Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Hamis Luwongo, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa, Naomi Marijani.
Uamuzi huo umetolewa jana Februari 26, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo, Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi 14 na vielelezo 10 uliotolewa mahakamani hapo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023 Hamis, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, alikuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya Naomi kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku. Inadaiwa masalia ya mwili na majivu alikwenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake.
Upande wa mashitaka ulifunga ushahidi Novemba 18, 2024 baada ya kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo tisa, huku upande wa utetezi ukiufunga Novemba 19, 2024 baada ya kumuita shahidi mmoja ambaye ni mshtakiwa mwenyewe, bila kuwasilisha kielelezo chochote.
Mshtakiwa katika utetezi alikana kumuua mkewe akidai hajafa bali alitoroka na kwamba, taarifa alizowaeleza Polisi kuwa alimuua na kuchoma moto mwili wake akazika majivu na masalia yake shambani hazikuwa za kweli.
Alidai aliwadanganya ili kujinusuru na mateso ya kipigo kutoka kwa askari polisi waliomtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.
Jaji Mwanga amesema kuna mambo matatu ambayo Mahakama inapaswa kujiuliza katika kesi ya mauaji kabla ya kitoa uamuzi ambayo ni iwapo imethibitishwa kama kweli Naomi aliuawa, iwapo kifo hicho kilikuwa si cha kawaida na kama mshtakiwa ndiye anahusika na kama alikuwa na dhamira ovu.
“Kesi hii ina mazingira tofauti kidogo na majibu yake yanatokana na mazingira hayo, ni kutokana na kutokupatikana mwili wa Naomi na kutofanyiwa ripoti ya uchungu,” amesema.
Amesema upo uamuzi wa Mahakama kuwa ushahidi wa mazingira unaweza kuthibitisha vitu bila hata mwili kufanyiwa uchunguzi wa chanzo cha kifo.
“Kosa la mauaji linaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa mazingira bila kufanyiwa postmortem na hiyo ipo hata hapa nchni katika Mahakama zetu za juu, ikiwemo Mahakama ya Rufaa.
“Uamuzi huu pia upo hata katika Mahakama ya India ambako wenzetu wanachoma miili yao, hivyo siyo lazima kuwa na mwili au ripoti ya uchunguzi ili kuthibitisha kesi za mauaji,” amesema.
Amesema hakuna ubishi kuwa kifo cha Naomi kilikuwa si cha kawaida bali kilikuwa cha mateso.
“Kama Naomi ni marehemu, basi wenye jukumu la kuthibitisha mashtaka ni upande wa mashtaka kuonyesha Hamis ndiye aliyehusika na kifo cha mkewe,” amesema.
Akichambua ushahidi na majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali aliyefanya uchunguzi wa mabaki ya mifupa amesema mabaki ya mifupa na jino la Naomi yalionyesha kutokuwa na ubora kutokana kuungua sana, licha ya kuonyesha yalikuwa ya jinsia ya kike.
Amesema maelezo ya shahidi namba 10 aliyekwenda kufanya uchunguzi wa chumba kulikofanyika mauaji ya Naomi yanafanana na ya mshtakiwa aliyotoa Polisi.
“Mshtakiwa hakuyakataa maelezo yake ya onyo yaliyotolewa mahakamani hapa na upande wa mashtaka, badala yake amekuja kuyakataa wakati upande wa mashtaka umeshafunga ushahidi akiwa anajitete akidai aliyotoa yalikuwa ya uongo, mimi nakataa,” amesema.

Jaji amesema mshtakiwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu na kueleza Naomi amepotea.
“Hivyo, haya mauaji vidole namuelekezea mshtakiwa kwa sababu kitendo alichotumia baada ya kumuua Naomi inaonyesha alidhamiria,” amesema.
Akisoma hukumu amesema kwa mujibu wa sheria, kosa la kuua kwa kukusudia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
“Kitendo cha kumkunja Naomi kwa kutumia shuka mbili na kwenda kumchoma moto katika banda la kuku na kisha eneo hilo kulisakafia, siyo cha kibinadamu na mshtakiwa alifanya kwa kudhamiria na huyu mtu apotee na ateketee.
“Ni ngumu kwa binadamu wa kawaida kufanya hivi, alipelekwa kuchunguzwa afya ya akili Hospitali ya Isanga na ripoti ya daktari ya inaonyesha mshtakiwa alifanya kosa hilo akiwa na akili timamu,” amesema.
Amesema baada ya kupitia ripoti ya daktari iliyotolewa na Hospitali ya Isanga, upande wa mashtaka umethibitisha na Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa chini ya kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Amesema Mahakama imemtia hatiani kwa ushahidi wa kimazingira, maelezo yake ya onyo na ushahidi wa mashahidi.
“Hivyo, Mahakama inakutia hatiani kwa maelezo yako ya onyo uliyoyatoa polisi na kwa mlinzi wa amani pamoja na ushahidi wa mashahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, pamoja na ushahidi wa kiamzingira, hivyo nakuhukumu kunyongwa hadi kufa,” amesema.
Awali kabla ya adhabu hiyo kutolewa, Wakili Mkuu wa Serikali, Yasinta Peter akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava waliiomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye ndoa.
Akichambua ushahidi ulitolewa na upande wa mashtaka na ule wa utetezi, Jaji Mwanga amesema mshtakiwa alikuwa na mgogoro wa muda mrefu na mkewe ambao ulisababisha Naomi kupotea.
Amesema Hamis alikwenda vituo vya Polisi na kwa ndugu wa Naomi kutoa taarifa za kupotea kwa mke wake.
“Alipokuwa katika hatua za kutoa taarifa Polisi, Hamis alipata nafasi ya kuhojiwa na polisi ambako alidai mkewe alimtumia ujumbe kuwa amekwenda nje ya nchini na kwamba, amemwambia atawajibika kulea mtoto wao mmoja waliyezaa naye,” amesema Jaji Mwanga na kuongeza:
“Hamisi pia alihojiwa na polisi kuhusu mawasiliano ya simu aliyodai kutumiwa na Naomi ambayo yalionyesha yamefanyika eneo moja.”
Amesema katika simu ya Naomi kulikuwa na ujumbe mfupi (sms) sita za maandishi ambao Hamis alimweleza askari kuwa umetumwa na mkewe.
Amesema sms hizo zilionyesha zilitumwa eneo moja, hivyo mshtakiwa alitiliwa shaka na Jeshi la Polisi.
Miezi sita baada ya tukio hilo, Julai 16, 2019 alipohojiwa Polisi, Hamis alikiri kumuua mkewe nyumbani na jinsi alivyochoma moto mwili wake na kwenda kuzika baadhi ya mifupa na majivu.
Akizungumzia kielelezo namba mbili cha upande wa mashtaka ambayo ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa aliyoyatoa Polisi na kwa mlinzi wa amani, amesema Mei 4, 2019 mshtakiwa hakulala nyumbani kwake, bali alilala kwa mwanamke mwingine (Magreth) na asubuhi alikwenda nyumbani kwa mkewe alikokuta Naomi akimuandaa mtoto kwenda shule.
“Mshtakiwa alipofika nyumbani kwake, alipitiliza ndani bila kumsalimia mkewe na muda mfupi simu yake iliita na aliyekuwa anampigia alikuwa Magreth ndipo ugomvi ulipoanzia, Naomi amwambia Hamis aendelee kutembea na malaya wake,” amesema.
“Naomi baada ya kutoa maneno hayo, Hamis alimwambi Naomi achukue kila kitu kilichopo ndani kwao kwa sababu wamekaa miaka miwili kila mtu analala chumba chake, ambapo Hamis alikuwa analala chumba cha ghorofani, huku Naomi alikuwa analala chumba cha chini,” amesema jaji akipitia kielelezo hicho.
Kutokana na majibu hayo amesema ugomvi uliibuka, ndipo Naomi alishika kwa nguvu korodani za Hamis.
Hali hiyo ilisababisha amsukume Naomi aliyejigonga ukutani na kwenye mlango wa choo ndani, kisha kuanguka chini huku damu ikiruka hadi ukutani chumbani humo.
Baada ya kuona hivyo, mshtakiwa alitoka nje na kwenda kufunga geti la nje huku akitafakari nini cha kufanya ili asibainike kuwa ameua.

Jaji Mwanga amesema kabla ya kuuchoma moto mwili wa mkewe alimpigia simu dereva wa bodaboda na kumuagiza ampelekea mafuta ya taa lita tano.
Amesema bodaboda alimpelekea na kuishia nje ya geti lake ndipo alikwenda na mafuta hayo kwenye banda la kuku akamuagiza mpwa wake achimbe shimo na kwenda kununua gunia moja la mkaa.
Pia aliagiza gunia jingine la mkaa lipelekwe nyumbani kwake, agizo ambalo lilitekelezwa na dereva wa bodaboda.
Baada ya shimo kukamilika alichukua mafuta hayo na mwili wa Naomi pamoja na viatu vilivyoharibika na kuwasha moto.
Katika maelezo yake alidai viatu vibovu huwa vinachochea moto kuwaka kwa muda mrefu lakini pia alikuwa anaficha na kuzuia harufu ya mwili wa binadamu unaochomwa usinuke wala kutoa harufu ya nyama.
“Alianza kuuchoma moto mwili huo akiwa peke yake hadi saa tisa mchana aliporudi mtoto wake kutoka shule akaenda kumnunulia chipsi,” amesema na kuongeza:
“Alichukua shuka mbili na kuufunika mwili wa Naomi na kisha kuupeleka ndani ya banda la kuku na kuuchoma moto, kisha masalia na majivu ya mwili huo akayazika shambani kwake katika Kijiji cha Marongoro wilayani Mkuranga.”
Wakili Mnzava aliiomba Mahakama mabaki ya mwili wa Naomi ambayo ni mifupa wapatiwe ndugu wa marehemu wakazike.
“Kwa asili ya kifo cha Naomi, hakupewa haki yake ya kuzikwa kama binadamu, hivyo tunaomba Mahakama iridhie mabaki ya mifupa ya Naomi wapewe ndugu zake kwa ajili ya maziko,” aliomba.
Baada ya hukumu, ndugu wa Naomi waliokuwapo mahakamani walisikika baadhi wakisema Alhamdulillah.
Kwa upande wake mdogo wa mshtakiwa, Yusta Luwongo aliangua kilio akaondolewa ndani ya ukumbi wa Mahakama.
Nje ya Mahakama, baba ndogo wa marehemu, Richard Marijan, alisema ameridhishwa na hukumu iliyotolewa. Amesema wanatarajia kuzika mabaki ya mwili wa Naomi.