Katika maeneo mengi ya biashara, kumekuwa na tabia ya wateja kuombwa kulipa “ya kutolea” wakati wa kufanya malipo kwa njia ya mtandao wa simu. Huu ni msamiati ambao umekuwa maarufu, na ingawa umekubalika kwa kiasi fulani, hatuwezi kushauri kuwa ni utaratibu bora wa kuigwa. Kwa mtazamo wangu, hili ni kama gharama isiyosemwa ambayo ni mzigo unaoongeza uzito fulani kwa wateja wakati wa kufanya malipo.
Changamoto hii ya “ya kutolea” inawakabili wateja wanaoamua kufanya malipo kwa njia ya huduma fedha kwa simu katika maeneo mbalimbali ya biashara. Kwa mfano, madukani, masokoni, kwenye migahawa, vyombo vya usafiri, na sehemu nyinginezo, wakati wa kufanya malipo ya huduma au bidhaa unaweza kuombwa kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya kulipia “ya kutolea”.
Kwa mfano, badala ya kulipa bei ya bidhaa mliyokubaliana, mathalan shilingi 10,000, unaweza kulazimika kulipa 11,000, na kiwango hicho kinaweza kuongezeka kadiri unavyoongeza kiasi cha malipo unayotaka kufanya. Sababu kubwa, anayepokea malipo aweze kufidia gharama za kutoa, hela yake “isikatwe” wakati akienda kuitoa kwa wakala.
Jambo hili tunaliendekeza, lakini linadhoofisha juhudi za kuchagiza matumizi ya huduma za kifedha kupitia mtandao, na linakwaza ujumuishi wa huduma za kifedha kwa njia kadhaa:
Kwanza, ‘ya kutolea’ inaongeza gharama za kufanya miamala kwa mlipaji. Hii ni gharama isiyo rasmi, haisemwi lakini ipo, inatozwa na anayepokea malipo kwa mteja. Inaweza kupunguza baadhi ya watumiaji, hasa wa kipato cha chini, kutumia huduma za kifedha kwa njia ya simu mara kwa mara. Inaleta ukakasi kufikia malengo ya matumizi ya huduma za fedha za kidijitali ambayo lengo lake huduma hizo zifikie na kutumika kwa watu wengi zaidi.
Pili, gharama hii inaweza kulazimisha baadhi ya watumiaji, hasa wenye kipato cha kawaida, kurudi kutumia fedha taslimu kwa ajili ya malipo, kwa sababu fedha taslimu haina ‘ya kutolea’. Inaweza kurudisha nyuma juhudi za kupunguza matumizi ya fedha taslimu na inaweza kupunguza mapato ya kampuni kutokana na ada za miamala, pamoja na kupunguza mapato ya serikali kutoka kwa tozo za miamala.
Tatu, ‘ya kutolea’ ni kero kwa walipaji. Si watumiaji wote wana uwezo wa kuongeza kiasi cha fedha wakati wa kufanya malipo. Mfano, shilingi 1,000 inayohitajika kama ‘ya kutolea’ inaweza kuwa kiasi hichohicho ndio mteja alichopatana kama punguzo la bei, au ndiyo nauli yake ya daladala kumfikisha nyumbani.
Nne, kwa wafanyabiashara, hususan wale wadogo, ‘ya kutolea’ inaweza kuwafanya kupoteza aina fulani ya wateja. Wakazi wengi, hasa katika maeneo ya mijini, wanapendelea kulipa kwa njia ya simu kwa kuwa ni rahisi na salama zaidi kuliko kutembea na fedha taslimu. Changamoto za kulipa ziada ikiwa ni mara kwa mara, mteja anaweza kuhamia kwa muuzaji au mfanyabiashara mwingine ambaye hamdai ziada wakati wa kulipa.
Wafanyabiashara masokoni, madukani, vyombo vya usafiri, na wengineo wanapaswa kujiunga na huduma za malipo kama LIPA NAMBA, ili kuwapa wateja wao fursa ya kulipa kwa urahisi, na hili litawawezesha kupokea malipo kwa urahisi na salama.
Vilevile, makampuni yanayoendesha huduma za kifedha za simu yana nafasi ya kuongeza elimu kwa wafanyabiashara wa ngazi mbalimbali. Elimu hii inaweza kujumuisha faida za kuwa na huduma za kupokea malipo, na jinsi huduma hizi zinavyoweza kurahisisha kazi zao. Pia, wafanyabiashara wanaweza kufahamishwa kuhusu vigezo vya kujisajili na usalama wa kutumia huduma hizo ili wapate ari ya kujiunga.
Sambamba na hilo, kampeni za kusajili wateja wa huduma za malipo zinaweza kuandaliwa, kama vile usajili wa laini za simu za kawaida unavyofanyika nyumba hadi nyumba, makampuni yanayotoa huduma za malipo yanaweza kufanya hivyohivyo kusajili wafanyabiashara wenye sifa duka hadi duka, ili kuwafikia kwa urahisi na kwa karibu zaidi.