Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimewataka wananchi kutoka maeneo tofauti nchini kujitokeza kwa wingi katika kambi maalumu ya huduma za Afya bure ikiwa ni pamoja na upimaji magonjwa mbalimbali yasiyoambikiza inayo tolewa na Chuo hicho Kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salama.
Kambi hiyo ya siku tatu iliyoanza leo Februari 26,2025 na itamalizika Februari 28,2025 itakuwa endelevu kwa lengo la kuenzi mchango wa aliyekuwa Mkuu wa chuo hicho na Rais wa awamu ya pili wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo ya matibabu, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema programu hiyo ilianza mwaka 2024 na kwamba wataanza kuisogeza karibu na wananchi kwenye Kata na Vijiji ili waweze kupata fursa ya kutambua afya zao.
Amesema katika tafiti walizofanya kuhusu magonjwa ya kuambukiza yakiwamo malaria, Virusi Vya Ukimwi (VVU), zimewezesha Tanzania kukabiliana na magonjwa hayo ila magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yameongezeka hivyo, kambi hizo zitawawezesha kugundua wananchi wenye changamoto na kuwapatia rufaa.
“Kambi hii ni maalum kuenzi mchango wa hayati Mwinyi katika sekta ya afya, wengi mnafahamu kwamba pamoja na uzee wake alipenda kufanya mazoezi, hivyo ni jukumu letu kuona tunatoa huduma bora za afya,” alisisitiza.
Profesa Kamuhabwa amesema katika kambi hiyo, wananchi watapata huduma za uchunguzi wa afya kwa magonjwa ya macho, masikio, pua, koo, kinywa na meno na magonjwa ya saratani ya matiti na shingo ya kizazi, homa ya ini na tezi dume kwa kipimo cha damu.
Pia kutatolewa elimu kuhusu madhara ya maambukizi ya dawa na usugu wa dawa mwilini, magonjwa ya kuambukiza, utengenezaji na ukarabati wa vifaa tiba, uchakataji wa taarifa za afya kwa kutumia akili mnemba na lishe.
Profesa Kamuhabwa ametoa fursa kwa wananchi kujionea bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wataalamu wa MUHAS kwa upande wa taaluma ya famasia na tiba asilia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya kambi hiyo, Dk Ferdinand Machibya alisema wanatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 600 kwa siku mbili na kwamba wanatoa huduma za uchunguzi wa awali.
Dkt. Ferdinand alisema wananchi watakaobainika kuwa na magonjwa watashauriwa mahali sahihi pa kupata huduma hizo.
” Hii ni huduma muhimu kwetu na wajibu wetu kutoa huduma kwa wananchi. Waliojisajili mpaka sasa ni wananchi 130 na tunatarajia kuwafikia wananchi 600 kwa siku hizi mbili,” alisema.
Amefafanua kambi hiyo ina wabobezi katika nyanja mbalimbali za afya ambao pia watatoa elimu ya kujikinga na magonjwa yanayosumbua jamii na namna bora ya kutatua changamoto zao za afya.
Naye Adela Bulusha (86) mkazi wa Msakuzi jijini, Dar es Salaam, ameshukuru kuwepo kwa kambi hiyo kwani inawasaidia kupima afya zao bure ila ameshauri kuwepo kwa huduma za dawa katika kambi hizo ili kuwawezesha kupata matibabu pia.
Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirkishi Muhimbili (MUHAS) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kambi Maalumu ya huduma za Afya bure kuelekea kongamano la kumuenzi aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho na Rais wa pili wa awamu ya pili wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Ali Hassan Mwinyi