Zipo sababu kadhaa za kimfumo na kiuchumi zinazofanya mishahara kulipwa kwa utaratibu wa mwezi, wiki, au siku badala ya mwaka mzima. Kwa nchi nyingine mishahara hulipwa kila baada ya wiki mbili. Hapa Tanzania, mara nyingi mshahara hulipwa kwa mwezi.
Ulipwaji wa mishahara kwa muda mfupi wa wiki au mwezi ni mfumo bora wa malipo kwa ajili ya utulivu wa kifedha kwa wafanyakazi na una faida kiuchumi kwa ujumla. Ni muhimu kujua sababu hizi ni pamoja na zifuatazo.
1. Urahisi wa kudhibiti fedha kwa waajiri
Waajiri hupata mapato yao kidogokidogo kwa kuuza bidhaa au huduma zao. Kwa hivyo, kulipa mshahara mara moja kwa mwaka kungekuwa mzigo mkubwa wa kifedha kwa kampuni nyingi. Badala yake, waajiri hulipa mishahara kulingana na mapato yao ya kila mwezi, hivyo kusaidia kudhibiti mtiririko wa fedha.
Hii inawasaidia kuepuka matatizo ya kifedha na kuhakikisha kuwa kampuni inaweza kufanya shughuli zake kwa urahisi. Inategemewa kuwa mfanyakazi awe na weledi wa kutosha ili kuwezesha waajiri kuweza kumudu kulipa mishahara.
2. Usalama wa kifedha kwa wafanyakazi
Mishahara hutoa usalama kwa wafanyakazi na kuwa na uhakika wa malipo ya uhakika (hata kama ni kidogo) kwa kila mwisho wa mwezi. Mshahara hutoa fursa ya kupanga bajeti ya mapato na matumizi ya kila mara na hivyo kuweza na kutumia fedha kwa mahitaji ya kila mwezi kama vile chakula, malipo ya nyumba, na shule za watoto. Hii inawalinda wafanyakazi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha na kuwasaidia kuishi kwa utulivu.
3. Sheria za kazi na malipo ya kodi
Mishahara hukatwa kodi ambayo pia husaidia na kutumiwa kama mapato kwa serikali ili kuweza kuendesha shughuli zake na hivyo inafanya utekelezaji wa sheria za kodi. Serikali kama mtu binafsi ni taasisi ambayo inapata fedha zake kupitia vyanzo mbalimbali na haipati kwa mkupuo na hivyo kulipa mishahara kila mwezi ni njia rahisi ya kuangalia ukuaji wa shughuli za kiuchumi pia.
4. Kuepuka matumizi mabaya ya fedha
Utoaji wa mishahara kila mwezi unawezesha urahisi wa kupanga matumizi. Watu wengi wangeweza kutokuthamini kazi iwapo wangelipwa mara moja kwa mwaka. Mfumo wa malipo ya mshahara kwa mwezi au wiki unawasaidia wafanyakazi kuwa na uhakika wa kupata fedha kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku, hivyo kuepuka matumizi mabaya ya fedha.
5. Faida za kijamii na kiuchumi
Kulipa mshahara kidogokidogo kuna faida kwa uchumi, kwa kuwa watu wanatumia pesa mara kwa mara, hivyo kusaidia biashara ndogo na mzunguko wa pesa katika jamii. Ikiwa kila mtu angelipwa mara moja kwa mwaka, basi miezi michache ya kwanza ya mwaka ingejaa matumizi makubwa, kisha uchumi ungedorora miezi mingine.
6. Unyumbufu katika malipo ya ziada
Malipo ya mshahara kwa kipindi kifupi husaidia kutathimini utendaji wa mfanyakazi na hivyo kutoa fursa ya kupanda cheo na hivyo kutoa posho, bonasi, na marupurupu mengine kwa urahisi. Ikiwa mshahara ungetolewa mara moja kwa mwaka, ingekuwa vigumu kurekebisha nyongeza au motisha za wafanyakazi.
Mapato ya mshahara ama ya kibiashara ambayo yanapatikana kidogokidogo na kwa muda mrefu ni muhimu katika kujenga uhimilivu na pia kuwa na uwezo wa kupanga bajeti yako. Husaidia biashara ndogondogo, uchumi na ustawi wa jamii kwa jumla.