MSHAMBULIAJI nyota wa Yanga, Mzambia, Kennedy Musonda hachezi mpira tu, lakini amekuwa akiwafuatilia wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini na kuwataja watatu kati yao kuwa ndio wanaomkuna na kumfanya apende kusikiliza ngoma zao pale anapokuwa amepumzika nje ya uwanja.
Musonda anayemiliki mabao matatu kwa sasa katika Ligi Kuu Bara, amewataja wasanii hao ni Zuchu, Diamond na Harmonize, akisema amekuwa akisikiliza ngoma zao na kukunwa na vipaji walivyonavyo.
Aliliambia Mwanaspoti, mbali na kucheza mpira anapenda kusikiliza muziki.
“Mimi napenda sana muziki kisikiliza na kucheza, huwa napenda pia kuwasikiliza Zuchu, Diamond na Harmonize nawapenda sana, nyimbo zao zinanitoa uchovu pale ninakuwa nimechoka,” alisema Musonda na kuongeza anajivunia kufahamu Kiswahili vizuri tofauti na alipoingia Tanzania hakuwa anajua sana kuongea lugha hiyo.
“Kwa sasa najua jua Kiswahili kidogo, naongea na kuelewa mtu akiongea, kama hivi hapa tunaongea, kabla ya hapa nilikuwa sikielewi vizuri na hata ninaposikiliza ngoma za wasanii hawa huwa nazielewa maana yake na ninapenda mno muziki,” alisisitiza.