande hizo mbili zikizidi kuvutana kuhusu majibu hayo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo nayo ilitumiwa nakala ya barua hiyo ikizungumza na mwananchi kupitia kwa Naibu Msajili Sisty Nyahoza aliyejibu kwa kufupi,  “Hatujaona majibu.”   

Tangu Februari 18, 2025, Mchome alipowasilisha barua hiyo yeye mwenyewe makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam na kuituma ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kumekuwa na mijadala mikali ndani na nje ya chama hicho.

Jumanne Februari 25, 2025, Mchome alizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha alitoa saa 48 kuanzia siku hiyo akitaka kujibiwa kwa barua yake hiyo aliyodai akidi ya wajumbe wa baraza kuu ni wanachama 412 ambayo inayotakiwa angalau iwe na wajumbe 309 sawa na asilimia 75, lakini viongozi hao walipitishwa na akidi ya wanachama 85 tu sawa na asilimia 20.6.

Saa hizo 48 zimemalizika jioni ya jana Jumatano ambapo leo Alhamisi Februari 27, 2025 Mwananchi lilizungumza na Mchome likitaka kujua nini kinafuata baada ya kupita saa hizo ambapo amesema bado hajapata majibu yake pamoja na kutoa saa 48 , hivyo anaendelea kutafakari hatua za kuchukua ndani ya siku hizi mbili.

“Hadi sasa (saa 4.29 asubuhi) majibu ya barua yangu bado sijayapata, na saa 48 zimeisha jana jioni lakini nahitaji muda kidogo ili niweze kujua nini naweza kukifanya na baada ya hapo nitaongea na Watanzania ili wajue  hatua ninazoenda kuchukua,” amesema.

Katika maelezo yake Mchome amesema baada ya kuwasilisha pingamizi lake Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alitakiwa kumpatia majibu kulingana na anuani ya barua aliyowapatia lakini  hajajibiwa.

“Sijui kwa nini katibu mkuu anashindwa kunipatia majibu na anaenda kuandika mtandaoni bado sielewi maana ya katibu mkuu,”amesema.

Baadaye Mwananchi ilimtafuta Golugwa kujua jambo gani linakwamisha kumpatia majibu yake, ambaye alianza  kwa kusema hawawezi kufanyia kazi saa 48 aliyotoa na hawana msukumo wowote wa kikanuni na kisheria wa Mchome kutoa muda.

“Tulishamjulisha aje achukue majibu yake lakini tunashindwa kuelewa anuani yake ni wapi? Kwa sababu Mwanga hayupo, Kilimanjaro hayupo na tunashindwa kuelewa hasa yeye anaishi wapi?, anuani yake ni wapi,” amesema.

Aliporudiwa kwa mara nyingine Mchome na kumueleza kilichosemwa na Golugwa, amesema katibu mkuu wa chama hicho anajua yeye ni Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Mwanga kama walishindwa kufikisha Mwanga basi walipaswa kupitia ofisi ya mkoa wa Kilimanjaro.

“Wanaposema hawana anuani yangu nashindwa kuelewa namba yangu mbona wanayo na katibu mkuu hatujaanza kufahamiana leo anapajua hadi nyumbani kwangu ninapoishi,” amesema.

Mchome amesema anashindwa kuielewa ofisi hiyo kudai kwamba hayupo Mwanga ilihali yeye bado yupo sehemu hiyohiyo na anaendelea na shughuli zake.

“Golugwa nimefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka 10, ananifahamu na anajua ninapoishi na anazijua ofisi za chama wilaya ya Mwanga kwa sababu nilifanya naye kazi akiwa katibu Kanda ya Kaskazini anajua jinsi ya kunipata na namba yangu bado anayo,” amesema.

Baada ya majibu hayo ya Mchome Mwananchi ilimrejea tena Golugwa ambaye naye amejibu kwa kusema ugumu unaopitia ofisi hiyo ni namna ya kumpata na kumfikishia majibu kada huyo, huku akieleza kwa taarifa walizonazo Mwanga hayupo  na hawajui anapatikana wapi?.

“Kilimanjaro Moshi mjini hayupo hatujui anapatikana wapi, Arusha ambako tunaona anatoa matamko hatujui anapatikana wapi? Dar es Salaam hapa hatujui anapatikana wapi,” amesema.

Hata hivyo, jana Jumatano, kupitia mtandao wa kijamii X, Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika aliandika kuwa  Februari 24, 2025 alimtumia ujumbe Mchome kuwa majibu ya barua yake yako tayari aende akachukue ofisini kama alivyopeleka barua ya awali. “Akasoma ujumbe huo ukawa na blue tick na hakajibu.”

“Badala yake Februari 24, 2025 kutaka katibu mkuu amjibu ni kwa nini hakusema ukweli kuwa majibu yake yako tayari isipokuwa yeye mwenyewe hujayafuata au kupendekeza atumiwe kwa njia ipi mbadala? Ana nia gani kuendelea kusema uongo dhidi ya katibu na Chadema?,” alisema.

Related Posts