KANDASIKIRA WAISHUKURU FAJU 45 KUWAJENGEA OFISI

Na Mwandishi wetu, Simanjiro

WAKAZI wa Kijiji cha Kandasikira Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameishuku kampuni ya Faju 45 company LTD kwa kuwajengea ofisi ya kisasa.

Pamoja na kujenga ofisi ya kisasa iliyogharimu sh. 20 milioni pia kampuni ya Faju 45 LTD kupitia Mkurugenzi wake Safina Msangi, imenunua samani za ofisi za ndani na kuwavutia nishati ya umeme.

Mmoja kati ya wakazi wa kijiji hicho Esupati Laizer akizungumza na waandishi wa habari amesema kampuni ya Faju 45 inastahili pongezi kwa kuwajengea ofisi hiyo.

“Kampuni hiyo kupitia mkurugenzi wake Safina Msangi wametusaidia kujenga ofisi ya kijiji na sasa shughuli za kiserikali zinaendelea,” amesema Laizer.

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Kandasikira Habiba Njau amempongeza mkurugenzi wa kampuni hiyo Msangi kwa kufanikisha ujenzi wa ofisi hiyo.

Njau amesema jitihada za wadau wa maendeleo kama hao zinapaswa kuungwa mkono kwani Msangi amefanikisha maendeleo hayo ambayo awali hayakuwepo.

“Kwa kweli huyu ni mwekezaji mdogo ila amefanya jambo kubwa kwa miaka michache sana, wawekezaji wengine waige mfano kupitia kampuni hii,” amesema Njau.

Hata hivyo, mkurugenzi wa kampuni ya Faju 45 Ltd, Safina Msangi ambayo inachimba madini ya ujenzi eneo la Kandasikira amethibitisha kujenga ofisi hiyo.

“Ni kweli tumetumia kiasi cha sh. milioni 20 kwa ajili ya kujenga ofisi ya kijiji na kununua samani na kuweka nishati ya umeme,” amesema Msangi.

Amesema amefanya hivyo kupitia kampuni hiyo kwani anachimba madini ya viwandani kwenye kijiji hicho akaamua asaidie ujenzi wa ofisi.

“Mara ya kwanza kufika kwenye ofisi hiyo nilishangazwa mno kwani walikuwa wanakaa njee kwenye mawe huku wakifanya kazi za jamii,” amesema Msangi.

Amesema aliamua kujitolea kwa kujenga ofisi hiyo ya kisasa nakununua samani za ndani ikiwemo viti na kuvuta nishati ya umeme kwa lengo la kusaidia jamii ya eneo hilo.

Meneja wa kampuni hiyo Omary Ndwatta amesema moyo wa kujitolea kwa jamii alionao mkurugenzi wao ndiyo umesababisha hayo.

“Wadau wengine wa maendeleo waige mfano wa mkurugenzi wetu katika kusaidia jamii inayowazunguka kwa kurudisha kidogo kwa kile wanachokipata,” amesema Ndwatta.

 

Related Posts