SIMBA inajiandaa kulihama jiji la Dar es Salaam ili kwenda Arusha kuvaana na Coastal Union kabla ya kurejea kujiwinda dhidi ya Yanga katika Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Machi 8, kuna mambo flani ni kama hayaeleweki kikubwa kikiwa ni afya za mastaa wa kikosi hicho.
Bahati nzuri ni kwamba, mastaa karibu wote wako fiti na wanaendelea kujifua chini ya kocha Fadlu Davids, ambaye amefanikiwa kuwaweka mashabiki wa Msimbazi katika mbio za kufukuzia ubingwa wa mashindano ya Bara.
Lakini benchi la ufundi chini ya kocha huyo limepata mshtuko kwa kuumia beki wa kati, Che Fondoh Malone, ambapo
Mcameroon huyo aliumia kwenye mchezo uliopita kati ya Simba na Azam FC aliotolewa dakika za mapema na nafasi yake kuzibwa na Chamou Karaboue, huku mechi ikiisha kwa sare ya 2-2.
Che Malone aliyesajiliwa misimu miwili iliyopita amekuwa beki tegemeo katika kikosi cha Simba kilichopita mikononi mwa makocha wanne akiwamo Fadlu aliyeshtushwa na tukio hilo linaloweza kumfanya Che Malone kuikosa Coastal Union na kuwa katika hatihati ya kuivaa Yanga.
Beki huyo aliumia goti na taarifa za klabu zinasema ilikuwa ikisubiri vipimo vya mwisho ili kujua hali yake kama atakuwa kwenye msafara utakaoifuata Coastal jijini Arusha au la, lakini Fadlu hofu yake ni kuhusu mechi ya Dabi ya Kariakoo huku akiwa na deni la kipigo cha bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu amesema amepata wasiwasi kwa Che Malone kwa jeraha la goti akitaka afanyiwe vipimo haraka kujua hali yake ili ajue namna ya kujipanga katika mechi mbili zijazo kabla ya Ligi Kuu kusimama kupisha michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), Simba ikipangwa na TMA.
Fadlu aliyeiongoza Simba katika mechi 31 za mashindano yote ikiwamo mbili za Ngao ya Jamii, moja ya Shirikisho (FA), nane za Shirikisho Afrika na 20 katika Ligi Kuu Bara akishinda 23 kutoka sare tano na kupoteza tatu, amesema kuumia kwa Che Malone ni pigo kwa timu kwani ni tegemeo.
“Jambo linalonipasua kichwa sasa ni kuhusu hali aliyonayo (Che Malone), kwani sijajua atakaa nje kwa muda kama akifanyiwa vipimo. Tuna mechi muhimu mbele yetu, hivyo kwangu sihitaji kumkosa mchezaji yeyote ili kuhakikisha timu inakuwa imara kila sehemu,” amesema Fadlu.
“Yapo majeraha yanayomfanya mchezaji akae nje muda mrefu au mfupi, lakini majibu hayo yatatokana na vipimo hivyo tuombe Mungu.”
Hata hivyo, hadi jana hakukuwa na taarifa rasmi juu ya vipimo alivyofanyiwa beki huyo, lakini Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema walikuwa wanasubiri vipimo ili kujua ukubwa wa jeraha ya beki huyo aliyeunda ukuta mgumu sambamba na Abdulrazaq Hamza na Chamou Karaboue katika timu hiyo.
Chini ya mabeki hao, Simba imekuwa timu inayoongoza kwa kuruhusu idadi ndogo ya mabao (8) kupitia mechi 20 ikizizidi Yanga iliyofungwa tisa na Azam (11) zinazofukuzana kileleni kusaka taji na Ligi Kuu kwa msimu huu. Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 55, Simba (51) na Azam (44).