Muheza. Rekodi ya mtoto, Georgina Magesa ya kupewa fursa ya kuketi katika kiti cha Rais Samia Suluhu Hassan, imevunjwa na Esther Barua anayesoma kidato cha pili katika Shule ya Kata ya Magila wilayani Muheza, Tanga.
Hiyo ni baada ya Esther naye, kupishwa na Rais Samia ili aketi katika kiti chake, baada ya kueleza kwa kina kazi zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita, lakini kuweka wazi ndoto yake ya kuwa Rais wa Tanzania baadaye.
Kama ilivyokuwa kwa Georgina Mei 18, 2023, alipewa fursa ya kukalia kiti hicho, baada ya Rais Samia kuona kipande cha video inayomwonyesha mtoto huyo akieleza ndoto yake ya kuwa Rais wa Tanzania.
Kitendo cha Rais Samia kuwapisha watoto hao wakalie kiti chake katika matukio tofauti, kwanza kinawatanguliza mguu mmoja mbele kutimiza ndoto zao, lakini kinawahamasisha na kuimarisha ndoto walizonazo.
Georgina alipewa fursa hiyo Mei 18, 2023 katika tukio la uzinduzi wa minara ya mfumo wa urushaji wa matangazo ya televisheni ya Azam Media Limited kwa kutumia antena (DTT).
Baada ya hatua hiyo kwa mtoto Georgina, Rais Samia alisema, “ni katoto…kajukuu ka kiafrika…ambako kana mtazamo wa mbele na mtazamo mkubwa. Kameanza kazi ya kuandika vitabu kwa umri ule…Mungu amkuze…Mungu amnyooshee afike pale anapotaka.”
Tukio la mtoto Esther kukalia kiti cha Rais, limetokea leo Alhamisi, Februari 27, 2025 wilayani Muheza, katika mkutano wa Rais Samia wakati wa ziara yake mkoani Tanga.
Tukio la mtoto Esther anayesoma katika Shule ya Sekondari Magila ni tofauti kidogo na ilivyokuwa kwa Georgina.
Esther alipata nafasi hiyo, baada ya kueleza kwa lugha ya Kiingereza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita.

Katika maelezo yake hayo, Esther alionekana anayejiamini, aliyezungumza huku akionyesha ishara kwa mikono huku akiweka vituo panapostahili kupumzika.
Aliyachombeza mazungumzo yake hayo na kauli kuwa, anazungumza hayo kwa lugha ya Kiingereza kuthibitishia umma kuwa, shule za kata zinazalisha wanafunzi mahiri nchini.
Katika hitimisho la maelezo yake kwa kujiamini, amesema kwa yaliyofanywa na Rais Samia yanakonga moyo na yanamfanya atamani kuwa Rais wa Tanzania baadaye.
Baada ya maneno yake, Esther na wenzake waliitwa meza kuu na Rais Samia alimpisha mtoto huyo akaketi kwenye kiti chake, jambo lililoibua shangwe kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Hata hivyo, kilichofanywa na Esther kilitanguliwa na onyesho la watoto wengine kutoka shule mbalimbali za kata walioigiza maneno ya wakuu wa nchi wote waliowahi kuiongoza Tanzania, kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza hadi sita.
Kilichoibua shangwe zaidi katika igizo hilo ni mtoto aliyemuigiza Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, akianza kwa kuigiza kupiga simu ya kumwamrisha mmoja wa wateule wake ahudhurie mkutano ndani ya dakika tano, kama alivyokuwa akifanya mwanasiasa huyo.

Kwa mtoto aliyemwigiza hayati Ali Hassan Mwinyi, alianza kwa kutaja falsafa ya Rais huyo wa awamu ya pili ambayo ni ruksa.
Vivyo hivyo, ilikuwa kwa mtoto aliyemwigiza hayati Benjamin Mkapa, akizungumza kwa kujinasibisha na uandishi wa habari, iliyokuwa taaluma ya mwanasiasa huyo.
Kwa upande wa mtoto aliyemwigiza Jakaya Kikwete, alizungumza akiitaja iliyokuwa kauli mbiu yake ya ‘Ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.’
Mwingine alimwigiza, Rais Samia akirejea kauli mbalimbali zilizowahi kutolewa na kiongozi huyo, ikiwemo ile ya ‘ukinizingua tutazinguana.’
Alichosema Rais Samia, Mwenyekiti CCM
Katika hotuba yake, Rais Samia amewapongeza watoto hao kwa igizo walilofanya, huku akimpongeza Esther kwa kueleza utekelezaji wa miradi kwa lugha ya kigeni.
“Nilizungumza naye nikamuuliza, umepita shule ya mchepuo wa Kiingereza akasema hapana, akasema nimesoma Magila msingi na sekondari. Nikasema hayo ndio matunda ya shule za ata,” amesema.
Amesema ni imani yake kuwa, alivyo Esther kutakuwa na wanafunzi wengine wengi wa shule za kata wenye uwezo mkubwa.
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahman amesema shule za kata ni mkombozi wa elimu nchini na hii imethibitishwa na mtoto Esther.
“Wapinzani wa chama chetu wanazikejeli shule hizi kwa kuziita majina mabaya ili kuwakatisha tamaa Watanzania, nimewasihi Wanatanga shule hizi ni mkombozi, haya yametafsiriwa vyema na mtoto wetu na mjukuu wako anayesoma shule ya kata ya Magila.
“Leo Watanzania wameshuhudia kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika uboreshaji wa elimu yetu,” amesema Abdulrahman.