Milioni 400 za bodaboda Arusha bado kizungumkuti

Arusha. Sakata la ‘upigaji’ wa Sh400 milioni zinazodaiwa kuchotwa kwenye akaunti ya Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha (Uboma), limeingia sura mpya baada ya viongozi wa umoja huo kuililia Serikali iingilie kati ili fedha hizo zipatikane na kuimarisha mfuko wao na kuwasaidia kukua kiuchumi.

Kati ya fedha hizo Sh280 milioni zinadaiwa kuchotwa benki kwa nyakati tofauti na waliokuwa viongozi wa umoja huo, huku Sh120 milioni zikidaiwa kutolewa kama mikopo kwa akina mama, ambapo hadi sasa hatima ya fedha hizo haijajulikana kutokana na akaunti yao kufungwa kwa ajili ya uchunguzi.

Kufuatia malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoani humo mpaka kufikia  Machi 27, 2025 itoe ripoti ya uchunguzi wa suala hilo lilipofikia.

Kilio hicho kimetolewa leo Alhamisi Februari 27, 2025, na viongozi hao katika kikao maalumu cha kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kujadili makadirio ya mpango wa bajeti ya mwaka 2025/2026.

Mwaka 2018 kupitia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Arusha Mjini, wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara walichangia Sh400 milioni ambazo ziliwekwa kwenye akaunti maalumu ya umoja huo.

Akizungumza kikaoni hapo, Katibu wa Umoja huo mkoa wa Arusha, Hakim Msemo, amehoji iweje watuhumiwa wanaodaiwa kuchota fedha hizo huku kukiwa na kigugumizi cha kuwakamata na kuwafikisha mahakamani, fedha zinazodaiwa kuibiwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2018 hadi 2021.

Amesema mwaka 2018, Sh120 milioni zilitolewa kama mikopo kwa akina mama na kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2020, Sh280 milioni zilitolewa benki bila utaratibu na  mpaka wafadhili kutotaka kuwasaidia tena.

Amesema wizi wa fedha hizo walianza kuibua wao mwaka 2022 baada ya kuingia madarakani na kukuta akaunti hiyo ni tupu, huku nyaraka za benki zikionyesha namna fedha hizo zilivyochukuliwa katika matawi mbalimbali ya benki katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

“Mimi nimeenda hadi Dar es Salaam, kufuatilia na nikapata hadi namba ya gari la mwenyekiti, ila Takukuru hawakumfuata wala kuchukua hatua, tumeenda nyumbani kwa mwingine Sinoni ila tulipopeleka taarifa Takukuru hawakuchukua hatua,” amesema.

“Mtia saini mwingine nilipata taarifa zake kuwa ametokea Dar ameenda Rombo kutibiwa, nikawajulisha Takukuru ili wafuatilie ila hawajafuatilia, tunaomba Serikali itusaidie.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Hemed Mbaraka ameomba wanasiasa  kutokuingilia umoja huo na kuwagawa kwa masilahi yao binafsi, na kuwa yeyote atakayewaingilia na kutaka kuwagawa watawafikisha kwa uongozi wa mkoa.

Kwa upande wake Makonda amesema amesikia kuhusu suala hilo kabla hajawa kiongozi wa mkoa huo na kuwa sasa suala hilo linapaswa kufika mwisho na wahusika kuchukuliwa hatua, kwani Takukuru wasipolifuatilia suala hilo likaisha itaonekana Serikali inawalinda wahalifu.

“Kama hawa bodaboda wanajua mahali wahalifu walipo inakuaje nyie mamlaka ya uchunguzi mnashindwa kuwapata? Takukuru unajisikiaje kuwa na jalada lisilofikia mwisho?”

“Suala hili limesemwa sana hadi limekuwa kero, nawapa muda hadi Machi 27,2025 mtoe ripoti mmefikia wapi kwenye uchunguzi wa suala hili. Kama hakuna majibu tutahitimisha ninyi ni  sehemu ya wanufaika, mnajinasuaje kwenye hizi lawama? Amehoji.

“Kuhusu wanasiasa,niwasihi hofu isiwepo hatujatumwa kuja kutafuta nafasi msiwe na hofu hawa bodaboda, bajaji na machinga tuwaache wafanye biashara tusiharibu kwa kuwagawa nyie ndiyo viongozi,” amesema.

Kaimu Mkuu wa Takukuru, mkoani humo,  Daniel Kapakala akijibu hoja hiyo amesema wameshachunguza suala hilo ila tatizo kubwa walilopata ni kuwapata watuhumiwa wasili na kuwa wameshirikiana na Jeshi la Polisi ila bado hadi sasa hawajawapata.

“Watu wa Benki nao tumeshawahoji, mbunge pia na watu wengine ila kilichobaki ni kuwapata hao watu na tumeanza kuwatafuta tangu mwaka 2023.Ile akaunti ya akina mama waliopewa mkopo wa Sh120 milioni, wamerejesha Sh68 milioni ila akaunti tumeifunga kwa sasa zisije na hizi zikachukuliwa,” amesema.

Sakata hilo la bodaboda limekuwa likipigiwa kelele kila mara ambapo Desemba mwaka jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Mohamed Kawaida alisema suala hilo litafikishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ili mgogoro huo utatuliwe na fedha zao zirejeshwe.

Kikao hicho kiliidhinisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya Sh430.7 bilioni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026.

Related Posts