BoT yaweka kibano mikopo ‘kausha damu’

Mtwara. Baada ya wabunge kucharuka kuhusu mikopo ‘kausha damu’ kwenye mitandao, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuja na mwarobaini unaozuia mkopeshaji kuingia kwenye namba za simu za mteja.

Mbali na hilo, BoT imeelekeza kampuni inayokopesha kwenye mtandao iweke wazi masharti yake na si kuandika ‘masharti na vigezo’ pekee, badala yake kila sharti na kigezo lifahamike kwa mteja kabla ya kukopa.

Uamuzi wa BoT umetokana na agizo la Bunge la kuitaka Serikali kuhakikisha inawabana wakopeshaji wanaotuma ujumbe kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mtu waliyemkopesha kwa lengo la kumdhalilisha.

Kauli hiyo ya BoT ilitolewa jana, Februari 27, 2025 na Ofisa Mkuu Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania, Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Deogratias Mnyamani, kwamba utaratibu mpya utawabana wakopeshaji wa mtandaoni na pia wenye taasisi za kukopesha mitaani, ambazo zimesababisha kuzaliwa jina la ‘mikopo kausha damu.’

Kwa mujibu wa Mnyamani, baada ya kuzifungia aplikesheni 80 za taasisi zinazotoa mikopo kidijitali, ni watoa huduma 10 tu ndio waliofanikiwa kutimiza vigezo vipya na kuruhusiwa kuendelea na biashara hiyo.

Suala la mikopo ‘kausha damu’ liliwahi kuibuka bungeni, ambapo Mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond, kwenye mchango wakei alilalamikia udhalilishaji kwa wakopaji kwa kutuma ujumbe mbaya kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote ambao namba zao za simu ziko kwenye simu ya mkopaji.

“Wanatukanwa, wanadhalilishwa, ndiyo maana tunasema kuna uhusiano kati ya taasisi hizi za ukopeshaji na kampuni za simu,” alisema.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, ambaye aliongoza kuwabana mawaziri; Dk. Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha) na Nape Nnauye (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), kuhusu riba kubwa na mikataba kati ya wakopeshaji na kampuni za simu, huku Bunge likiiagiza Serikali kulifanyia kazi.

Jana, Ofisa Mkuu Mwandamizi wa BoT, Mnyamani, amesema mwongozo mpya unatoa haki kwa pande zote—wakopaji na wakopeshaji—huku ikisema sasa imezuia uwezekano wa mkopeshaji kupata namba za simu zilizomo kwenye simu ya mkopaji, ikiwamo kumzuia kuingia kwenye makundi ya WhatsApp.

Pia, amesema taasisi inayokopesha lazima ifahamike zilipo ofisi zake, ikiwamo kuweka wazi masharti na vigezo kwa mkopaji kabla ya kukopa.

Katika kutekeleza hilo, amesema BoT imeingia makubaliano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ajili ya kuwadhibiti wakopeshaji wa mitandaoni.

“Sisi tumeandaa miongozo, lakini tulikaa chini na TCRA kushughulikia jambo hili, kwa hiyo tunapopata taarifa sisi tunatoa kwa TCRA, kisha yeye ndiye anamfungia,” amesema.

Kuhusu mikopo ya ‘kausha damu’ inayotolewa na taasisi ndogo za fedha za mitaani, amesema wanadhibiti kwa kutoa elimu kwa pande zote mbili—mtoa huduma na mpokeaji huduma.

“Unajua hawa watu wa kutoa huduma ndogo za fedha ni tofauti na watu wa benki ambao wanajua sheria, ila upande huu mtu akiwa na fedha zake anaamua kuendesha biashara bila hata kuwa na elimu.

“Ila tukiona tatizo linajirejea, tunatoa onyo, ama faini, kumsimamisha kutoa huduma kwa muda au kumfutia leseni kabisa ya kutoa huduma,” amesema.

Kuhusu masharti ya mkopo, amesema ni vizuri mkopaji akaomba kufafanuliwa namna ya kulipa mkopo huo na marejesho yake kabla ya kukopa.

“Mara nyingi tunapofanya ukaguzi tunakuta mikataba kandamizi, kwa kweli watu wanaumizwa kwa maslahi ya wachache,” amesema.

Hata hivyo, amesema ili kuwa salama zaidi katika mikopo, mkopaji anatakiwa kurejesha kwa wakati, kukopa kwa ajili ya maendeleo, na iwapo mkopaji akijikuta ameshaumizwa, lipo dawati la malalamiko wakatoe ripoti.

Kwa mujibu wa BoT, hadi kufikia Februari 21, 2025, walikuwa na maombi ya watoa huduma 3,075, kati ya hao waliopewa leseni ni 2,450, huku kukiwa na wastani wa maombi 18 hadi 20 kwa wiki.

Kuhusu mchezo wa upatu, amesema ni utapeli na amewataka wananchi kuchukua tahadhari, kwani hakuna taasisi inayotoa akiba ya asilimia kubwa, kwa hiyo wazinduke—huo ni utapeli kama ulivyo utapeli mwingine.

Related Posts