CCM yataka haki ugawaji maeneo Mbuyuni, yaonya utozwaji wa fedha

Moshi. Kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM)  Mkoa wa Kilimanjaro, imeiagiza serikali mkoani humo kuhakikisha haki inatendeka wakati wa ugawaji wa maeneo ya biashara katika soko la mbuyuni, ambalo limefanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kuungua moto.

Mbali na hilo, Kamati hiyo pia imeonya utozwaji wa fedha kwa wafanyabiashara wakati wa mchakato huo wa ugawaji maeneo na kuagiza kama kuna wafanyabiashara ambao walishatoa fedha warudishiwe.

Maelekezo hayo yametolewa leo, Alhamis Februari 27, 2025 na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel wakati wa ziara ya kamati ya siasa ya Mkoa huo, kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho,

Soko la mbuyuni liliungua Moto Februari 5, 2024 na kuteketeza zaidi ya vibanda 2000 vya wafanyabiashara mbalimbali ikiwemo mamalishe na wajasiriamali wadogo.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, akizungumza, Mercy Mollel akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la mbuyuni, wakati kamati ya siasa ya chama hicho ilipotembelea kukagua ujenzi wa soko hilo.Picha na Florah Temba

Wakati wa ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa Soko la Mbuyuni, Katibu wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Kilimanjaro, Mollel, alizungumza na wafanyabiashara na kueleza kuwa serikali iliamua kujenga upya soko hilo baada ya kuungua ili kuwezesha wafanyabiashara kufanya biashara katika mazingira salama na rafiki. Alisisitiza kuwa haki lazima itendeke na wafanyabiashara waliokuwepo awali wapewe kipaumbele.

“Soko hili limejengwa kwa ajili ya wananchi kufanya biashara katika mazingira mazuri. Tuipongeze serikali kwa kazi kubwa ya kulijenga, kwani Rais Samia amemaliza sehemu yake, sasa ni jukumu letu kuhakikisha ugawaji wa maeneo unafanyika kwa haki,” alisema Mollel.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Kamati ya Siasa ya Mkoa, kipaumbele cha kwanza katika ugawaji wa maeneo litakuwa kwa wafanyabiashara waliokuwepo kabla ya soko kuungua. Aidha, alimwagiza Mkuu wa Mkoa, Nurdin Babu, kuhakikisha kuwa kamati iliyoundwa inasimamia haki katika mchakato huo.

“Wafanyabiashara wanajuana, hivyo waliokuwepo waingie kwanza bila kudaiwa chochote. Ikiwa mtu yeyote atadai fedha kwa ajili ya kuingia, hatua kali zichukuliwe dhidi yake,” alionya.

Mollel alisisitiza kuwa hakuna mfanyabiashara atakayetozwa gharama yoyote ili kupata eneo lake la biashara. Alibainisha kuwa ikiwa kuna fedha ambazo tayari zimetolewa, zinapaswa kurejeshwa mara moja. Kauli yake ilipokelewa kwa shangwe na wafanyabiashara waliokuwepo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni, wakati kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi, ilipotembelea soko hilo.Picha na Florah Temba

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema kuwa serikali imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara waliokuwepo wanapata maeneo yao bila kikwazo.

“Haiwezekani soko limeungua, likajengwa upya, halafu watu wa awali waondolewe na wengine waingizwe kwa ujanja ujanja. Hilo halitakubalika,” alisema Babu kwa msisitizo.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kufanya maboresho ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wadogo pia wanapata maeneo mazuri na rafiki kwa biashara zao.

Wafanyabiashara wafunguka

Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko la Mbuyuni walieleza kuwa, ingawa kujengwa kwa soko hilo ni faraja kwao, bado kuna changamoto katika ugawaji wa maeneo.

Yohana Simon alisema kuwa changamoto kubwa ni kuingizwa kwa watu ambao awali hawakuwa sehemu ya soko hilo, hali inayosababisha malalamiko.

“Baadhi ya watu ambao awali walikuwa wakifanya biashara maeneo mengine wanajiandikisha ili wapate maeneo ndani ya soko, huku wafanyabiashara waliokuwepo awali bado hawajaandikishwa,” alisema Simon.

Alisisitiza kuwa uongozi wa soko unawafahamu wafanyabiashara waliokuwepo awali na bidhaa walizokuwa wakiuza, hivyo usimamizi wa ugawaji unapaswa kuwa wa makini ili kuzuia upendeleo.

Flora Msuya naye alieleza wasiwasi wake kuhusu idadi kubwa ya wafanyabiashara wapya walioandikishwa, huku waliokuwepo awali wakiwa hawajui hatma yao.

“Tunaomba utaratibu wa wazi kuhusu jinsi tutakavyopata maeneo yetu, kwa sababu hadi sasa hatujui nini kitatokea,” alisema Msuya.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa soko hilo, mhandisi wa ujenzi Manispaa ya Moshi, Elibahati Kimaro amesema soko hilo limejengwa kwa gharama ya Sh1.58 bilioni ambayo ni mapato ya ndani na tayari limekamilika.

Kamati hiyo pia ilitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la utawala Manispaa ya Moshi ambalo limegharimu Sh2 bilioni na utekelezaji wake umefikia asilimia 99, pamoja kukagua matengenezo ya barabara ya matunda kwa kiwango cha lami.

Related Posts