Mitazamo ya wawakilishi kuhusu mwelekeo wa Bajeti ya Serikali

Unguja. Siku moja baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwasilisha mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, Wawakilishi wameishauri iongeze wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuwa hayajakusanywa inavyotakiwa.

Katika bajeti hiyo, SMZ inatarajia kukusanya Sh6.8 trilioni, ikilinganishwa na Sh5.8 trilioni za mwaka wa fedha 2024/25.

Jana Jumatano, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dk Saada Mkuya aliwasilisha mwelekeo wa mpango na bajeti ya mwaka 2025/26 katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi, akionyesha kutakuwa na ongezeko la Sh1.62 trilioni, sawa na asilimia 31.

Akichangia hoja ya mwelekeo wa bajeti hiyo, Mwakilishi wa Paje, Soud Nahoda amesema licha ya ongezeko hilo, bado Serikali inapaswa kufanya ufuatiliaji wa karibu katika ukusanyaji wa mapato katika sekta ya utalii.

Amebainisha kuwa yapo mapato mengi katika sekta hiyo ambayo bado hayapatikani na hayaingii katika mfuko mkuu wa Serikali, badala yake yanaishia katika mikono ya wachache.

Pia, amesema bado Serikali haijaipa kipaumbele sekta ya kilimo kwa kuipatia zana za kisasa zitakazosaidia kuongeza uzalishaji.

Ameishauri Serikali kuzalisha mazao yanayotumiwa na wananchi kwa lengo la kudhibiti mfumko wa bei na kuthamini bidhaa zinazozalishwa ndani kuliko kuagiza bidhaa zinazopatikana kisiwani hapo.

Ameongeza kuwa uanzishaji wa viwanda vidogovidogo utaweza kukuza uchumi wa nchi, kusaidia kutoa ajira kwa vijana na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.

Aidha, ameiomba Serikali kuongeza ushuru kwenye bidhaa za vinywaji vikali ili kudhibiti mfumko wa bei wa ndani na kuvutia watalii zaidi, kwa kuhakikisha Mji Mkongwe unakuwa safi, hasa mitaro ya maji taka.

Mwakilishi wa Wawi, Bakari Hamad Bakari, amesema michango ya halmashauri na serikali za mitaa hairidhishi, hivyo SMZ inapaswa kuongeza nguvu ili kufuatilia matumizi ya fedha hizo.

Ameongeza kuwa idadi ya watalii wanaoingia nchini hailingani na makusanyo ya fedha yanayopatikana, hivyo akaishauri Serikali ifuatilie pengo hilo ili kuongeza mapato.

Bakari pia amesema Zanzibar bado haijaweza kutumia ipasavyo bahari kama chanzo cha mapato, hivyo Serikali inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kununua meli za uvuvi wa bahari kuu badala ya kutegemea fedha za mikopo.

Mwakilishi wa Kiembesamaki, Suleiman Haroub Suleiman, ameshauri Serikali kuwekeza katika kumbi za mikutano ili kuvutia watalii kufanya mikutano yao kisiwani humo na hivyo kuchochea utalii wa mikutano.

Mwakilishi wa Kiembesamaki,  Suleiman Haroub Suleiman

Ameongeza kuwa ingawa Serikali imetangaza kuwekeza katika utalii wa michezo, bado sekta hiyo haijapewa kipaumbele vya kutosha.

Kuhusu mikopo kwa wananchi, Suleiman amesema kuwa taasisi ya uwezeshaji wananchi bado inakumbwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa maombi na kutokuwepo elimu ya kutosha kuhusu urejeshaji wa mikopo hiyo.

Pia, ameshauri Serikali kutenga fungu maalumu kwa ajili ya mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mwakilishi wa Kwahani, Yahya Rashid Abdulla amependekeza kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali katika milango ya kuingia watalii, hususan viwanja vya ndege.

Mapendekezo ya Kamati ya Bajeti

Akiwasilisha ripoti ya maoni ya Kamati ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema Serikali inapaswa kufanya tathmini ya kina ili kuelewa namna ongezeko la watalii linavyoakisi ukuaji wa pato la Serikali na uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mwanaasha Khamis Juma

Kamati hiyo imependekeza Serikali iimarishe sekta ya kilimo kwani imeajiri wananchi wengi na uwekezaji wake unaweza kusaidia ongezeko la mazao na kuboresha uchumi wa wananchi.

Pia, Kamati imependekeza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula ili kudhibiti mfumuko wa bei na hivyo, imeitaka Serikali kuweka mkakati wa kuagiza bidhaa ambazo hazizalishwi Zanzibar na kurekodi takwimu za bidhaa zinazouzwa nje, ikiwemo mwani, dagaa na viungo vya chakula.

Katika sekta ya utalii, Kamati imependekeza Serikali kuimarisha usafi wa mazingira na kuhakikisha ajira katika sekta hiyo zinawanufaisha wananchi wa Zanzibar.

Pia, imeshauri Serikali kuhakikisha wahitimu wa vyuo vikuu na vya kati wanapewa elimu ya ubunifu ili waweze kujiajiri badala ya kutegemea ajira serikalini.

Kamati pia imeishauri Serikali kuhakikisha miradi ambayo tayari ina wawekezaji inaanza kutekelezwa na inawanufaisha wananchi wa Zanzibar.

Hatimaye, Kamati imependekeza serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Related Posts