Kagera. Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amesema mara ya mwisho kuonekana hadharani Wakili Seth Niyikiza, ilikuwa Februari 19, 2025 hadi alipopatikana akiwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake.
Wakili Seth alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake maeneo ya Bukoba mjini, Februari 25, 2025 baada ya mteja wake kuona inzi wengi dirishani na majirani kuhisi harufu mbaya kutoka ndeani ya nyumba hiyo aliyokuwa akiishi.
Hatahivyo, Mwabukusi amesema Wakili Seth hakuwa mwenyekiti au makamu wa TLS Mkoa wa Kagera kama ilivyofahamika enzi za uhai wake, bali alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Msaada wa Kisheria.
Akijibu swali la mwandishi alilomuuliza kwa ujumbe mfupi wa simu leo Alhamisi Februari 27, 2025.
Mwabukusi amesema baada ya kutoonekana hata simu zake kutopokelewa zilipopigwa, mteja wake huyo aliamua kwenda kumtafuta nyumbani kwake na kukuta amefariki dunia.
“Kimsingi, hakuwa Convernor wala Vice ila alikuwa ni Mwenyekiti wa Legal Aid Commitee ya Chapte, wakili mwenzetu alikuwa anakaa mwenyewe kwenye nyumba anayoishi baada ya kuachana na mwenza wake.
“Mara ya mwisho kuonekana publicly (hadharani) ilikuwa tarehe 19 Februari, lakini baada ya hapo, simu zake hazikuwa zinapokelewa hadi mteja wake alipoamua kumtafuta hadi home (nyumbani) kwake, maana walikuwa na kesi na ilikuwa marked last adjournment (awali iliahirishwa),”amesema Mwabukusi.
Amesema kuwa mteja wake alipofika nyumbani Februari 25, 2025, eneo la dirishani kulikuwa na inzi wengi na harufu kali katika eneo hilo, huku gari lake likiwa limeegeshwa kwenye sehemu ya maegesho.
“Kwa hiyo, alitoa taarifa kwa uongozi wa mtaa na baadaye polisi. Walipofungua mlango, walimkuta akiwa kitandani, amejifunika shuka, huku mwili wake ukiwa tayari umeanza kuharibika,” amesema Mwabukusi.
Akaongeza: “Kwa hiyo, mchana huu uchunguzi umekamilika na kaka wa marehemu ameomba iandikwe kuwa ni kifo cha kawaida. Inaonekana kuna taarifa ambazo hazitakiwi kujulikana. Mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumamosi hii katika wilaya ya Misenyi.”
Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Ziwa, Seleman Gilla, amesema viongozi wa chama cha wanasheria watahudhuria mazishi ya wakili hhuyo wakiwa wamevalia mavazi yao ya kikazi kama ishara ya heshima kwa mchango wake alioutoa kwenye tasnia hiyo ya sheria.
Mwananchi linaendelea kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, ili kupata ufafanuzi kuhusu uchunguzi wa kifo cha wakili huyo.
Hata hivyo akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Februari 26, 2025 Kamanda Chatanda alisema
wanaendelea na uchunguzi zaidi kubaini kiini cha kifo chake.
Kwa mujibu wa kaka yake, Laurent Seth, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba, wakisubiri kufanyiwa uchunguzi ili kujua chanzo cha kifo chake.
Mkazi wa Kata Minziro Wilaya Missenyi, Egbart Rwegasira ambaye ni mtu wa karibu wa familia ya marehemu, amesema wakili huyo alikuwa ndiye msaidizi wa familia na ukoo wao kwa ujumla hivyo wamepoteza mtu muhimu.
“Msiba umeshtua sana maana ni mtu ambaye alikuwa hatumii hata vileo ila amekutwa ndani amefariki imeumiza ukoo mzima maana alikuwa anategemewa, mimi nimeanza kumfahamu muda mrefu na alikuwa wakili wangu,” amesema Rwegasira