KOCHA wa Polisi, Zadock Odhiambo amesema timu inayofanya maandalizi mazuri katika Ligi Daraja la Kwanza, Mkoa wa Dar es Salaam, ndiyo itakayopanda BDL.
Odhimabo aliliambia Mwanaspoti, kwa misimu mitano katika ligi hiyo, amegundua kama timu inayojipanga vizuri ndiyo yenye nafasi kubwa ya kucheza BDL akizitolea mfano DB Oratory, KIUT, Dar City, Crows, Polisi, Stein Warriors na Kurasini Heat zilizopanda daraja.
Hata hivyo, kati ya hizo ni Crows ndiyo iliyoshuka mwaka jana pamoja na na kuungana na Jogoo na Ukonga Kings.
“Timu zinazocheza bila mipango zinakuwa na wakati mgumu baada ya kushtuka zikiwa zimepoteza kuanzia michezo sita, kuanzia hapo timu hizo zinaanza kushinda na kufungwa,” alisema Odhiambo.
Kuhusu Ligi Daraja la Kwanza, alisema ilikuwa ngumu tofauti na watu walivyokuwa wanafikiria kutokana na ushindani uliokuwepo wa kila timu ukitafuta nafasi ya kucheza ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL).
Kwa mujibu wa Odhiambo, kikapu Dar es Salaam unakua kwa kasi kila mwaka, kuanzia Ligi Daraja la Kwanza hadi BDL.