Dar es Salaam. Ongezeko la wagonjwa wa kiharusi nchini, limewaibua wataalamu wa afya wanaotaja mambo ya kuepuka kupata tatizo hilo, huku wenye shinikizo la juu la damu wakitajwa kuwa hatarini zaidi.
Matumizi yasiyo sahihi ya dawa za kisukari, shinikizo la juu la damu lisilotibiwa, matumizi ya dawa za kulevya, unywaji dawa bila ushauri wa daktari, pombe kali au kunywa kupita kiasi ni miongoni mwa visababishi vya kiharusi.
Tangu Juni mwaka 2023, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI), imekuwa ikipokea wagonjwa watatu mpaka sita kwa wiki waliopata kiharusi cha kupasuka mshipa wa damu.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa na taasisi hiyo katika Wilaya ya Kinondoni unaonyesha, kati ya waliopata kiharusi, asilimia 63 kilisababishwa na shinikizo la juu la damu ‘presha’ , huku asilimia 49 kati yao hawakuwa wakijua hali zao za presha.
Hali hiyo pia imekuwa ikionekana katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), ambayo hupokea wagonjwa wawili mpaka watatu waliopata kiharusi kwa siku.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Edwin Ochina amesema muhimu ni kuepuka vihatarishi vinavyosababisha kiharusi ikiwemo kuangalia hali ya shinikizo la damu maarufu presha.
“Hata kama hujaambiwa na daktari ni vema kupima shinikizo la damu na kujua hali yako. Watu wajitahidi sana kuishi bila kubweteka,” amesema.
Dk Ochina amesema ikitokea mtu ameshapata shinikizo la damu, mgonjwa anatakiwa kutumia dawa vizuri.
“Shida hawatumii dawa vizuri, ukimkuta wa kiharusi alikuwa na presha, hamezi dawa kwa wakati au leo amemeza kesho ameacha. Mgonjwa wa presha ameze dawa kila siku, vitu vingine ni kufanya uchunguzi sababu moja ya visababishi ni mafuta kupita kiasi, mapigo ya moyo hayako sawa ni muhimu kuhudhuria kliniki,” amesema.
Pamoja na hayo, amesema watoto wadogo walio na selimundu wako hatarini kupata kiharusi, ikiwa hawatachunguzwa kwa kufanyiwa kipimo cha kichwa mara kwa mara.
Daktari bingwa na mbobezi wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu MOI, Alpha Kinghomella ametaja visababishi mbalimbali ikiwemo shinikizo la juu la damu na wale wenye kisukari cha muda mrefu, ambao hawajatibiwa au kinatibiwa lakini wana sukari ambayo haijakaa kwenye ule usawa unaohitajika.
Ametaja sababu nyingine ni matumizi ya dawa za kulevya au unywaji dawa bila ushauri wa daktari, unywaji pombe kali au kunywa kupita kiasi.
“Kuna sababu zingine za magonjwa ya kurithi au vivimbe vidogo vidogo kama shinikizo la damu sio kubwa sana, hivi vivimbe haviwezi kupasuka kwani hatari inakuwa ni ndogo sana chini ya asilimia moja, lakini kama kutakuwa na mabadiliko ya presha au msukumo wa damu kuna uwezekano vivimbe hivi kupasuka,” amesema.
Dk Kinghomella amesema umri pia umeshuka, kwani wagonjwa wanaopata kiharusi ni kati ya miaka 20 hadi 50 zaidi ikilinganishwa na miaka ya zamani.
“Zamani tulitibu wenye shinikizo wakiwa na miaka 50 mpaka 60 lakini siku hizi tunaona chini ya miaka 50 mpaka 20 ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Wana harakati nyingi katika kumudu maisha na wanakuwa bize na hawa ndiyo wanaokuja kupata kiharusi na hawakujua kama wana shinikizo la damu au kisukari,” amesema na kuongeza kuwa wengi hawafanyi uchunguzi wa afya zao.
“Tukitibu kiharusi tunaanza kutibu magonjwa mengine yanayoibuka na kugundulika lakini yalikuwa ya muda mrefu na ndiyo yamesababisha kiharusi,” anafafanua.
Kiharusi hutokea damu inapovuja juu ya ubongo, mishipa kupasuka au kuna ugonjwa ulikuwepo hapo kabla ambao mara nyingi ni vivimbe vidogo vidogo vinavyoota juu ya mshipa wa damu unaoenda kwenye ubongo.

Kwa mujibu wa Dk Kinghomella, kunapokuwa na mabadiliko ya presha au msukumo wa damu ndani ya mishipa ya damu, vivimbe hivyo hupasuka vyenyewe na kusababisha kiharusi.
“Sisi tunaona asilimia 40 ya wagonjwa wote wa kiharusi, maana zipo za aina mbili ipo hii inayotokana na kuvuja kwa damu kichwani, na ile ambayo damu hushindwa kupita kufika sehemu mbalimbali za ubongo kwa sababu mishipa ya damu inakua imeziba.”
Amesema tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu ni kubwa zaidi na machapisho mbalimbali yanaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa hupata kiharusi cha aina hiyo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kila mwaka, watu milioni 15 duniani hupata kiharusi. Kati yao, milioni tano hufa na wengine milioni tano hubaki na ulemavu wa kudumu, jambo linalowaletea mzigo familia na jamii
Kumtambua mwenye kiharusi
Moja, uso wa mgonjwa unaanza kwenda upande, wakati mwingine mdomo unaenda upande au upande mmoja wa uso unashuka.
Pili, mkono wa kulia au kushoto kupoteza nguvu. Anaweza kukwambia anaona mkono wake hauwezi kushika kitu, wakati mwingine kama alikuwa anafanya kazi mkono unashindwa kufanya chochote.
Tatu, kuongea kwake hubadilika, ataanza kuongea bila kueleweka inaweza kufanana na mtu asiejua kuongea au aliyelewa. Mara nyingi hushindwa kuzungumza vizuri na kuumba maneno kama inavyotakiwa.
Nne, muhimu ni kuhakikisha mgonjwa amepata matibabu ndani ya saa nne hadi nane ili kuokoa maisha na asipate ulemavu. Akiwahi matibabu hupona na kuendelea na maisha kama kawaida.