Bukavu. Watu kadhaa wanahofiwa kujeruhiwa baada ya milipuko miwili kutokea wakati wa mkutano wa viongozi wa kundi la waasi la M23 katika mji wa Bukavu, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Picha na video zilizosambazwa mitandaoni leo, Alhamisi Februari 27, 2025, zinaonyesha taharuki huku watu wakikimbia kwa hofu, na miili ikiwa imetapakaa damu.
Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza kati ya viongozi wa M23 na wakazi wa Bukavu tangu waasi hao kutangaza kuuteka mji huo mapema mwezi huu, uliingia dosari kutokana na milipuko hiyo inayodhaniwa kuwa ya mabomu au risasi.
Miongoni mwa waliokuwepo ni Kiongozi Mkuu wa Muungano wa Makundi ya Waasi DRC ya Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), Corneille Nangaa.
Kwa mujibu wa Mwandishi wa habari wa Shirika la Associated Press aliyekuwa eneo la tukio, viongozi hao, akiwamo Nangaa, walilazimika kuondolewa jukwaani baada ya milipuko hiyo.
Waasi wa M23 wanaotuhumiwa kuungwa mkono na Rwanda, wameendelea kuimarisha udhibiti wao katika eneo hilo, wakiteka miji muhimu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000 katika mji wa Goma pekee.

Serikali ya DRC inakadiria kuwa na jumla ya zaidi ya watu 7,000, wakiwamo raia na wapiganaji, wamepoteza maisha kutokana na machafuko haya.
Katika mashambulizi ya kasi ndani ya wiki tatu, M23 imedhibiti miji mikuu ya majimbo ya Kivu Kaskazini (Goma) na Kivu Kusini (Bukavu), huku wakidai kusaidiwa na takriban wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda, kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
Waasi hao wameapa kuendelea na mapambano hadi Kinshasa, umbali wa zaidi ya kilomita 1,600.
Rwanda, kwa upande wake, imeishutumu DRC kwa kuwaajiri wapiganaji wa Kihutu wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa kati.
M23 inadai kuwa inapigana kuwalinda Watutsi na raia wa DRC wenye asili ya Rwanda dhidi ya ubaguzi, huku ikidai lengo lake ni kuibadilisha kuwa taifa la kisasa.
Hata hivyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alipoulizwa na CNN Januari mwaka huu, alikanusha vikali madai ya kufadhili waasi wa M23, akisisitiza kuwa hana taarifa ya uwepo wa wanajeshi wa Rwanda ndani ya DRC. Wachambuzi wa masuala ya usalama wanahisi kuwa madai ya M23 ni kisingizio cha kuhalalisha ushiriki wa Rwanda katika mzozo huu, ambao umeleta machafuko na kuhatarisha maisha ya mamilioni ya raia wa DRC.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.