RC SIMIYU AZUNGUMZIA UMUHIMU WA KUTUNZA AMANI,KUSIMAMIA HAKI

Na Mwandishi Wetu,Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amesisitiza umuhimu wa wananchi kutunza amani na kama kuna changamoto au kero basi yeye pamoja na viongozi wengine wa mkoa wapo tayari kutafuta majawabu kwa njia inayostahili.

Kihongosi ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza katika Machimbo ya Ikinabushu mkoani Simiyu na kupokelewa na maelfu ya wananchi ambapo ametumia nafasi hiyo kuzungumza masuala mbalimbali na msisitizo ameuweka wa kuhimiza ushirikiano kati ya wananchi na Serikali.

“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aliponiteua kuja Simiyu amenituma kufanya mambo mawili kwanza ni kuhakikisha nasimamia haki za wanananchi ikiwa pamoja na kufanya kazi zao kwa uhuru na hiyo ndio kazi ninayoifanya Simiyu.

“Jambo la pili ni kusimamia miradi ya maendeleo ,Rais ameleta fedha Simiyu hivyo nihakikishe zinasimamiwa kikamilifu na wananchi wapate mandeleo.”

Akieleza zaidi katika mkutano huo wa hadhara ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kusikiliza kero za wananchi,Kihongosi amesema amewaomba wananchi kuweka kipaumbele suala la ushirikiano kati ya wao kwa wao lakini na Serikali.

“Niwaombe sana ushirikiano wenu ninyi kwa ninyi ukawe kipaumbele lakini ushirikiano wenu na serikali ukawe kipaumbele kingine kwasababu Serikali inawapenda na ndio maana hata hili jambo limeruhusiwa na linafanyika hapa katika machimbo.

“Rais Dk.Samia ameruhusu mfanyekazi hapa wajibu wetu sisi ni kuwasimamia mfanyekazi katika mazingira mazuri kama kuna kero kuna mambo hayaendi Mkuu wa mkoa nipo,Mkuu wa Wilaya yupo ,viongozi ndani ya kata wapo .

“Hivyo hakuna sababu ya kwenda katika vurugu,migomo au maandamano wakati Serikali ikiwepo .Kama kuna jambo mtaniambia Mkuu wa Mkoa , kuna kero yupo mkuu wa wilaya yupo ,kama kuna shida yuko diwani na viongozi wengine, hivyo hatutarajii shida au vurugu ya aina yoyote itokee,”amesema.

Ameongeza jambo jingine kubwa la kusisitiza ni kutunza amani kwani palipo na vurugu hakuna fedha kwasababu hakutakuwa na shughuli zitakazofanyika kama mtaruhusu vurugu lakini tukidumisha upendo,umoja na mshikamano maendeleo yatapatikana.Hivyo wasikubali mtu yoyote akawa chanzo cha kuvuruga amani .


 

Related Posts