MECHI 10 zilizobaki za Simba mzimu huu zinaendelea kuwaumiza viongozi wa klabu hiyo wakipiga hesabu za namna ya kuzicheza ili wabebe ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, huku kukiwa na mambo kibao yanayowasubiri mezani kwao.
Bahati nzuri ni kwamba, katika nafasi walizopo juu kwa sasa Simba, wana nafasi kubwa ya kumaliza ndani ya top four na hivyo msimu ujao wakaendelea kukipiga katika mashindano ya kimataifa, ingawa lengo kubwa ni ubingwa wa Bara unaoshikiliwa na watani zao, Yanga, kwa sasa.
lakini, wakati mabosi wa Msimbazi wakiendelea kukuna vichwa namna ya kumalizana na beki wa kushoto na nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye mkataba alionao upo ukingoni na Yanga ikitajwa kumfukuzia, kuna taarifa mpya namna beki huyo alivyowatikisha Waarabu.
Siku chache baada ya beki huyo kutajwa katika kikosi bora cha hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, timu mbili za Kiarabu, wakiwamo watetezi wa michuano hiyo ya CAF, Zamalek ya Misri na Al Ahli Tripoli zimedaiwa zimetuma ofa kwa ajili yaa kutaka kumbeba.
Klabu hizo mbili zinadaiwa zinapigana vikumbo ili kuwania saini ya beki huyo mwandamizi wa Simba kwa ajili ya msimu ujao, kutokana na kuvutiwa na uwezo na kiwango bora alichodumu nacho kwa muda mrefu akiwa na kikosi hicho kilichotinga robo fainali ya Shirikisho Afrika.
CAF ilitoa orodha ya wachezaji 11 bora, wanaounda kikosi cha makundi kupitia mechi zilizochezwa kwa hatua hiyo Tshabalala akiwa mmoja wao sambamba na kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua na inaelezwa moto aliouwasha katika mechi sita za makundi umezivutia timu hizo za Afrika Kaskazini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Tshabalala, Carlos Sylvester ‘Mastermind’ amesema ubora wa mchezaji huyo aliyedumu kwa kiwango bora misimu zaidi ya kumi ndio siri ya ofa nyingi wanazoendelea kuzipokea, huku akisisitiza Zamalek na Al Ahli Tripoli zimemkomalia.
“Tshabalala anahesabu siku ndani ya Simba, kwani tunaendelea kupokea ofa siku hadi siku kitendo cha kutajwa kwenye orodha ya wachezaji 11 bora, wanaounda kikosi cha timu moja kutokana na mechi za hatua ya makundi nimepokea ofa nyingine kutoka Al Ahli Tripoli, Al Ittihad zote zinaulizia nafasi ya kumpata mchezaji huyo,” amesema Carlos.

“Ukiondoa timu hizo ambazo zinaendelea kutuma ofa sasa kumbuka kulikuwa na Zamalek, Kaizer Chiefs ambayo pia bado inaendelea kumfukuzia chini ya kocha, Nasreddine Nabi ambao walikuwa wanamhitaji kuanzia mwaka jana na dirisha dogo pia waliulizia uwezekano wa kumpata.”
Carlos amesema Simba walikataa kumtoa Tshabalala kwenda Kaizer Chiefs ambayo ilikubali kumsubiri kipindi atakachokuwa mchezaji huru ili kwenda kuziba pengo la mchezaji kiraka raia wa Msumbiji, Edmilson Dove aliyeumia wakati msimu unakaribia kuisha na chaguo la kwanza lilikuwa kwa Zimbwe JR.
“Kaizer Chiefs walimhitaji Tshabalala tangu mwaka jana, lakini Simba haikuwa tayari kumuachia, lakini bado haijakata tamaa sasa wanamtumia kijana waliyempandisha kutoka timu ya vijana katika eneo hilo na waliniita niende Sauzi kwa mazungumzo, ila niliwaambia wasubiri mchezaji amalize mkataba,” amesema Carlos.
“Ukimuondoa beki wa Al Ahly, Ali Maaloul, Afrika hii hakuna beki aliyecheza kwa ubora kwa misimu mitano na zaidi, siwashangai Kaizer Chiefs kuendelea kumng’ang’ania Zimbwe na wanamhitaji mchezaji huyo kwa gharama yoyote.”
Amesema hizo ni timu chache tu mara baada ya ligi kuisha vurugu zitakuwa nyingi zaidi kutoka timu mbalimbali zikimhitaji mchezaji huyo ambaye anaamini kama atachukua ubingwa na kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho atapanda zaidi thamani.
“Tshabalala akiwa ndani ya Simba amefanya kila kitu ametwaa mataji ameipeleka timu hiyo katika hatua kubwa kimataifa kwa sasa anachoakiangalia ni biashara timu ambayo itafikia makubaliano tutakayoweka mezani ndio itakayonufaika na mchezaji huyo,” amesema Carlos.
Tshabalala alijiunga na Simba mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar na amekuwa mmoja ya nyota tegemeo kwa beki ya timu hiyo, licha ya kuletwa wachezaji wanaocheza nafasi hiyo ambao walichemsha mbele yake akiwamo Gadiel Michael, Asante Kwasi, Jamal Mwambeleko na sasa akiwa na Valentin Nouma kutoka Burkina Faso.
