Unguja. Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi amesema Serikali inaboresha mazingira na kuchukua hatua maalumu za kuondoa vikwazo na urasimu kwa kuweka miongozo na sera bora kuvutia uwekezaji.
Dk Mwinyi ametoa tamko hilo leo Februari 27, 2025 alipofungua kongamano la biashara la Zanzibar na Ulaya, Mjini Unguja.
Ameeleza kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni pamoja na uimarishaji na ujenzi wa viwanja vya ndege, bandari na miundombinu ya barabara ili wawekezaji wawekeze kwa matumaini na mafanikio.
“Hatua zinachukuliwa kuondoa vikwazo na urasimu, Serikali imeweka miongozo mbalimbali nia kuvutia uwekezaji mkubwa,” amesema.
Amesema Umoja wa Ulaya una mchango mkubwa na muhimu kwa maendeleo ya sekta ya uwekezaji pamoja na ustawi wa maisha ya wananchi,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amezitaja sekta sita ambazo Serikali imezipa kipaumbele katika uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji ni za uchumi wa buluu, uvuvi wa bahari kuu, utalii, mafuta na gesi, kilimo, teknolojia ya habari na mawasiliano na miundombinu ya barabara.
Dk Mwinyi amesema, Zanzibar itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya katika nyanja mbalimbali za maendeleo kwani ni mshirika muhimu katika juhudi za kukuza uchumi wa kisiwa humo.
Mbali na hilo, Dk Mwinyi ameuhakikishia umoja huo kuwa Serikali inachukua juhudi maalumu kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji, ili wawekezaji wanaokuja wawekeze katika mazingira bora na endelevu.
Awali, Jumuiya ya Ulaya (EU) pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji (Zipa) zimetiliana saini ya makubaliano (Mou) ambayo yataijengea uwezo taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake ikiwemo kutangaza uwekezaji duniani.
Akizungumza baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Balozi wa EU, Christine Grau amesema makubaliano hayo yatasaidia kujenga uwezo kwa watendaji wa mamlaka hiyo kwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi na ukusanyaji wa takwimu za uwekezaji.
”Jumuiya ya Ulaya tunataka kuona Zipa inakuwa taasisi bora yenye ufanisi katika utendaji wa majukumu yake, ikiwemo kuitangaza Zanzibar kama kituo bora cha uwekezaji duniani,” amesema Grau.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zipa, Saleh Saad Mohamed amesema wamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano na Jumuiya ya Ulaya ambayo ni miongoni mwa wadau wakubwa katika ushawishi wa biashara ya utalii na uwekezaji.