Mtoto mwenye ulemavu ashambuliwa na panya watatu hadi kufa

Morogoro. Mtoto mwenye ulemavu wa akili na viungo, Christian Ngalika (Dotto) mwenye umri wa miaka 12 amefariki dunia baada ya kushambuliwa na panya watatu sehemu mbalimbali za mwili wake akiwa nyumbani kwao Kata ya Mang’ula Wilaya ya Kilombero.

Akisimulia tukio hilo babu wa mtoto huyo, Salumu Natechi amesema limetokea jana Februari 26, 2025 wakati mama wa mtoto huyo, Habiba Salumu alipokwenda hospitali kufuatilia vipimo vya Christian ambaye alikuwa akisumbuliwa na homa.

“Mtoto huyu (marehemu) wiki hii yote alikuwa akisumbuliwa na homa kali, sasa jana mama yake alichukua sampuli ya mkojo kwa ajili ya kwenda kupima maabara aliporudi kutoka maabara ndipo alipoingia ndani na kumkuta mtoto huyu akiwa anashambuliwa kwa kuliwa na panya maeneo mbalimbali ya mwili,” amesema Natechi.

Ameongeza; “wakati anashambuliwa na panya mtoto huyo hakulia wala kupiga kelele kwa vile hakuwa na ufahamu wowote. Mimi nilikuwa jirani na nyumbani nacheza bao nikashangaa naitwa ghafla nilipofika nyumbani, nikamkuta mjukuu wangu ndio anamalizikia kukata roho na tayari mwili wake ulikuwa umeshaanza kuwa wa baridi,” amesema Natechi.

Babu huyo amesema mpaka sasa hafahamu panya hao ni wa aina gani na kwa nini wamemshambulia mjukuu wake mpaka kufariki dunia.

“Kwa huku kwetu vijiji panya kuwepo ndani ni kitu cha kawaida kwa kuwa tunahifadhi mazao, lakini hawajawahi kumtafuna mtu, kinachonishangaza na kunisikitisha hawa panya wote watatu kumshambulia mjukuu wangu kwa wakati mmoja,” amesema Natechi.

Amesema baada kufariki dunia mwili wa mtoto huyo waliupeleka kituo cha afya Mang’ula ambako waliufanyia uchunguzi na kisha kukabidhiwa kwa ajili ya taratibu za mazishi na  kwamba leo Februari 27 walimpumzisha mtoto huyo.

Kwa mujibu wa bibi wa mtoto huyo, Saada Abdalah amesema mjukuu wake (marehemu) alizaliwa akiwa mkamilifu wa akili na viungo, lakini wakati anakua alipata homa kali iliyosababisha degedege ambalo lilimfanya apate ulemavu wa viungo na akili.

“Marehemu Christian alizaliwa wakiwa pacha ambapo mwenzake kulwa anasoma darasa la pili, lakini huyu alishindwa kupelekwa shule kutokana na changamoto yake ya ulemavu aliyoipata tangu akiwa na umri wa miaka sita,” amesema Saada.

Bibi huyo amesema kuwa siku hiyo ya Februari 26 asubuhi alimnywesha maziwa mjukuu wake akamnawisha na kutoka nje kuendelea na shughuli zake.

“Nikiwa bado naendelea na kazi zangu mama yake mzazi akarudi nyumbani akitokea maabara alikopeleka kipimo cha homa ya Christian, alipoingia ndani ndio akakuta mwanaye akiwa anashambuliwa na panya akaanza kupiga kelele…mama njoo umuone mwanangu huku anaumizwa… nikakimbia kuingia ndani ndio nikamkuta mtoto akiwa na hali mbaya, tangu nilipomuacha ndani mpaka tukio hilo linatokea haizidi hata nusu saa,” amesema Saada.

Ametaja sehemu ambayo mtoto huyo amenyofolewa nyama ni pamoja na kwenye mdomo wa juu, shavu, tumboni na kwenye vidole vya mikono.

Mmoja wa majirani, Zahania Abdallah amesema kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea katika eneo lao na limewashangaza, huku wakiwa hawajui panya hao wametoka wapi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema taarifa za tukio hilo bado hazijafikishwa polisi na kuahidi kuzifuatilia.

Related Posts