Hamas yakabidhi maiti wanne wa Waisrael – Global Publishers



Vyombo vya habari vimeripoti mapema leo Alhamisi kwamba mchakato wa kuwaachilia huru mateka wa Kipalestina umeanza baada ya HAMAS kukabidhi miili ya mateka wanne wa Israel.

Miili ya mateka hao wanne wa Israel, ambao majina yao yalitangazwa jana usiku na Abu Ubaidah, msemaji wa Brigedi ya Al-Qassam (tawi la kijeshi la Hamas), nayo imekabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu huko Gaza.

 

Halikadhalika makumi ya mateka wa Kipalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Quds wameachiliwa huru mapema leo Alhamisi alfajiri ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Hamas na Israel, na wamepokewa kwa shangwe kubwa Ramallah.

Mateka 42 wa Kipalestina wameachiliwa huru mapema leo Alhamisi, 37 kati yao wameelekea makwao huko Ramallah na mateka wengine watano wamerejea makwao katika mji wa Baytul Muqaddas. Wamo pia wale mateka wa Kipalestina ambao Israel iliwahukumu kifungo cha miongo kadhaa jela.

Mateka wa Kipalestina huko Bithynia, magharibi mwa Ramallah, pia wamepata mapokezi ya mashujaa na kwa shangwe kubwa.
Kabla ya hapo gazeti la Israel la Haaretz, lilinukuu duru moja ya usalama ya Israel ikisema kuwa, mateka wa Palestina wangeachiliwa huru baada ya miili ya mateka wa Israel kutambuliwa katika kivuko cha Karam Abu Salem.

Hapo awali, ofisi ya vyombo vya habari ya Chama cha Mateka wa Palestina ilitangaza kwamba kuna uwezekano wa kuachiliwa huru mateka 590 hadi 594 wa Palestina katika Ukanda wa Gaza saa kadhaa zijazo kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya HAMAS na Israel.


Related Posts