Rwanda yaichongea DRC UN | Mwananchi

Geneva. Mgogoro unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umechukua sura mpya baada ya Rwanda kuishtakia Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kuwa inatekeleza mauaji dhidi ya raia.

Katika hotuba yake jana mbele ya Baraza la 58 la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UN) Geneva Uswisi, Waziri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe amesema Serikali ya Rais Tshisekedi inapandikiza chuki dhidi ya jamii na makundi kwa kigezo cha ukabila.

Nduhungirehe katika hotuba yake amesema Rwanda haihusiki katika mzozo unaoendelea Mashariki mwa DRC, badala yake ni matokeo ya chuki inayopandikizwa na viongozi wa Serikali ya DRC katuka jamii hususan ni kabila la Watutsi waishio nchini humo.

“Mashariki mwa DRC matamshi ya chuki, mateso, mauaji ya hadharani na hata vitendo vya unyama kama ulaji wa nyama za binadamu dhidi ya Watutsi wa Congo yamekuwa jambo la kawaida na la kusikitisha.Uhalifu huu dhidi ya ubinadamu unaofadhiliwa na Serikali unashuhudiwa kote DRC,” amesema Nduhungirehe.

Nduhungirehe ameenda mbali na kudai kuwa vikosi vya Jeshi la DRC kuwa vinaendesha mashambulizi dhidi ya jamii ya Kitutsi wanaoitwa ‘Banyamulenge’.

Kwa mijibu wa Waziri huyo, vikosi vya Serikali huwateka, kuwalipua kwa mabomu huku wengine wakipelekwa kusikojulikana huku akilitaja kundi la Codeco kuwa ni miongoni mwa makundi yanayotumiwa na Serikali kutekeleza unyama huo.

“Kinshasa, Watutsi wa Congo na hata wazungumzaji wa Kiswahili wanateswa na kuuawa mchana kweupe, huku kaskazini huko Ituri, mbali na mpaka wa Rwanda, kabila la Hema linachinjwa na wanamgambo wa CODECO wanaoshirikiana na Serikali ya DRC na ADF wanaoungwa mkono na Dola la Kiislamu, bila kuchukuliwa hatua yoyote,” amesema Nduhungirehe

Ameenda mbali na kumtaja, Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Wegner kuwa kauli yake ya Januari 28,2025, mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa iwapo baraza hilo halitoingilia kati basi: “mitaa itajishughulikia”, akionya kwamba: “Mtaa hauna utaratibu wala uvumilivu”.

“Na kweli baada ya hotuba yake mitaa ikajishughulikia. Kuwalenga, kuwaua, na kuwapiga Watutsi mashariki mwa DRC, pamoja na Kinshasa, kuliongezeka.
Zaidi ya mauaji haya yaliyopangwa, vijiji vya Banyamulenge huko Minembwe, Kusini mwa Kivu, vinashambuliwa kwa ndege zisizo na rubani za jeshi la Congo,” amesema waziri huyo.

“Uhalifu huu unanikumbusha kijiji cha Nturo katika eneo la Masisi, Kivu Kaskazini, ambapo nyumba 300 za Watutsi wa Congo zilichomwa moto na wanamgambo wa serikali mnamo Oktoba 2023 mchana kweupe, huku vikosi vya Burundi vikitazama tu,” amesema

Mauaji hayo yamerekodiwa vyema na yanaonyesha hali ya kutisha nchini DRC huku akisema robo ya mwisho ya mwaka 2024 pekee, Umoja wa Mataifa uliripoti kuwa vyombo vya usalama vya DRC vilihusika na zaidi ya asilimia 30 ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo yenye migogoro.

“Chini ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu, haki zote ni sawa. Hata hivyo, kuna dhahiri upendeleo katika namna jamii za Watutsi zinavyotendewa Congo. Je, Baraza hili linawezaje kunyamaza mbele ya ukosefu huu wa haki?,” alihoji waziri huyo.

Nduhungirehe amesema Serikali ya Rwanda kwa kuzingatia hiyo inatoa wito kwa Baraza la Haki za Binadamu kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukomesha mateso hayo kwa raia.

“Tunatumai kuwa tume ya hivi karibuni ya kutafuta ukweli kuhusu DRC itafanya uchunguzi wa haki juu ya ukiukwaji huu kwa kuzingatia ukweli, ambao kwa sasa unachezewa kisiasa na Serikali ya DRC kwa msaada wa nchi na mashirika yenye maslahi maalum katika eneo hili,” amesema Nduhungirehe.

Wakati, Rwanda ikitoa shutma hizo, Serikali ya Rais, Felix Tshisekedi imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwafadhiri waasi wa M23 ambao wameyateka maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Miongoni mwa Miji iliyoko mikononi mwa M23, inayoongozwa na Corneille Nangaa ni pamoja na Goma ambao ni Makao Makuu ya Jimbo la Kivu Kaskazini na Bukavu ambayo ni makao Makuu ya Jimbo la Kivu Kusini.

Waasi hao wanatajwa kuendelea kujitanua kwenda eneo la kusini Mji wa Uvira huku Nangaa akidai kuwa lengo lao ni kufika Makao Makuu ya nchi hiyo, Kinshasa na kuung’oa utawala wa Rais Tshisekedi madarakani.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts