Dar es Salaam. Ili kuhakikisha sekta ya uchumi wa buluu inagusa maisha ya watu kwa vitendo, Serikali imeanzisha sera mpya ya uchumi wa buluu nchini iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Sera hiyo imeanzishwa ili kuhakikisha sekta hiyo mpya ambayo ndiyo uelekeo wa nchi nyingi inaongozwa kwa utaratibu wa kisera na sheria.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Februari 27, 2025 katika hafla ya kufunga mkutano wa siku nne uliowakutanisha wadau wa bahari kutoka nchi 20 duniani kujadili mpango bunifu wa ‘The BAHARI Accelerator’, unaolenga kufanikisha biashara zinazotokana na tafiti za kisayansi katika uchumi wa buluu zinaleta tija katika maisha ya watu.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uvuvi, Dk Edwin Mhede amesema awali sekta hiyo ilionekana kuwa na changamoto ya uratibu wa kisera jambo lililoisukuma Serikali kuja na sera hiyo mpya.
Amesema sera hiyo ni mwongozo wa kuelekea kutengenezwa kwa sheria, kanuni mbalimbali zinazozingatia uelekeo wa kisera.
“Hii inalenga kuhakikisha kunakuwa na tafsiri zaidi inayolenga kufanya uchumi wa buluu uende kugusa maisha ya watu,” amesema Dk Mhede.
Hilo linafanyika wakati ambao watu waliopo katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo ni takriban milioni sita na kati yao asilimia 60 ni wanawake.
Akizungumzia maazimio yaliyotolewa katika mkutano huo, Dk Mhede amesema moja wapo ni nchi zilizopo ukanda wa Afrika kukubaliana kuwapo ulazima wa kuhakikisha matokeo ya kisayansi yanayopatikana ili kuleta suluhisho kwa watu waliopo katika mnyororo wa thamani.
Hilo litawezekana kwa kuongeza uwezo wa kiufundi kwa watu ili waweze kutafsiri matokeo hayo, jambo ambalo litaenda sambamba na kuwapo kwa misingi ya kiutawala bora.
“Rasilimali ya bahari kama zilivyo nyingine lazima zisimamiwe kwa misingi ya utawala bora ambayo itafanya kuwapo kwa uendelevu wa bahari na viumbe vyake, lazima kuwe na miundo ya Serikali na taasisi zake ambazo zinaonyesha kutapatikana tija ya kiutawala kwa kuwapo mawasiliano yaliyonyooka, watu wafikiwe kwa urahisi na wafanyabiashara waweze kuwafikia watoa huduma wa umma kwa wakati ili waweze kufanya kazi kwa tija,” amesema.
Suala lingine lililojadiliwa ni kujenga mazingira yatakayovutia zaidi wanawake katika nchi mbalimbali, kwani wao ndiyo wasimamizi wakubwa wa kaya katika vyakula jambo ambalo pia litaongeza uchumi wao.
Pia, wametaka kutumika kwa sayansi ili kuondoa mtazamo wa kuwapo kwa uvuaji wa samaki kupita kiasi, huku nchi hizo zikihamasishana kuboresha vinasaba ya viumbe maji.
Akizungumzia kile ambacho Tanzania inafanya katika kuhakikisha inakuza kipato cha wavuvi amesema Serikali ilikuja na mpango wa ugawaji boti kwa wavuvi.
Amesema mwaka jana boti 160 ziligawiwa katika maeneo mbalimbali ya maziwa na baada ya tathimini ya awali ilionekana kuna uhitaji zaidi.
“tathimini hiyo ilionyesha kuongezeka kwa mchango wa sekta kutoka tani za samaki 422,000 mwaka 2022 hadi tani 522,000 Desemba mwaka jana,” amesema Dk Mhede.
Jambo hilo lilifanya Serikali kuja na awamu ya pili ya kukabidhi boti za kisasa 120 ambapo 70 zitakuwa ukanda wa mikoa ya Pwani, 29 ziwa Victoria na 21 zinakwenda Ziwa Nyasa na Tanganyika.
Akizungumzia suala la kubadilisha matokeo ya kisayansi, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Samaki (Tafiri), Dk Isamel Kimirei ameahidi kufanyia kazi maagizo waliyopewa.
“Tutahakikisha matokeo yanayotolewa yanaleta masuluhisho na kuongeza tija katika sekta hii,” amesema Dk Kimerei.