Wafula Chebukati, alikuwa mada kuu wakati wa matokeo ya urais, uchaguzi mkuu wa Kenya 2022. Samuel Kivuitu ni jina lililojadiliwa kwa hisia kali baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya 2007. Wote wamefariki dunia Februari. Sababu ya vifo vyao ni shambulizi la moyo (cardiac arrest).
Chebukati na Kivuitu, wote wameugua maradhi ya saratani kwa muda mrefu kabla ya kupatwa na shambulizi la moyo, lililokatisha uhai wao. Chebukati tarehe yake ya mauti ni Februari 20, 2025, wakati Kivuitu alitangazwa kufariki dunia Februari 25, 2013.
Mbali na uhusika wake kwenye uchaguzi mkuu wa Kenya 2022, Chebukati pia alikuwa mada ya uchaguzi mkuu wa Kenya 2017. Chebukati na Kivuitu, waliongoza tume za uchaguzi Kenya ndani ya miongo miwili iliyopita, na nyakati zote ulipoibuka mgogoro wa kiuchaguzi, majina hayo yalikuwa katikati ya taswira.
Kivuitu aliugua saratani ya koo kwenye sanduku la sauti (laryngeal cancer), upande wa Chebukati, familia yake ilitoa taarifa kwamba alisumbuliwa na maradhi ya saratani ya ubongo na alifanyiwa upasuaji mara mbili nchini Ujerumani, kuondoa uvimbe kwenye ubongo.
Alipokuwa hai, Kivuitu alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK) na aliiongoza nchi hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1997, 2002 na 2007. Vilevile, Kivuitu alikuwa Mwenyekiti wa ECK, aliyesimamia kura ya maoni ya katiba (referendum) mwaka 2005.
Kivuitu alikuwa mlalamikiwa wa uharibifu wa uchaguzi mkuu wa mwaka 1997, uliomwidhinisha Rais wa pili wa Kenya, Daniel Arap Moi kuendelea na urais kwa muhula wake wa mwisho. Kivuitu alitupiwa kila lawama kutokana na vifo vya Wakenya zaidi ya 1,000, vilivyosababishwa na vurugu baada ya kumtangaza Mwai Kibaki mshindi wa kiti cha urais kwa muhula wa pili, dhidi ya Raila Odinga.
Chebukati, alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Kenya, wakati wa uchaguzi mkuu wa Kenya 2017, ambao ulishuhudiwa kwa mara ya kwanza, matokeo yake ya urais yakibatilishwa na Mahakama Kuu Kenya, hivyo uchaguzi wa urais kurudiwa tena.
Uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2022, Chebukati alikuwa Mwenyekiti, aliyeiongoza tume (IEBC), ambayo ilikuwa na mgawanyiko mkubwa. Makamishna wanne wa IEBC, walipinga matokeo ya urais ambayo Chekubaki aliyatangaza. Makamishna hao walimtuhumu Chebukati kupika matokeo kivyake.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Chebukati 2022, ndiyo yaliyompa ushindi William Ruto dhidi ya Raila, hivyo kuibua tamthilia ya kisiasa ambayo iliinyima Kenya utulivu kwa takriban miaka miwili. Wafuasi wa Raila walimtuhumu Chebukati kuwa alihongwa na Ruto.
Machi 8, 2025, mwili wa Chebukati unatarajiwa kuhifadhiwa kaburini kwenye kijiji cha Sabata, Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia. Kifo chake kimetokea ikiwa imepita miaka miwili, miezi sita na siku tano, tangu alipomtangaza Ruto kuwa mshindi wa kiti cha urais hapo Agosti 15, 2022.
Machi 9, 2013, Kivuitu alipumzishwa kaburini, kijijini kwao Maiuun, Jimbo la Mwala, Kaunti ya Machakos. Kifo chake kilitokea ikiwa imepita miaka mitano, mwezi mmoja na siku 26, tangu alipomtangaza Kibaki kuwa mshindi wa kiti cha urais baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Kivuitu alimtangaza Kibaki kushinda muhula wa pili Desemba 30, 2007.
Kivuitu, baada ya kuondoka ofisini ECK, alikaa miaka minne, miezi miwili na siku tisa kabla ya kufikwa na mauti. Upande wa Chebukati, tangu alipoondoka IEBC, aliishi miaka miwili, mwezi mmoja na siku tatu, kisha alivuta pumzi ya mwisho.
Wakati mauti yanamfika Kivuitu, alikuwa na umri unaokadiriwa kufikia miaka 74. Chebukati, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63, miezi miwili na siku moja. Kila mmoja, sababu ya kifo chake inahusishwa na uamuzi wake alipokuwa anaongoza tume ya uchaguzi.
Tangu Chebukati atangazwe kuwa mwenda zake, watoa maoni ambao hawakuridhishwa na uamuzi wake wa kumtangaza Ruto kuwa mshindi wa kiti cha urais, wamekuwa wakidai kwamba kifo cha mwenyekiti huyo wa zamani wa IEBC kimetokana na vilio vyao ambavyo walivipeleka kwa Mwenyezi Mungu.
Watoa maoni hao kwa mfululizo, wamekuwa wakioanisha vifo vya Chebukati na Kivuitu kuwa vilitokea muda mfupi baada ya kuharibu uchaguzi. Wanajaribu kujenga taswira kwamba vifo vyao vimeharakishwa na manung’uniko ya waliodhulumiwa uchaguzi.
Vifo vya Chebukati na Kivuitu pamoja na maoni yanayotolewa, yanatoa mafunzo mawili ya kimsingi; mosi ni kuwa baada ya kifo chako watu watakujadili kwa namna ambavyo uligusa maisha yao. Walioguswa upande hasi, wanamsimanga Chebukati tangu kifo chake kilipotangazwa.
Waliofurahishwa na msimamo wa Chebukati kumtangaza Ruto mshindi wa kiti cha rais, wao maoni yao ni chanya. Wanamtambulisha kuwa ni shujaa, mzalendo na jasiri aliyetenda haki kipindi chote alichokuwa Mwenyekiti wa IEBC, hususan aliposimama kidete uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2022.
Somo la pili ni kuwa baada ya kifo, watu wataunganisha mifano na matukio ili kusherehesha yaliyomo kwenye vifua vyao. Kifo cha Chebukati kimefanya jina la Kivuitu lirejee kwa kishindo kwenye uso wa jamii na vyombo vya habari. Vinalinganishwa kwa namna ambayo kuna watu wanajaribu kufurahia au kusherehesha hisia zao.
Walioumizwa na uamuzi wa Kivuitu kumtangaza Kibaki kuwa Rais wa Kenya kwa muhula wa pili Desemba 30, 2007, kisha wakateswa na Chebukati alivyotangaza matokeo yenye utata uchaguzi mkuu wa Kenya 2017 na 2022, wamepata jambo la kupoza nyoyo zao. Wanaona maombi yao na vilio, sasa vimepata majibu.
Ukweli ambao unabaki ni huu, mwisho wa kila binadamu ni hesabu kwenye kitabu cha kila aliyeumbwa kwa udongo. Mungu huamua kumchukua kila mja kwa wakati wake. Vyovyote vile ambavyo watu watajaribu kufananisha vifo vya Chebukati na Kivuitu, jambo lisilopingika ni moja; kila nafsi itaonja mauti.