Tanzania na Malawi zakubaliana kuhamishiana wafungwa

Dar es Salaam. Katika kuendeleza ushirikiano muhimu wa kidiplomasia, nchi za Tanzania na Malawi zimesaini hati ya makubaliano kwenye sekta ya afya sambamba na mkataba wa kuhamisha wafungwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje, makubaliano hayo yamesainiwa Februari 26, 2025 wakati wa Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi uliofanyika jijini Lilongwe, Malawi.

Makubaliano hayo rasmi kuhusu uhamishaji wa wafungwa kati ya mataifa hayo mawili yanalenga kuweka utaratibu wa kisheria na kiutendaji ili kurahisisha mchakato wa kuwarudisha wafungwa katika nchi zao za asili, ili watumikie vifungo vyao karibu na familia zao. 

Hati hiyo ya makubaliano inahusisha masharti mbalimbali, yakiwemo vigezo vya uhamisho, haki za wafungwa,na ushirikiano wa kimahakama kati ya Tanzania na Malawi.

Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa haki za wafungwa zinalindwa na wanapata fursa bora ya kujumuika tena katika jamii zao baada ya kumaliza vifungo vyao. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyeongoza ujumbe wa Tanzania amesaini makubaliano hayo kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Nancy Tembo.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili jirani, huku yakirahisisha usimamizi wa haki za wafungwa na kuboresha mfumo wa haki jinai kwa pande zote mbili.

“Kusainiwa kwa makubaliano haya ni moja ya mafanikio ya mkutano na ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi. Taasisi na sekta husika zinapaswa kuhakikisha makubaliano yanatekelezwa kwa tija na ufanisi ili kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili,” amesema Waziri Kombo.

Nancy amepongeza hatua hiyo muhimu na kubainisha kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo ni chachu ya mabadiliko katika sekta za afya na haki za wafungwa.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo utaimarisha huduma za afya na kusaidia katika kusimamia haki za wafungwa walioko katika magereza ya mataifa hayo.

Mbali na kusainiwa kwa makubaliano hayo, mkutano pia umejadili maeneo mengine ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi, yakiwemo biashara, elimu, miundombinu, nishati na usalama wa mipaka.

Pia, wamekubaliana kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo unapaswa kufanyika kwa wakati ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa na kuongeza ushirikiano wa pande mbili kwa kiwango cha juu zaidi.

Related Posts