Makipa Bara wapewa msala | Mwanaspoti

KAMA unafikiria mambo ni mazuri kwa makipa, basi elewa kwamba kuna mambo yanayoendelea viwanjani ambayo yamewagusa katika timu, huku mechi za Ligi Kuu Bara zikibakia takriban tisa ili kumalizika kwa mashindano hayo.

Kutokana na namna ligi hiyo ilivyo kwa sasa, kila mchezaji amekuwa akijifua kuonyesha kuwa tayari kwa ajili ya kulibeba jahazi la kutoruhusu mabao kirahisi katika kikosi, ilhali mabeki na mastraika wakiwa kazini kutimiza majukumu yao.

Lakini, huku nyuma makipa wanne walioanza msimu huu wa Ligi Kuu Bara wakiwa chaguo la kwanza katika timu zao wamejikuta wakiponzwa na makosa waliyofanya katika baadhi ya mechi na kuwafanya wasoteshwe benchi na makocha wa timu hizo.

Kwa sasa nafasi za makipa hao zinachukuliwa na wenzao ambao hapo kabla ndio walikuwa wakisota benchi.

Kabla ya mchezo dhidi ya Tabora United, Beno Kakolanya ndiye alikuwa kipa aliyedaka idadi kubwa ya mechi za Namungo ambapo alikuwa ameanza kikosini katika michezo minane.

Hata hivyo, inaonekana kushindwa kuokoa mpira wa krosi ya Offen Chikola iliyowapa Tabora Utd bao la ushindi, kulimponza Kakolanya kwani tangu hapo hajadaka tena katika mechi nne zilizofuata za Namungo ambayo kwa sasa imekuwa ikimpanga Jonathan Nahimana kuwa kipa namba moja.

Fikirini Bakari ni kipa mwingine ambaye licha ya kuanza kwa kujihakikishia nafasi ya kucheza kikosini, amejikuta akianza kusotea benchi muda mfupi baada ya kufanya makosa yaliyowapa faida wapinzani.

Katika mechi dhidi ya Pamba Jiji ambayo Fountain Gate ilipoteza kwa kufungwa 3-1, Fikirini alifanya kosa la kupiga pasi kwa mchezaji wa timu pinzani, huku yeye akiwa hayupo langoni na Ally Ramadhan wa Pamba aliunasa mpira huo, akausukuma wavuni.

Tangu hapo, Fikirini Bakari hakupata tena nafasi katika kikosi cha kwanza cha Fountain Gate hadi pale Singida Black Stars ilipomrejesha katika dirisha dogo la usajili, kisha ikamtoa tena kwa mkopo kwenda Tabora Utd ambako hata huko hajapata nafasi ya kutosha ya kucheza mbele ya Mgaboni Jean Noel Amonome.

Upepo hivi sasa unaonekana kutomuendea vizuriĀ  kipa aliyejizolea sifa nyingi mwanzoni mwa msimu, Castor Mhagama anayeitumikia KenGold ya Mbeya tangu timu hiyo ilipopoteza kwa mabao 6-1 katika mchezo dhidi ya Yanga.

Katika mchezo huo Mhagama alifanya makosa mengi ikiwemo kuuokoa vibaya mpira wa krosi ambao haukuwa na nguvu uliopigwa na Chadrack Boka ambao ulitua miguuni mwa Clement Mzize aliyeujaza kimiani.

Tangu mchezo wa Yanga ulipomalizika hadi sasa, Mhagama hajapata tena nafasi katika lango la KenGold ambayo sasa inamtumia kipa Mussa Mussa.

Kocha wa makipa wa Tabora United, Razack Siwa amesema kuwa ni jambo la kawaida kwa makocha kumweka benchi mchezaji baada ya mechi aiiyokosea ili kumfanya awe makini akipata tena nafasi.

“Makipa nao ni binadamu na kuna nyakati wanakuwa wanakosea. Sasa wanapokosea unawakumbusha wajibu wao kwa kuwaweka pembeni kidogo na kuwapa fursa hiyo wengine ambao nao watajitahidi kuepuka makosa kwa vile watahofia kukaa benchi kama wenzao.

“Mimi sioni tatizo na hili linaonyesha kuwa ligi yetu iina kundi kubwa la wachezaji ambao wana viwango vizuri na ndio maana unaweza kuona kipa mmoja anapumzishwa na mwingine akafanya vizuri tu,” amesema Siwa, huku kipa wa zamani wa kimataifa aliye pia kocha wa makipa kwa sasa, Idd Pazi ‘Father’ akisema kuwa sio rahisi kwa makocha kuwabadilisha makipa mara kwa mara.

“Mchezaji wa kawaida akikosea, kocha anaweza kumpa tena nafasi lakini sio kwa nafasi ya kipa na ndio maana unapocheza katika nafasi hiyo unatakiwa kuwa makini kwa vile ukikosea umeigharimu timu na ndio maana makocha huwa hatupendelei kubadilisha makipa hadi itokee aliyepo amekosea sana,” amesema Father aliyewahi kutamba na Simba, Majimaji Songea, Taifa Stara na kucheza soka la kulipwa Indonesia na Sudan.

Related Posts