Muheza. Huenda kilio cha bei ya gesi nchini kikapata suluhu baada ya Serikali kuweka wazi mikakati yake ya kuhakikisha inawapunguzia wananchi gharama ya nishati hiyo.
Mikakati hiyo kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan ni pamoja na kutoa ruzuku kwa wanaochakata gesi kuwa nishati na kuweka mazingira rafiki yatakayochochea ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli hiyo.
Serikali inaeleza mikakati hiyo, wakati bei ya mtungi wa kilo sita wa gesi uliokamilika na jiko lake ukiuzwa kati ya Sh45,000 na Sh55,000 kutegemea na kampuni husika, kwa mujibu wa wafanyabiashara wa gesi Kimara, Dar es Salaam, Majid Hussein.

Mfanyabiashara huyo, amesema bei ya kujaza gesi kwa mtungi huo wa kilo sita ni kati ya Sh23, 000 hadi Sh24, 000 kutegemea na kampuni.
Kwa upande wa mtungi wa kilo 15, amesema kujaza ni kati ya Sh57, 000 na Sh58, 000.
“Kama ndiyo unaanza, bei ya mtungi wa kilo 15 ni kati ya Sh85, 000 na Sh100, 000 kutegemea na kampuni.
Matazamio ya wengi ni kuona mkakati huo wa kupunguza bei ya gesi, unamwezesha mwananchi anaipata nishati hicho chini ya bei za soko, ili kuvutia wengi kuchana na nishati chafu na asilimia 80 ya Watanzania kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Rais Samia ameeleza mikakati hiyo, leo Alhamisi, Februari 27, 2025 baada ya kuzindua awamu ya pili ya mradi wa ugawaji wa mitungi 452,000 ya gesi kwa wananchi, alipokuwa Muheza katika mwendelezo wa ziara yake ya mkoani Tanga.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kutunga sera rafiki zitakazowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika kuwezesha nishati safi ya kupikia kupatikana kwa gharama nafuu.
“Serikali yenu itaendelea kutunga sera rafiki zitakazowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa bei nafuu,” amesema.
Mbali na hilo, amesema Serikali imeanza kutoa ruzuku kwa wachakataji wote wa gesi kuwa nishati na wanaendelea kutoa majiko ya gesi.

Ruzuku hiyo kwa mujibu wa Rais Samia, inahusisha kugharimia asilimia 50 ya bei ya mtungi wa gesi, huku mwananchi akichangia asilimia 50 kwa maeneo ya vijijini.
Kwa upande wa vijijini, amesema Serikali inatoa ruzuku ya asilimia 20, huku mwananchi akichangia asilimia 80 ya bei ya mtungi huo kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Sambamba na hilo, mkuu huyo wa nchi ameonyesha matumaini ya kufikiwa kwa lengo la asilimia 80 ya Watanzania watakaotumia nishati safi ya kupikia kabla ya mwaka 2030, licha ya matumizi hayo kwa sasa kuwa chini ya asilimia 10.
“Kwa kasi tunayoendelwa nayo, nina hakika kabla ya kufika 2034, tutakuwa tumefikia lengo tulilojiwekea kwenye mkakati wetu, hilo nina hakika,” amesema.
Amewataka wananchi waliopewa mitungi hiyo ya ruzuku, wahakikishe wanaitunza na kuendelea kuitumia badala ya kuiacha ndani baada ya gesi kuisha.
“Mlionufaika na majiko haya ya gesi wa Muheza na kokote nchini, muitumie, sio gesi ikiisha mnakaa na mitungi ndani kama pambo,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, Rais Samia amesema ameshakutana na sekta binafsi na wamemhakikishia wanafungua maeneo ya kujazia gesi ili inapoisha, wananchi hasa wa vijijini waweze kujaza nyingine.
Amesema msisitizo kwenye matumizi ya nishati safi, unalenga kulinda mazingira na afya za wananchi, hasa wanawake, ambao aghalabu hufanya shughuli za mapishi.
Amebainisha kuwa matumizi ya kuni mbali na madhara ya kiafya, pia yanawasababisha wasichana kupata ujauzito wakati wa kutafuta kuni na kuwaharibia maisha yao.
Vilevile, Rais Samia amesema wazee waliotumia kuni kwa muda mrefu, zimewaharibu macho kwa maana ya kuwa mekundu au kupata mtoto wa jicho.
Amesema gesi mchanganyiko zinazotokana na kuni zinasababisha maradhi ya kupumua na waathirika wengi wanapoteza maisha.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, Serikali inalenga kuwafanya watu wote wanaopika wawe salama.
Katika mazingira ya sasa, amesema kuni na mkaa vikiendelea kutumika kama vyanzo vya nishati, kuna hatari ya kusababisha ukame na hatimaye njaa.
Rais Samia amesema Tanzania ina gesi asilia na makaa ya nawe yanayowezesha safari ya utekelezwaji wa mkakati wa nishati safi kufanikiwa.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa REA, Advera Mwijage amesema wakala huo unatekeleza mradi wa ugawaji wa mitungi ya kilo sita awamu ya kwanza, uliotekelezwa na kampuni nne kwa Sh4.3 bilioni.
Amesema mitungi 99,350 imegawiwa kwa wananchi kupitia wabunge na kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 97.8.
Mradi mwingine, amesema unagharimu Sh8.4 bilioni kwa kusambaza mitungi 452,445 na kila wilaya itapata mitungi 3,255.
Katika mradi huo, Advera amesema mitungi inauzwa kwa bei ya punguzo, Serikali ikigharimia asilimia 50.
Kutokana na asilimia 50 ya ruzuku inayotolewa na Serikali kwa kila mtungi wa kilo sita wa gesi, mwananchi atalipa Sh17, 500, akipata mtungi, gesi, kichomeo na figa.
Mradi mwingine, amesema ni usambazaji wa majiko banifu unaotekelezwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia (WB) wenye gharama Sh15.2 bilioni na majiko 4,200 yameshatolewa.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Rais Samia amekuwa na msukumo mkubwa wa kuhakikisha malengo ya mkakati wa nishati safi ya kupikia yanapatikana.
“Uzinduzi wa mpango jumuishi utawezesha kupunguza uharibifu wa mazingira na kupunguza athari zingine za kijamii na kiafya, na kiuchumi,” amesema Kapinga.
Mbunge wa Muheza, Hamisi Mwinyijuma maarufu Mwana FA amesema katika miaka ndani ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita, wilaya hiyo imepokea Sh5.1 bilioni zilizotumika katika matumizi mbalimbali ukiwemo uboreshaji wa huduma katika hospitali ya wilaya.
Amesema uboreshaji huo umewezesha wananchi kupata huduma karibu badala ya kwenda kuzitafuta wilaya za jirani.
“Kwenye elimu Wilaya ya Muheza kata 13 hazikuwa na sekondari ila hadi sasa ni kata mbili tu zimebaki hazina. Vijii 75 kati ya 106 vimepata umeme na juhudi za kuendelea kusambaza kwenye maeneo yaliobakia lengo kila kitongoji kifikiwe,” amesema Mwana FA ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mbunge huyo amemwomba kwa Rais Samia kusaidia kupatikana kwa soko la kimataifa la Machungwa katika Wilaya ya Muheza, akisema kukosekana kwa soko kunasababisha wakulima kuuza bidhaa hiyo kwa bei isiyo na faida kwao.
“Endapo wakulima watapatiwa soko la uhakika, itasaidia kuuza mazao yao baada ya kukomaa, sambamba na kukwepa walanguzi wanaonunua machungwa yakiwa shambani,” amesema Mwana FA.
Katika hotuba yake wilayani humo, Rais Samia ameeleza namna wasanii wa muziki aliowateua katika nafasi mbalimbali – Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA na Nickson Simon maarufu Nikki wa Pili wanavyomsaidia.
Mwinjuma ni Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na Simon ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.
“Nilipomteua (Mwana FA) yeye na yule mkuu wangu wa Wilaya ya Kibaha watu hawakuelewa. Wakasema ‘mama anateua wachekwe hawa itakuwaje, hawa wamezoea majukwaa na kurap watakwenda kufanya kazi gani’,” amesema.
Amesema viongozi hao wanamsaidia kazi hasa Mwana FA, akimtaja kuwa mahiri wa lugha ya vijana iwapo Serikali inahitaji kuwaeleza jambo.
Imeandikwa na Bakari Kiango, Juma Issihaka na Rajabu Athumani