Tarime. Uhaba wa madawati katika Shule ya Sekondari ya Nyanungu Wilaya ya Tarime mkoani Mara unawafanya baadhi ya wanafunzi kukalia matofali darasani, huku wengine wakibeba viti kutoka nyumbani kwenda navyo shule.
Kutokana na kila mwanafunzi kuwa na kiti cha aina yake, mpangilio darasani sio maalumu hivyo wengine wanalazimika kukaa pembeni kuangalia mlangoni na kugeuza shingo ili kuangalia ubaoni na wengine kukaa uelekeo wa kuangalia ubaoni.
Wapo wenye viti vya mbao maarufu office chair, wapo wenye viti vilivyotengenezwa na mbao lakini kiasili pia wapo wenye viti vya plastiki hali ambayo kwa namna moja ama nyingine inasababisha mbanano darasani kutokana na kila kiti kuwa na ukubwa tofauti.
Hayo yamebainika leo Alhamisi, Februari 27, 2025 wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Evans Mtambi baada ya kukagua maendeleo ya miradi ya sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Kegonga katika halmashauri hiyo, ambapo amesema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Nyanungu wilayani Tarime, wanafunzi hawa wanalazimika kutoka na viti nyumbani na wengine kukalia matofali kufuatia upungufu wa madawati shuleni hapo. Picha na Beldina Nyakeke
Kutokana na adha hiyo, Mtambi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele kusimamisha malipo ya posho za vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Tarime vijijini hadi pale fedha za kutekeleza miradi ikiwamo ya ujenzi wa madarasa na ununuzi wa madawati zitakapotelewa ili kutekeleza miradi hiyo.
Pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) mkoani humo, kufanya uchunguzi juu ya mfumo na mchakato wa manunuzi wa halmashauri hiyo.
Amesema amebaini uwepo wa mapungufu mengi katika sekta ya elimu ikiwamo upungufu wa madawati huku akitolea mfano wa Shule ya Sekondari Nyanungu ambapo wanafunzi wanalazimika kukaa kwenye matofali na wengine kuja na viti kutoka nyumbani.
“Serikali kuu ilitoa zaidi ya Sh1.3 bilioni kwa ajili ya miradi miwili ya kujenga miundombinu ha shule katika Shule ya Sekondari Nyanungu pamoja na Sekondari mpya ya wa Kegonga tangu Juni 2024 lakini hadi sasa miradi yote inasuasua, hivyo kufanya yale malengo ya Serikali yasifikiwe,” amesema Mtambi.
Ameongeza mbali na fedha hizo pia halmashauri hiyo ni miongoni mwa zenye vyanzo vingi vya mapato nchini, lakini fedha hizo zimeshindwa kutumika ili kutatua changamoto hasa utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Mtambi amesema inashangaza kuona shule inakabiliwa na upungufu wa madawati wakati kila mwaka halmashauri hiyo imekuwa ikikusanya fedha zaidi ya bajeti inayotengwa, jambo ambalo amesema haikubaliki.
Amesema lengo la miradi hiyio pia ni kuwapunguzia adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 wanafunzi kutoka kijiji cha Nyandage kwenda Nyanungu Sekondari, lakini halijatimia.
” Changamoto zilizoelezwa kukwamisha miradi hiyo hazina mashiko. Hapa eti mzabuni wa vifaa vya ujenzi kama matofali ni mmoja tu ambaye anatakiwa kuyasambaza kwenye miradi yote, hii haikubaliki ina maana Tarime nzima mtu mwenye matofali ni mmoja tu, hapa kuna jambo, Takukuru hebu fanyeni kazi ili tujue ukweli,” amesema.
Amesema haiwezekeni Serikali inahangaika usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi, lakini malengo yanashindwa kufikiwa.

Awali, akitoa taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo miwili, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyanungu, Casmir Kanga amesema miongoni mwa kilichochelewesha miradi hiyo ni pamoja na kutokupatikana kwa wakati kwa vifaa vya ujenzi yakiwamo matofali.
“Pia tumekumbana na changamoto mfumo wa malipo wa nest kwani awali ulisumbua sana hali iliyolazimu miradi kuanza kutekelezwa Novemba mwaka jana, licha ya kuwa fedha ilipokelewa mapema zaidi” amesema.
Akizungumza kuhusu upungufu wa madawati Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Simon Kles amesema tayari baraza la madiwani limepitisha bajeti ya Sh200 milioni kwa ajili ya utatuzi wa changamoto hiyo, jambo ambalo mkuu huyo wa mkoa alilikataa.
“Sitaki mambo ya kwenye makaratasi na ndio maana nimekuja moja kwa moja kwenye mradi, mmepitisha fedha ziko wapi kwa nini hazitoki zije kwenye mradi, ninachotaka ni kuona wanafunzi wanakalia madawati lakini sio habari ya kutenga na kupitisha bajeti,” amesema Mtambi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Peragia Balozi amesema mapungufu yaliyopo yatafanyiwa kazi na miradi hiyo itakamilika ndani ya siku 30 kuanzia sasa.
“Mara nyingi tukitangaza zabuni, wazabuni hawajitokezi ndio maana tuliamua kumtumia mzabuni mmoja, lakini kutokana na miradi kuchelewa tunaanza rasmi kwenda kununua mahitaji kwa watoa huduma moja kwa moja,” amesema.